UCSAF YAENDELEA KUPANUA WIGO WA HUDUMA ZA MAWASILIANO NCHINI

Na Tatu Mohamed

MFUKO wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umeeleza kuwa unaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kupanua huduma za mawasiliano nchini, kwa kulenga zaidi maeneo ambayo hayajafikiwa na miundombinu ya mawasiliano au yenye huduma zisizo za uhakika.

Hatua hiyo inalenga kupunguza pengo la upatikanaji wa huduma za mawasiliano, intaneti na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi kunufaika na fursa za kijamii na kiuchumi zinazotokana na teknolojia.

Hayo yameelezwa leo Novemba 3, 2026 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Utafiti na Maendeleo wa UCSAF, Albert Richard, aliyemwakilisha Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko huo, katika kikao kazi kati ya wahariri wa vyombo vya habari na Mfuko huo, kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR).

Akizungumza katika kikao hicho, Richard amesema UCSAF inaendelea kutekeleza miradi ya kuboresha upatikanaji wa huduma za mawasiliano, ikiwemo kuwezesha huduma za intaneti katika maeneo ya wazi yanayotembelewa na wananchi wengi, ili kuongeza fursa za kupata huduma za kidijitali.

Aidha, amesema Mfuko huo unaendelea na mradi wa kuongeza uwezo wa minara ya mawasiliano kutoka teknolojia ya 2G kwenda 3G na 4G, hatua inayolenga kuboresha ubora na upatikanaji wa huduma hizo.

“Kwa mwaka wa fedha 2024/25, minara 62 ilihusishwa na mpango huo, kati yake 37 ya Vodacom na 25 ya TTCL,” amebainisha.

Katika sekta ya utangazaji, amesema UCSAF imeendelea kusaidia ujenzi wa vituo vya kurushia matangazo ya Redio ya Taifa (TBC), kwa lengo la kuongeza wigo wa upatikanaji wa taarifa kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.

Ameeleza kuwa juhudi hizo pia zimeelekezwa katika sekta ya elimu, ambapo Mfuko huo unagharamia mafunzo ya TEHAMA kwa walimu wa shule za msingi na sekondari za umma.

“Tangu mwaka wa fedha 2016/17, jumla ya walimu 5,094 wamepatiwa mafunzo hayo, wakiwemo 4,533 kutoka Tanzania Bara na 561 kutoka Zanzibar,” ameeleza.

Amesema katika mwaka wa fedha 2026/27, UCSAF imepanga kuwawezesha walimu wengine 692 kupata mafunzo hayo, ambapo 592 wanatoka Tanzania Bara na 100 Zanzibar.

Katika kuwawezesha wasichana kushiriki katika maendeleo ya teknolojia, Richard amesema UCSAF pia inaendelea kutekeleza mpango wa Girls in ICT Day unaofanyika kila mwaka mwezi Aprili, ambao hadi sasa umewawezesha wasichana 1,581 kutoka shule za sekondari za umma kupata mafunzo ya TEHAMA.

Amesema kwa mwaka wa fedha 2026/27, wasichana 440 wanatarajiwa kunufaika na mpango huo kupitia ushirikiano kati ya UCSAF na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Vilevile, amesema Mfuko huo unaendelea na mradi wa kuunganisha halmashauri kwa kutumia miundombinu ya mawasiliano ya faiba, ili kuboresha mawasiliano na kurahisisha upatikanaji wa huduma za Serikali katika maeneo husika.

Katika kuimarisha matumizi ya TEHAMA mashuleni, Richard amesema UCSAF imewekeza Sh bilioni 17.7 katika usambazaji wa vifaa vya TEHAMA na ujenzi wa maabara za kompyuta katika shule za umma nchini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupunguza pengo la kidijitali na kuboresha ufundishaji na ujifunzaji.

Amesema hadi Oktoba 2026, uwekezaji huo umewezesha jumla ya shule za umma 1,167 kunufaika.

Ameeleza kuwa UCSAF itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha wananchi, hususan wale wanaoishi katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa na huduma za uhakika za mawasiliano, wanapata fursa sawa za kunufaika na maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano.

spot_img

Latest articles

AFICD YAPUNGUZA MSONGAMANO WA MALORI DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu Matumizi ya reli kusafirisha makontena kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda...

TANZANIA YATUMIA MKUTANO MKUU WA ISA INDIA KUVUTIA UWEKEZAJI WA NISHATI JUA KUFIKIA MALENGO YA DIRA 2050

📌Hatua zinazochukuliwa na Serikali kupunguza gharama za awali za uwekezaji zaelezwa Na Mwandishi Wetu TANZANIA...

NECTA YAFUTA MATOKEO YA WATAHINIWA 31 WA DARASA LA SABA

Na Tatu Mohamed BARAZA la Mitihani la Tanzania (NECTA) limefuta matokeo ya watahiniwa 31 wa...

MATENGENEZO YA BOMBA KUU KUPUNGUZA MAJI KWA SIKU NNE DAR NA PWANI

Na Mwandishi Wetu ‎‎WAKAZI wa maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam wanatarajiwa kukabiliwa na...

More like this

AFICD YAPUNGUZA MSONGAMANO WA MALORI DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu Matumizi ya reli kusafirisha makontena kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda...

TANZANIA YATUMIA MKUTANO MKUU WA ISA INDIA KUVUTIA UWEKEZAJI WA NISHATI JUA KUFIKIA MALENGO YA DIRA 2050

📌Hatua zinazochukuliwa na Serikali kupunguza gharama za awali za uwekezaji zaelezwa Na Mwandishi Wetu TANZANIA...

NECTA YAFUTA MATOKEO YA WATAHINIWA 31 WA DARASA LA SABA

Na Tatu Mohamed BARAZA la Mitihani la Tanzania (NECTA) limefuta matokeo ya watahiniwa 31 wa...