📌MD Twange atoa taarifa ya maendeleo ya utekelezaji wa Miradi ya kuimarisha Gridi ya Taifa.
📌Lengo ni kuhakikisha wananchi wanaendelea kunufaika na umeme wa uhakika
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI Nishati, Dkt. Juma Homera, amesema Serikali kupitia TANESCO itaendelea kutekeleza miradi ya umeme kwa lengo la kuimarisha Gridi ya Taifa sambamba na kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati ili wananchi waendelee kunufaika na umeme wa uhakika kwa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
Amesema Serikali itaendelea kuwezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo, ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kuleta matokeo yaliyokusudiwa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Dkt. Homera ameyasema hayo Novemba 16, 2026 baada ya kupokea taarifa ya maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Bw. Lazaro Twange, ikihusisha miradi ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme.

“Mikakati hii ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya kuimarisha Gridi ya Taifa, kuongeza upatikanaji wa umeme, kuvutia uwekezaji na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii nchini,” amesema Dkt. Homera.
Awali, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo katika Ofisi za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam, Twange amesema miradi hiyo inahusisha ujenzi wa njia za kusafirisha umeme pamoja na vituo vya kupokea na kupoza umeme katika mikoa mbalimbali nchini, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha miundombinu ya umeme.

Akielezea miradi ya kimkakati inayotekelezwa katika Mkoa wa Dar es Salaam, Twange amesema Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme kutoka Kimara kupitia Ubungo na Mabibo hadi Ilala, wenye urefu wa kilomita 16.5, umefikia asilimia 87.5 ya utekelezaji.
Amesema kukamilika kwa mradi huo kutaongeza uwezo wa kusafirisha umeme kutoka Kinyerezi kwenda Ilala na kuimarisha uwezo wa mfumo wa usafirishaji wa umeme katika eneo hilo.
‘’ Tunaishukuru Serikali kwa kuwezesha utekelezaji wa miradi ya umeme, kumekuwa na maendeleo mazuri ya utekelezaji wa miradi ya umeme ikiwemo ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji umeme. Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Kupokea na Kupoza Umeme cha Dege, Kigamboni, umefikia asilimia 89.4 ya utekelezaji lengo ni kuimarisha uwezo wa usambazaji wa umeme na kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii’’alieleza Twange.

Akifafanua maendeleo ya miradi mingine, Twange amesema Mradi wa Ujenzi wa Njia ya Kusafirisha Umeme kutoka Shinyanga hadi Simiyu umefikia asilimia 63.32 ya utekelezaji, huku Mradi wa Ujenzi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa Msongo wa Kilovolti 220 kutoka Songea–Tunduru , Tunduru–Masasi ukiwa umefikia asilimia 57.5.
Amesema kukamilika kwa miradi hiyo kutaiwezesha mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara kuunganishwa kikamilifu na Gridi ya Taifa, hatua itakayoongeza uhakika wa upatikanaji wa umeme katika maeneo hayo na kufungua fursa zaidi za maendeleo ya kiuchumi na kijamii.



