Na Tatu Mohamed
MFUKO wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umeingia mikataba na watoa huduma za mawasiliano kwa ajili ya ujenzi wa minara 2,324 katika kata 2,306 zenye vijiji 5,505 nchini, hatua inayotarajiwa kuwawezesha wananchi zaidi ya milioni 32.7 kupata huduma za mawasiliano kwa uhakika.
Utekelezaji wa miradi hiyo, ambayo ina gharama ya jumla ya Sh bilioni 374, unalenga kupunguza pengo la upatikanaji wa huduma za mawasiliano, hususan katika maeneo ya vijijini ambayo hayajafikiwa na miundombinu hiyo au yenye huduma zisizo za uhakika.
Hayo yameelezwa leo Novemba 3, 2026 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Utafiti na Maendeleo wa UCSAF, Albert Richard, aliyemwakilisha Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko huo, katika kikao kazi kati ya wahariri wa vyombo vya habari na Mfuko huo, kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR).

Amesema hadi Septemba mwaka huu, tayari huduma za mawasiliano zimefika katika kata 2,053 zenye vijiji 5,185 kupitia ujenzi wa minara 2,199.
“Utekelezaji huo umewezesha wakazi 30,051,214 kunufaika na huduma za mawasiliano, huku kazi ya ujenzi ikiendelea katika kata nyingine 253 zenye vijiji 320,” amesema.
Amebainisha kuwa, katika maeneo ambayo bado yanaendelea na ujenzi, minara 251 inajengwa ili kuwafikia wakazi 2,973,121 na kuwaunganisha na huduma za mawasiliano.

Amesema pindi ujenzi wa minara yote 2,324 utakapokamilika, jumla ya wananchi 32,789,590 watanufaika na huduma za mawasiliano ya simu kwa uhakika.
“Pamoja na ujenzi wa minara, UCSAF inaendelea na mradi wa kuongeza uwezo wa minara ya mawasiliano kutoka teknolojia ya 2G kwenda 3G na 4G ili kuboresha ubora wa huduma, ambapo katika mwaka wa fedha 2024/25 minara 62 ilihusika, kati yake 37 ya Vodacom na 25 ya TTCL,” amesema.
Katika sekta ya elimu, amesema Mfuko huo umewekeza Sh bilioni 17.7 katika usambazaji wa vifaa vya TEHAMA na ujenzi wa maabara za kompyuta katika shule za umma, ambapo hadi Oktoba 2026 jumla ya shule 1,167 zilikuwa zimenufaika.

Amesema pia tangu mwaka wa fedha 2016/17, walimu 5,094 kutoka shule za msingi na sekondari za umma wamepatiwa mafunzo ya TEHAMA, wakiwemo 4,533 kutoka Tanzania Bara na 561 Zanzibar, huku walimu wengine 692 wakitarajiwa kunufaika katika mwaka wa fedha 2026/27.
Aidha, amesema UCSAF inaendelea kutekeleza mpango wa Girls in ICT Day unaolenga kuwawezesha wasichana kushiriki katika maendeleo ya teknolojia, ambapo hadi sasa wasichana 1,581 kutoka shule za sekondari za umma wamepata mafunzo hayo.

Amesema katika mwaka wa fedha 2026/27, wasichana wengine 440 wanatarajiwa kunufaika na mpango huo kupitia ushirikiano kati ya UCSAF na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Ameongeza kuwa Mfuko huo pia unaendelea kusaidia ujenzi wa vituo vya kurushia matangazo ya Redio ya Taifa (TBC), kuunganisha halmashauri kwa kutumia miundombinu ya faiba pamoja na kuwezesha huduma za intaneti katika maeneo ya wazi ili kuongeza upatikanaji wa taarifa na huduma za kidijitali kwa wananchi.



