Na Tatu Mohamed
BENKI ya CRDB na Benki ya Maendeleo ya China (CDB) zimesaini makubaliano ya kimkakati ya ushirikiano yanayolenga kuimarisha upatikanaji wa mitaji ya muda mrefu kwa ajili ya kufadhili miradi mikubwa ya maendeleo nchini, ikiwemo miundombinu, nishati, madini na viwanda.
Makubaliano hayo yaliyosainiwa leo Novemba 05, 2026 katika makao makuu ya CRDB jijini Dar es Salaam, yanatarajiwa kufungua fursa za uwekezaji na biashara kati ya Tanzania na China, sambamba na kuunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga uchumi wa dola trilioni moja.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Dk. Abdulmajid Nsekela, amesema ushirikiano huo ni hatua muhimu ya kuunganisha mitaji ya kimataifa na mahitaji ya uwekezaji wa ndani ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

Amesema CRDB ina uzoefu wa kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta za usafiri, maji, nishati, madini, viwanja vya ndege, barabara na elimu, ikiwemo kushiriki katika ufadhili wa Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere kwa kushirikiana na taasisi nyingine za kifedha.
Dk. Nsekela amesema Benki ya Maendeleo ya China imechaguliwa kutokana na uwezo wake wa kutoa mitaji mikubwa ya muda mrefu, ambayo pia inaweza kusaidia taasisi nyingine za kifedha kupata rasilimali za kufadhili miradi ya maendeleo.
Ameeleza kuwa ushirikiano huo utajikita katika maeneo matano, ambayo ni miundombinu na nishati, madini na viwanda, kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wa kati, kurahisisha biashara na malipo ya kimataifa pamoja na uwekezaji katika nishati safi na miradi inayozingatia mazingira.

Kwa mujibu wa Dk. Nsekela, fursa nyingine zinazoweza kuendelezwa kupitia makubaliano hayo ni pamoja na ujenzi wa Kituo cha Takwimu Zanzibar na ukarabati na uboreshaji wa Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA).Amesema ushirikiano huo pia utasaidia upatikanaji wa mitaji kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati, wajasiriamali wanawake pamoja na wazalishaji na wazabuni wa ndani, ili washiriki kikamilifu katika fursa za biashara na uwekezaji.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya CRDB, Profesa Neema Mori, amesema bodi, kampuni tanzu na makundi yote ya CRDB yanaunga mkono utekelezaji wa makubaliano hayo ili kuhakikisha yanazalisha matokeo yanayotarajiwa.
Amesema ushirikiano huo utaimarisha nafasi ya CRDB katika kufadhili mahusiano ya kiuchumi kati ya Tanzania na China, akibainisha kuwa uwekezaji kati ya nchi hizo unatarajiwa kuzidi dola bilioni 12 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Naye Rais wa Benki ya Maendeleo ya China, Huang Zhiqiang, amesema Tanzania ni miongoni mwa washirika muhimu wa China barani Afrika, akieleza kuwa alichagua kuanza ziara zake za nje ya nchi kwa kutembelea Tanzania tangu aliposhika wadhifa huo miezi mitatu iliyopita.
Amesema benki hiyo iliyoanzishwa mwaka 1994 inaipa Afrika kipaumbele katika ufadhili wa miradi ya maendeleo, hususan miundombinu na uwekezaji wa muda mrefu, huku Tanzania ikiwa na nafasi muhimu katika ushirikiano huo.
Huang amesema benki hiyo inaunga mkono miradi inayotekelezwa chini ya Mpango wa Ukanda Mmoja, Njia Moja (Belt and Road Initiative), akisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kifedha kati ya China na nchi za Afrika.

Ushirikiano huo unakuja wakati biashara kati ya Tanzania na China ikitarajiwa kuvuka Sh trilioni 31 mwaka 2026, huku biashara ya madini kati ya nchi hizo ikikadiriwa kuzidi dola bilioni mbili ifikapo mwishoni mwa mwaka huo.


