Na Tatu Mohamed
BODI ya Utalii Tanzania (TTB) imezindua kampeni ya CODE +255 – TWENZETU KUTALII, inayolenga kuwahamasisha Watanzania kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii nchini, hususan kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka.
Kampeni hiyo iliyoanza Oktoba 27, 2026, inatarajiwa kuendelea hadi Januari 15, 2027, ikishirikisha watu maarufu, watengenezaji wa maudhui ya mitandaoni na Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA) katika kutangaza vivutio vya utalii na kuhamasisha wananchi kushiriki utalii wa ndani.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 27, 2026 jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mkuu wa TTB, Dkt. Thereza Mugobi, amesema zaidi ya mabasi 400 yanatarajiwa kutumika kusambaza maudhui ya utalii kwa lengo la kuwafikia abiria wengi na kuwafahamisha kuhusu vivutio vinavyopatikana katika maeneo mbalimbali nchini.

Amesema kampeni hiyo pia itahusisha ofa na vifurushi maalumu vya safari kwa gharama nafuu ili kuwawezesha Watanzania wa makundi mbalimbali kushiriki utalii kulingana na uwezo wao wa kifedha.
Amesema kampeni hiyo haitajikita katika hifadhi za wanyamapori pekee, bali pia itatangaza fukwe, maeneo ya kihistoria, utamaduni, vyakula vya asili, sanaa na matamasha, ambavyo vina nafasi ya kuongeza kipato cha wajasiriamali na watoa huduma mbalimbali.

Makamu Mwenyekiti wa TABOA, Mbazi Mbazi, amesema chama hicho kinaunga mkono kampeni hiyo na kimejiandaa kutumia mabasi kutangaza vivutio vya utalii kupitia filamu na chaneli zinazooneshwa kwa abiria wakati wa safari.
“Tumejiandaa magari yetu yatatumika kusafirisha abiria kwenda maeneo mbalimbali yenye vivutio vya utalii, huku wananchi wakiangalia filamu. Tunafanya hivyo kwa sababu jambo hili ni la kizalendo na tupo tayari kuitangaza nchi yetu,” amesema Mbazi.

Mtengenezaji wa maudhui ya mtandaoni, Fadhil Atick, almaarufu Mr Pengo, amesema atashiriki kuandaa maudhui yatakayohamasisha Watanzania kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii nchini.

Kwa upande wake, mwigizaji Leah Mwendamseke (Lamata), amesema atatumia ushawishi alionao kuhamasisha utalii wa ndani na kuwa mfano kwa kutembelea maeneo mbalimbali yenye vivutio vya utalii.

Naye Maxwell Alfred ‘Mzee Shayo’, amesema Watanzania wanapaswa kutumia fursa ya utalii wa ndani kwa kuwa gharama za kutembelea baadhi ya vivutio ni nafuu ikilinganishwa na viwango vinavyotozwa watalii wa kigeni.Akitolea mfano, amesema kiingilio cha Sh5,900 kwa Mtanzania ni nafuu ikilinganishwa na dola 30 za Marekani, sawa na takribani Sh79,000, zinazotozwa mgeni katika kivutio alichokizungumzia.



