NOVEMBA 28 mwaka 1995 Rais Benjamin William Mkapa alitangaza baraza lake la kwanza la mawaziri. Rais Mkapa alikuwa ameteua mawaziri karibia wote wapya kasoro sura chache sana ambazo zilikuwamo katika baraza la mawaziri la Rais Ali Hassan Mwinyi. Mwinyi alikuwa amehitimisha utawala wake wa miaka 10 Novemba 23, 1995 siku Mkapa alipoapishwa kuwa Rais wa Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akitangaza baraza jipya la mawaziri Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Mkapa alisema serikali aliyounda ni ya awamu ya tatu na siyo mwendelezo wa serikali ya awamu ya pili. Ingawa watu wengi hawakutilia maanani sana hiyo kauli kwamba ni serikali ya awamu ya tatu na siyo mwendelezo wa awamu ya pili, ujumbe huo ulikuwa unabeba uzito mkubwa juu ya wajibu wa serikali anayounda.
Kwamba Rais Mkapa alikuwa anakusudia kuchora mpaka wa kiuwajibikaji. Kwamba sasa nchi ilikuwa chini ya uongozi mpya ambao kikatiba unabeba dhima nzima ya kuongoza taifa katika hali zote. Katika muktadha huo, yeye kama Rais Mtendaji atawajibika kwa yote yatakayofanywa na serikali yake.
Pia alitoa kauli hiyo pengine kutoa majibu kwa watu ambao wangehoji kwa mfano ni kwa nini ameacha mawaziri wengi wa serikali ya awamu ya pili. Itakumbukwa kwamba Mkapa aliwaacha mawaziri vigogo wengi kama Cleopa Msuya ambaye alishindana naye kwenye kinyang’anyiro wagombea watatu katika mkutano mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa kumchagua mgombea urais, mgombea wa tatu alikuwa ni Jakaya Kikwete. Pia aliwaacha akina Edward Lowassa, Horace Kolimba, Ernest Nyanda, Juma Hamad, Hassan Diria, Fatma Said Ally, Profesa Philemon Sarungi (ambaye hakupata jimbo la kugombea ubunge), Basil Mramba (aliyepoteza ubunge Rombo), Jaji Edward Mwisiumo na wengine wengi.
Tanzania kwa miongo sasa umejengeka utamaduni kwamba kila Rais anayeingia mdarakani, pamoja na kwamba anatokana na chama hicho hicho, anaanzisha awamu yake ya uongozi. Ni kweli ataendelea na sera za chama chake, na hata kutekeleza miradi mingine ya maendeleo iliyoanza na awamu iliyomtangulia, lakini atajipambanua kama awamu mpya.
Rais Samia Suluhu Hassan Machi 19 mwaka huu alitimiza miaka mitatu ya uongozi wake. Alichukua madaraka ya utawala wa nchi kufuatia kifo cha Rais John Magufuli. Rais Magufuli alikuwa ametawala kwa kipindi chake cha kwanza cha miaka mitano, 2015 – 2020; na ndiyo kwanza alikuwa ameanza kutumikia kipindi cha pili kuanzia 2020 -2025, lakini Mola wake akamtwaa Machi 17, 2021. Kwa hiyo awamu ya tano ya uongozi wa nchi ya JPM ilifikia tamati siku Rais SSH alipoapishwa Machi 19, 2021, hivyo kuwa mwanzo wa awamu ya sita.
Rais yeyote anapokiria na kusema wazi kwamba anaongoza awamu yake, kuna mambo makubwa anayotaka watu wajue. Moja, kwamba ndiye kiongozi mkuu wa dola kwa kipindi hicho. Kwamba mipango ya maendeleo itakayotekelezwa ni ya serikali yake pamoja na ukweli kwamba anatokana na chama kile kile cha mtangulizi wake.
Ndiyo maana kwa mfano, awamu zote za nchi hii kuanzia ya kwanza ya Mwalimu Nyerere; ya pili ya Rais Mzee Mwinyi; ya tatu ya Rais Mkapa; ya nne ya Jakaya; ya tano ya JPM na sasa ya sita ya SSH, zinatofautiana kwa vitu vingi vya msingi. Ingawa zote ni za Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katika ukweli huu, yupo kiongozi mmoja asiyetaka kabisa kutofautisha awamu hizi. Huyu anaitwa Paul Makonda. Huyu alipata kuwa Mkuu wa Wilaya, kisha akawa mkuu wa mkoa na hapa majuzi akateuliwa kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, kabla ya mwishoni mwa wiki kuteuliwa tena kuwa mkuu wa Mkoa wa Arusha.
Katika hotuba zake nyingi, hasa baada ya kupewa nafasi ya kuwa Mwenezi wa CCM, amekuwa na salamu ya kudumu, kwamba SSH na JPM ni kitu kimoja. Amekuwa anajitahidi sana kuhubiri hili jambo kwa hisia kali na kwa msukumo mkubwa mno.
Wiki iliyopita wakati Waziri Mkuu, Kassim Makaliwa, akiwa mgeni rasmi katika hafla fupi ya kupokea ndege mpya ya Kampuni ya Ndege ya Tanzania Limited (ATCL) jijini Dar es Salaam, Makonda kwa hisia kali sana alitamka tena kwamba SSH na JPM ni kitu kimoja, na alionya kwamba kuna watu wanafanya bidii ya kuwatenganisha.
Alikumbusha kwamba Rais SSH na JPM waliomba kura wote mwaka 2020, kwamba wao walikuwa wamoja na hata sasa SSH hawezi kutenganishwa na JPM. Huu umekuwa ni mradi mkubwa sana wa Makonda. Kila anapopata fursa ya kusimama anasema wazi kuwa SSH na JPM ni kitu kimoja. Ni wamoja, hawatenganishiki!
Mradi huu wa Mkonda umekuwa unanifikirisha walau katika maeneo mawili makubwa. Mosi, je, ni kweli kwamba JPM ndiyo turufu ya siasa za CCM kwa sasa hata kama hayuko tena katika ulimwengu huu? Na kwa maana hiyo, yeyote anayemtaja na kushikamana naye anakuwa amejihakikishia uhalali wa kiasiasa mbele ya umma, hasa inapokuja suala la sanduku la kura?
Pili, je, Makonda anataka kutuaminisha kubwa awamu ya sita peke yake haijitoshelezi, haitoshi, na haitatosha bila kushikamanishwa na awamu ya tano? Rais Mkapa mwaka 1995 alisema wazi, anakwenda kuunda serikali ya awamu ya tatu, siyo mwendelezo wa serikali ya awamu ya pili. Mkapa alisema hayo, akijibebesha wajibu wa kioungozi, uwajibikaji na utayari wa awamu yake kuwatumikia Watanzania kwa mujibu wa ridhaa waliyopata kwenye sanduku la kura mwaka huo.
Ukisikia tathmini ya uongozi wa miaka mitatu ya Rais SSH kwenye vyombo vya habari, kwenye mikutano ya hadhara, kwenye makongamano, kwenye mijadala bungeni kwa kifupi kila mahali, picha inayoonekana wazi ni kwamba Rais SSH amefanya makubwa. Kwa maana nyingine serikali ya awamu ya sita imefanya makubwa.
Sasa nimuulize Makonda ambaye kuanzia Alhamisi wiki hii, yaani Aprili 4. 2024 anaapishwa kuanza kutumikia wadhifa wa ukuu wa mkao wa Arusha, kwa nini anafikiri ni lazima Rais SSH atajwe pamoja na JPM? Je, Makonda haamini kwamba awamu ya sita inajitosheleza yenyewe bila msaada wa awamu ya tano?
Nijuavyo kila binadamu ana wivu na hadhi na nafasi yake katika jamii. Ana wivu zaidi hasa linapokuja suala la kutaka kutomaswa kwa njia yoyote ile madaraka aliyopewa kisheria, na hapo ndipo ninapokumbuka usemi “Huyu aliyeko hapa ni Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania ambaye umbile lake ni Mwanamke.” Kauli hii ya Rais SSH iliitoa kuhakikishia umma kwamba anatosha katika kiti cha urais, bila kujali jinsia yake.
Ni nadra sana Makonda kusimama mahali kuhutubia bila kumtaja JPM, anatamani sana JPM awe ndiye Rais mpaka sasa, hii ni bila kujali kuwa hata anayemteua kwenye nafasi hizi ni Rais SSH. Kuna nini nyuma ya ubongo wa Makonda katika mradi wake wa kutamani sana kumuungaisha SSH na JPM kila wakati?