Na Tatu Mohamed
SHIRIKA la Madini la Taifa (STAMICO) limeongeza mapato yake ya ndani kutoka Sh bilioni 1.3 mwaka 2018/19 hadi Sh bilioni 147.8 mwaka 2025/26, mafanikio yanayotajwa kuchangiwa na mageuzi ya kiutendaji, uwekezaji katika miradi ya kimkakati na kuimarisha ushiriki wa Watanzania katika sekta ya madini.
Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. CPA Venance Mwasse, amesema hayo leo Oktoba 16, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza katika kikao kazi kati ya Shirika hilo na wahariri wa vyombo vya habari, ambapo ameeleza mafanikio yaliyopatikana na mikakati ya kuongeza mchango wa shirika katika uchumi wa taifa.
“Wakati tunaingia, mapato ya ndani ya shirika yalikuwa Sh bilioni 1.3 kwa mwaka mzima. Leo hii tunapozungumza, kwa hesabu zinazomalizika mwaka 2025/26, mapato yote ni Sh bilioni 147.8,” amesema Mwasse.

Amesema ongezeko hilo limeiwezesha STAMICO kuimarisha uwezo wake wa kujiendesha bila kutegemea fedha za Serikali kwa matumizi ya kawaida, ikiwamo kulipa mishahara ya watumishi wake kwa kutumia mapato ya ndani.
“Kwa sasa huu ni mwaka wa nne tangu tuache kutegemea Serikali, na huu ni mwaka wa tatu tunajilipa wenyewe mishahara. Tangu shirika lianzishwe mwaka 1972, tumekuwa na faida na kutoa gawio kwa Serikali, ambapo hadi sasa tumeshatoa Sh bilioni 11,” amesema.
Katika kuimarisha uzalishaji na mapato, amesema STAMICO imewekeza katika miradi mbalimbali ikiwamo uchimbaji na biashara ya makaa ya mawe, huduma za uchorongaji miamba, uzalishaji wa nishati safi ya kupikia na kuwawezesha wachimbaji wadogo.

Mwasse amesema katika shughuli za uchorongaji, shirika limeongeza mitambo ya kibiashara kutoka mitatu hadi 18, inayotumika kutoa huduma za utafiti kwa kampuni mbalimbali za uchimbaji madini.
Amesema uwekezaji huo unalenga kuimarisha uwezo wa shirika kutoa huduma za kitaalamu katika hatua za utafutaji wa madini, huku ukipanua fursa za kibiashara katika sekta hiyo.
Akizungumzia uzalishaji wa nishati safi, amesema STAMICO imeanzisha bidhaa ya Rafiki Briquettes inayotengenezwa kwa kutumia mabaki ya makaa ya mawe, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupunguza matumizi ya kuni na mkaa unaotokana na ukataji wa miti.
“Tunataka watu waache kukata miti na watumie bidhaa inayotokana na rasilimali ya kwao, ambayo ni makaa ya mawe,” amesema.
Katika miradi ya makaa ya mawe, amesema STAMICO imejipanga kuendeleza miradi ya kimkakati, ikiwamo Mchuchuma, kwa lengo la kuongeza matumizi ya rasilimali hiyo katika uzalishaji na maendeleo ya taifa.
Hata hivyo, Mwasse amesema shirika limebaini changamoto zinazowakabili, zikiwamo ukosefu wa taarifa sahihi za kijiolojia, teknolojia duni, ukosefu wa mitaji na ugumu wa kupata masoko ya madini.
“Ukichimba bila kujua madini yako wapi, utapata shida kubwa sana. Utapoteza mtaji na muda. Ndiyo maana tuliamua kuwasaidia wachimbaji wadogo kwa kuwapatia teknolojia za utafiti na kuwaunganisha na taasisi za fedha,” amesema.
Amesema STAMICO imeweka mikakati ya kuwasaidia wachimbaji hao kwa kuwapatia huduma za uchorongaji na vifaa vya utafiti, kutoa mafunzo ya kitaalamu na kuwaunganisha na taasisi za fedha na wanunuzi wa madini.Katika hatua hiyo, shirika limeingia makubaliano na benki za CRDB, NMB, Azania na KCB ili kuongeza fursa za upatikanaji wa mikopo kwa wachimbaji wadogo.

Pia linaendelea na utaratibu wa kuanzisha Benki ya Wachimbaji kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo Tanzania (FEMATA).
Aidha, STAMICO imeanzisha vituo vya mfano vya kujifunzia teknolojia bora za uchimbaji katika maeneo ya Lwamgasa, Katente na Chunya, huku ikiendelea na programu za mafunzo kwa wachimbaji wadogo.
Mwasse amesema shirika pia limeanzisha kiwanda cha kuongeza thamani ya chumvi Lingaula, mkoani Lindi, na linaendelea na taratibu za kuanzisha vituo vingine Shinyanga na Mara.
Katika uwekezaji wa kimkakati, STAMICO inashiriki katika miradi ya ubia na kampuni mbalimbali katika madini ya dhahabu, nikeli, grafiti na shaba. Miradi hiyo ni pamoja na Mgodi wa Dhahabu wa Buckreef, mradi wa Nikeli Ntaka mkoani Lindi, mradi wa dhahabu Kigosi na mradi wa grafiti Mirerani.
Akizungumzia mchango wa wachimbaji wadogo, Mwasse amesema mchango wao katika mapato yatokanayo na sekta ya madini ulifikia asilimia 40 mwaka 2021/22, akieleza kuwa hali hiyo inaonesha umuhimu wa kuwawezesha Watanzania kushiriki zaidi katika uchimbaji na uvunaji wa rasilimali zao.
Kuhusu mipango ya baadaye ya Shirika hilo, amesema STAMICO ina mkakati wa MASTASHA, unaomaanisha ‘Make STAMICO Shine Again’, unaolenga kuimarisha utendaji wa shirika na kuongeza uwekezaji katika miradi ya kimkakati, ikiwamo kuendeleza migodi mikubwa ya dhahabu na grafiti.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amelitaka shirika hilo kuendelea kuwekeza katika utafiti, ubunifu na matumizi ya takwimu za kisasa ili kuongeza tija na kuimarisha mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa taifa.

Balile amesema mafanikio ya STAMICO yanapaswa kwenda sambamba na utafiti endelevu unaozingatia mabadiliko ya teknolojia na mazingira ya biashara, badala ya kutegemea takwimu za miaka iliyopita wakati sekta inaendelea kubadilika.


