Na Tatu Mohamed
JUMLA ya Waandishi wa Habari 64 na vyombo vya habari 11 vimefuzu hatua ya mwisho ya kuwania Tuzo za Uandishi wa Habari za Maendeleo (Samia Kalamu Awards 2026), huku washindi wakitarajiwa kutangazwa Desemba 5, mwaka huu.
Hafla ya utoaji wa tuzo hizo inatarajiwa kufanyika katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam, ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.

Orodha ya waliofuzu imetangazwa leo na Mkuu wa Idara ya Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Rolf Kibaja, katika mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika katika ofisi za mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam.
Kibaja, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Mhandisi Peter Mwasyalanda, amesema jumla ya kazi 3,003 ziliwasilishwa kuwania tuzo hizo, ambapo baada ya kufanyiwa tathmini na majaji, kazi 882 zilifuzu kuingia hatua ya kupigiwa kura na wananchi.

Amesema katika hatua ya upigaji kura, jumla ya kura 317,399 zilipigwa, huku waliofuzu hatua ya mwisho wakipatikana kupitia tathmini ya majaji 19 pamoja na kura za wananchi.
Ameeleza kuwa katika kufanya tathmini, majaji walizingatia ubora wa maudhui, uzingatiaji wa maadili ya taaluma ya habari, matumizi ya utafiti na takwimu, athari chanya kwa jamii pamoja na mchango wa kazi hizo katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Dkt. Rose Reuben, amesema uteuzi wa waliofuzu hatua ya mwisho ulizingatia ubora wa kazi zilizowasilishwa pamoja na vigezo vilivyochapishwa kwenye tovuti rasmi ya Samia Kalamu Awards 2026 wakati wa kutangaza nafasi za kushiriki.

Amesema Kamati ya Maandalizi itawapatia waliofuzu maelekezo kuhusu ushiriki wao katika hafla ya utoaji wa tuzo hizo, huku orodha kamili ya waliofuzu ikipatikana kupitia tovuti rasmi ya Samia Kalamu Awards.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Wakili Patrick Kipangula, amewashukuru Waandishi wa Habari kwa kushiriki katika mchakato huo na kuwataka kuendelea kuzingatia maadili, weledi na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao.

Amesisitiza kuwa utoaji wa taarifa sahihi kwa kuzingatia viwango vya taaluma ni muhimu katika kuimarisha imani ya jamii kwa vyombo vya habari.
Ameongeza kuwa tuzo hizo ni fursa kwa Waandishi wa Habari, Maafisa Habari na vyombo vya habari kutambuliwa na kuthaminiwa kutokana na ubora wa kazi zao zilizochapishwa au kurushwa hewani.

Samia Kalamu Awards zinaratibiwa na TCRA kwa kushirikiana na TAMWA na JAB, zikiwa na lengo la kutambua na kuhamasisha ubora, weledi na ubunifu katika uandishi wa habari za maendeleo.
Tuzo hizo zilianzishwa mwaka 2024, huku hafla ya kwanza ya utoaji wa tuzo hizo ikifanyika mwaka 2025. Msimu wa pili wa tuzo hizo una kaulimbiu isemayo “Kalamu kwa Maendeleo.”


