Waziri Chana afungua onesho la wiki ya ubunifu wa Italia

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi, Dkt. Pindi Chana amefungua rasmi Onesho la Wiki ya Wabunifu wa Italia linaloonesha picha za wabunifu mbalimbali wakubwa wa zamani kutoka nchini Italia na kuipongeza nchi hiyo kwa ushirikiano kati yake na Tanzania kwenye sekta ya utalii.

Ufunguzi huo umefanyika usiku wa Februari 10, 2025 katika Kituo cha Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni Jijini Dar es Salaam ambapo onesho hilo linatarajiwa kumalizika Februari 20,2025 likiwa na lengo la kukuza ushirikiano katika masuala ya utalii, historia na uchumi.

“Italia imejitolea katika juhudi zetu za kukuza utalii endelevu na kuhifadhi urithi wetu wa asili na kiutamaduni .Mfano mmoja mzuri wa ushirikiano huu ni mradi wa Kisiwa cha Bawe, ambao ni mwanzo mzuri unaoonyesha utalii endelevu. Mradi huu hauangazii tu uzuri wa visiwa vya Tanzania bali pia unaonesha matokeo chanya ya uwekezaji wa kigeni katika uchumi wetu.” amesisitiza Chana.

Aidha, amesema katika kuendeleza mahusiano hayo Tanzania na Italia zinatarajiwa kuwa na Kongamano la Biashara na Uwekezaji katika siku mbili zijazo, jijini Dar es Salaam ambalo ni jukwaa la mazungumzo, ushirikiano, na litatoa matokeo yenye manufaa kwa mataifa yetu yote mawili.

Chana amewasihi washiriki wote kutumia tukio hilo kutafiti njia mpya za ushirikiano, hasa katika nyanja za teknolojia ya kilimo, uchumi wa bluu, uchumi wa kijani, afya na dawa na viwanda vya ubunifu.

Katika hatua nyingine, Waziri Chana ameiomba Italia kuwekeza kwa vijana wa Kitanzania kwa kuunga mkono juhudi zao za ubunifu ili kutengeneza mustakabali wao ambapo Tanzania na Italia zinasherehekewa katika soko la kimataifa.

“Nchi yetu sio tu kitovu cha utalii bali pia ni shamba la uvumbuzi na ubunifu. Vijana wa Kitanzania wamejaa vipaji, na kwa usaidizi na uwekezaji unaofaa, wanaweza kuchukua nafasi yao miongoni mwa wabunifu na wavumbuzi wakuu duniani,” amesisitiza.

Naye, Balozi wa Italia nchini Tanzania, Giuseppe Coppola ameweka bayana kuwa onesho hilo ni moja ya fursa ya mashirikiano kati ya Tanzania na Italia na litasaidia pamoja na mambo mengine kufungua fursa za ajira kwa watu pamoja na kuimarisha uhusiano kati ya taasisi za nchini Italia na Tanzania.

Kwa upande wake, Kamishna wa Biashara wa Shirika la Biashara la Italia kutoka jijini Nairobi, Giuseppe Manenti amesema kuwa ni onyesho la kihistoria la heshima lenye umaridadi, ubunifu wa hali ya juu, kwa kuonyesha picha 44 za wabunifu mbalimbali wakubwa wa nchini Italia.

“Onesho hili linaadhimisha washindi wa Tuzo la Compasso d’Oro, lililotafsiriwa upya kupitia lenzi za wapiga picha wa Italia, wa kihistoria na wa kisasa. Mpango huu unalenga kuangazia upigaji picha sio tu kama zana ya hali halisi lakini pia kama njia ya ubunifu ambayo imechangia usambazaji na mafanikio ya ubunifu wa Italia” amesema Manenti.

Hafla hiyo imehudhuriwa na Viongozi mbalimbali kutoka Ubalozi wa Italia, Watendaji kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Makumbusho ya Taifa la Tanzania pamoja na baadhi ya wadau wa sekta ya utalii nchini.

spot_img

Latest articles

Ndumbaro: Sheria 300 Zimetafsiriwa kwa Kiswahili Ili Kuimarisha Uelewa kwa Wananchi

Na Tatu Mohamed WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro, amesema kuwa hadi...

Jessica: CCM inajali uongozi wa vijana

Na Mwandishi Wetu KATIBU wa Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi UVCCM TAIFA, Jessica Mshama...

Waziri Aweso: Tuna uhakika wa maji ya kutosha Dar na Pwani

Na Mwandishi Wetu WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso amewatoa hofu wakazi wa mikoa ya...

PURA yajivunia mafanikio katika Ajenda ya Nishati Safi na ushiriki wa Watanzania Sekta ya Mafuta na Gesi

Na Tatu Mohamed MAMLAKA ya Kudhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imesema inajivunia...

More like this

Ndumbaro: Sheria 300 Zimetafsiriwa kwa Kiswahili Ili Kuimarisha Uelewa kwa Wananchi

Na Tatu Mohamed WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro, amesema kuwa hadi...

Jessica: CCM inajali uongozi wa vijana

Na Mwandishi Wetu KATIBU wa Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi UVCCM TAIFA, Jessica Mshama...

Waziri Aweso: Tuna uhakika wa maji ya kutosha Dar na Pwani

Na Mwandishi Wetu WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso amewatoa hofu wakazi wa mikoa ya...