TMIC 2026 KUFUNGUA MILANGO YA UWEKEZAJI WA MADINI TANZANIA

Nchi zaidi ya 38 na Mawaziri zaidi ya 30 wanatarajiwa kushiriki mkutano huo

Utafiti wa madini, uongezaji thamani na uwekezaji kupewa kipaumbele

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde, amesema Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini (TMIC 2026) unalenga kupanua fursa za uwekezaji, kuongeza maarifa na ujuzi kwa wadau wa ndani na nje ya nchi, pamoja na kuchochea maendeleo ya sekta ya madini nchini.

Mavunde ameyasema hayo wakati wa mahojiano katika kipindi cha Morning Trumpet, kinachorushwa mubashara na kituo cha televisheni cha Azam Media, ambapo ameeleza kuwa mkutano huo utakuwa jukwaa muhimu la kuwakutanisha wawekezaji, wataalamu na wadau mbalimbali wa sekta ya madini kutoka sehemu tofauti duniani.

Amesema TMIC 2026 inatarajiwa kushirikisha wawakilishi kutoka zaidi ya nchi 38 na Mawaziri zaidi ya 30 wanaosimamia sekta ya madini katika nchi zao, hatua inayotarajiwa kufungua fursa mpya za uwekezaji, kubadilishana uzoefu na teknolojia, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa.

Ameongeza kuwa mkutano huo utakuwa na manufaa kwa wachimbaji wa madini nchini, hususan wachimbaji wadogo, kupitia upatikanaji wa maarifa, teknolojia na fursa za mitaji zitakazosaidia kuongeza tija katika shughuli zao.

Akizungumzia uongezaji thamani madini nchini, Mavunde amesema Sera ya Madini ya mwaka 2009 na Sheria ya Madini, Sura ya 123, vinaweka msingi wa kusimamia shughuli za madini, ikiwemo uongezaji thamani wa madini ndani ya nchi.

Amesisitiza kuwa kuimarisha uchakataji na uongezaji thamani madini nchini kutasaidia kuongeza ajira, kukuza kipato cha Watanzania, kuendeleza ujuzi na teknolojia, pamoja na kuhakikisha nchi inanufaika zaidi na rasilimali zake badala ya kusafirisha madini ghafi kwenda nje ya nchi.

Aidha, amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeweka msisitizo katika kukuza uchumi na kuongeza mchango wa sekta binafsi, hivyo sekta ya madini ina nafasi muhimu katika kufikia malengo ya maendeleo ya taifa kupitia uwekezaji, uzalishaji na uongezaji thamani.

Katika hatua nyingine, Mavunde amesema Serikali, chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kuimarisha utafiti wa madini kwa kuelekeza asilimia 10 ya mapato yanayokusanywa na Wizara ya Madini katika shughuli za utafiti.

Amesema hatua hiyo inalenga kuongeza eneo la nchi lililofanyiwa utafiti wa kina wa madini, ili kuwawezesha wachimbaji kupata taarifa sahihi za kijiolojia kabla ya kuwekeza katika shughuli za uchimbaji.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, Tanzania imefanyiwa utafiti wa kina wa madini kwa asilimia 16 pekee ya eneo lake, hali inayodhihirisha umuhimu wa kuongeza uwekezaji katika utafiti ili kupunguza uchimbaji wa kubahatisha, ambao unaweza kusababisha upotevu wa muda na mitaji.

Ameeleza kuwa kuongeza utafiti kutasaidia kubaini maeneo mapya yenye madini, kuongeza uzalishaji na kuvutia uwekezaji, hatua itakayochangia kukuza mchango wa sekta ya madini katika Pato la Taifa, ambao kwa sasa umefikia asilimia 10.3.

Vilevile, Waziri Mavunde ameeleza hatua mbalimbali zinazopigwa katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ya madini nchini, ikiwemo miradi ya Madini Tembo, Helium, Niobium, Kinywe, Mining for a Brighter Tomorrow na Kabanga Nickel.

Amesema miradi hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuvutia uwekezaji, kuongeza uzalishaji, kuimarisha uongezaji thamani madini na kutengeneza fursa za ajira kwa Watanzania.

Kupitia TMIC 2026 na utekelezaji wa miradi hiyo, Serikali inalenga kuimarisha nafasi ya sekta ya madini katika kukuza uchumi wa taifa, kuongeza mapato na kuhakikisha rasilimali za madini zinawanufaisha Watanzania kwa kiwango kikubwa zaidi.

spot_img

Latest articles

TTB YAZINDUA KAMPENI YA UTALII WA NDANI

Na Tatu Mohamed BODI ya Utalii Tanzania (TTB) imezindua kampeni ya CODE +255 – TWENZETU...

WAZIRI KAPINGA AKAZIA UMUHIMU WA BRELA KATIKA UBORESHAJI WA BIDHAA NA UKUAJI WA BIASHARA NCHINI

Na Tatu Mohamed WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Judith Kapinga, ameitaja Wakala wa...

LUHANGA WAPOKEA MABOMBA KUANZA KWA MRADI WA MAJI

Na Mwandishi Wetu WAKAZI wa Mtaa wa Luhanga, Kata ya Kisukuru, Wilaya ya Ilala,...

WAZIRI HOMERA AHIMIZA KASI YA UTEKELEZAJI WA MRADI UMEME SONGEA- TUNDURU NA TUNDURU- MASASI

📌Asema dhamira ya Serikali ni kuona wananchi wa kusini wananufaika na umeme wa uhakika 📌Atoa...

More like this

TTB YAZINDUA KAMPENI YA UTALII WA NDANI

Na Tatu Mohamed BODI ya Utalii Tanzania (TTB) imezindua kampeni ya CODE +255 – TWENZETU...

WAZIRI KAPINGA AKAZIA UMUHIMU WA BRELA KATIKA UBORESHAJI WA BIDHAA NA UKUAJI WA BIASHARA NCHINI

Na Tatu Mohamed WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Judith Kapinga, ameitaja Wakala wa...

LUHANGA WAPOKEA MABOMBA KUANZA KWA MRADI WA MAJI

Na Mwandishi Wetu WAKAZI wa Mtaa wa Luhanga, Kata ya Kisukuru, Wilaya ya Ilala,...