WAZIRI MKUU ASISITIZA AFRIKA KUIMARISHA USHIRIKIANO WA USAFIRI WA MAJINI

Na Tatu Mohamed

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema nchi za Afrika zinapaswa kuimarisha ushirikiano katika sekta ya usafiri wa majini kwa kuunganisha miundombinu ya bandari, reli na barabara ili kurahisisha biashara, kuongeza ajira na kukuza uchumi wa nchi wanachama.

Amesema hayo leo Oktoba 15, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akifungua rasmi Mkutano wa 10 wa Baraza la Mawaziri wa Shirika la Usafiri wa Majini la Afrika Mashariki, Kusini na Kaskazini (MOESNA), akisisitiza kuwa maendeleo ya usafiri wa majini ni muhimu katika kuunganisha masoko, maeneo ya uzalishaji na nchi za ukanda huo.

Amesema Tanzania ina nafasi muhimu katika usafirishaji wa kikanda kupitia Bandari ya Dar es Salaam, inayounganisha Bahari ya Hindi na nchi mbalimbali za Afrika, akieleza kuwa bandari hiyo ni lango la biashara linalohudumia Tanzania na nchi jirani.

“Mkutano huu ni fursa ya kutathmini utekelezaji wa maazimio ya mkutano uliopita uliofanyika Nairobi, Kenya, mwaka 2020 na kuweka mikakati mipya ya kukabiliana na changamoto za sekta ya usafiri wa majini,” amesema.

Ameeleza kuwa ajenda muhimu zinazojadiliwa ni pamoja na itifaki ya kikanda ya usafirishaji wa mizigo na abiria kwa meli, ushirikiano baina ya kampuni za usafirishaji na maandalizi ya kuanzisha Chuo Kikuu cha Kikanda cha Usafiri wa Majini kitakachokuwa kitovu cha elimu, utafiti na ubunifu katika sekta hiyo.

Amefafanua kuwa, maendeleo ya sekta hiyo yanapaswa kwenda sambamba na ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya reli na barabara ili kuhakikisha mizigo inayowasili bandarini inasafirishwa kwa ufanisi hadi maeneo ya uzalishaji na masoko.

Ametaja juhudi za Tanzania katika kuimarisha miundombinu ya usafiri kuwa ni pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR na ufufuaji wa reli ya TAZARA, ambazo zina umuhimu katika kuunganisha bandari na maeneo ya ndani ya nchi pamoja na nchi jirani.

Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema Tanzania inapokea kwa unyenyekevu na dhamira ya dhati jukumu la kuongoza ushirikiano wa kikanda katika sekta ya usafiri wa majini, akieleza kuwa maendeleo ya sekta hiyo ni msingi wa kukuza biashara, kuongeza uwekezaji, kutengeneza ajira na kuimarisha uchumi wa nchi wanachama.

“Katika kipindi cha uenyekiti wa Tanzania, msisitizo utawekwa katika kuimarisha usafirishaji wa majini, kuongeza ushiriki wa nchi za Afrika katika umiliki na uendeshaji wa meli, kuendeleza wataalamu na kukuza uchumi wa buluu,” amebainisha.

Hata hivyo, amewashukuru wajumbe na wadau waliochangia maandalizi ya mkutano huo, akieleza kuwa ushirikiano wa nchi wanachama ni muhimu katika kutimiza malengo ya pamoja ya kuendeleza sekta ya usafiri wa majini.

Naye Katibu Mkuu wa MOESNA, Kassim Mpaata, amesema takribani asilimia 88 ya biashara ya kimataifa husafirishwa kwa njia ya bahari, lakini sehemu kubwa ya shughuli hizo inadhibitiwa na kampuni za meli zinazomilikiwa na wageni.

Amesema hali hiyo inafanya nchi za Afrika kulipia gharama za usafirishaji wa bidhaa zao huku sehemu kubwa ya mapato yanayotokana na shughuli za sekta hiyo ikinufaisha wadau wa nje.

Mpaata amesema changamoto nyingine ni gharama kubwa za usafirishaji, tozo zisizo wazi, kutokuwa na uhakika wa ratiba za safari na mifumo ya udhibiti isiyolingana, hali inayopunguza ushindani wa biashara za Afrika.

Amesema MOESNA inaendelea kuhimiza nchi wanachama kuunganisha rasilimali, kubadilishana utaalamu na kuandaa mikakati ya pamoja itakayoongeza ushiriki wa Waafrika katika umiliki na uendeshaji wa meli, ujenzi na ukarabati wa meli pamoja na shughuli nyingine za mnyororo wa thamani wa usafiri wa majini.

Ameongeza kuwa ushirikiano huo unahusisha pia kuimarisha usalama wa meli, kulinda mazingira ya bahari na kuendeleza elimu na mafunzo ya wataalamu wa sekta hiyo.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema Mkoa huo una nafasi muhimu katika uchumi wa Tanzania kutokana na mchango wake katika biashara na usafirishaji wa majini.

Chalamila amesema Dar es Salaam ina wakazi wapatao milioni sita na ni kitovu muhimu cha biashara na Diplomasia, hivyo amewakaribisha wajumbe wa mkutano huo na kueleza kuwa maazimio yatakayofikiwa yanatarajiwa kuwa na manufaa kwa Watanzania na nchi nyingine wanachama.

spot_img

Latest articles

NDEJEMBI: MRADI WA TAZA KUWA CHACHU YA MAENDELEO YA KIUCHUMI MIKOA YA NYANDA ZA JUU KUSINI

📍 Akagua maendeleo ya ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme TAZA Sumbawanga na Songwe 📍...

Askofu Malasusa: Prof. Mmari alikuwa mnyenyekevu, mcha Mungu

Na Winfrida Mtoi Mkuu wa Kanisa na Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk....

TANESCO KUONGEZA UWEZO WA UPATIKANAJI WA UMEME KATAVI DISEMBA 1,2026-MD TWANGE

📌Aeleza Mpanda itakuwa na jumla ya megawati 80 na kukidhi mahitaji ya juu ya...

SERIKALI YAWASILISHA BUNGENI MKAKATI WA KUBORESHA UCHIMBAJI NA BIASHARA YA MADINI YA TANZANITE

Na Mwandishi Wetu WIZARA ya Madini imewasilisha Bungeni mkakati kabambe unaolenga kufanya mabadiliko makubwa...

More like this

NDEJEMBI: MRADI WA TAZA KUWA CHACHU YA MAENDELEO YA KIUCHUMI MIKOA YA NYANDA ZA JUU KUSINI

📍 Akagua maendeleo ya ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme TAZA Sumbawanga na Songwe 📍...

Askofu Malasusa: Prof. Mmari alikuwa mnyenyekevu, mcha Mungu

Na Winfrida Mtoi Mkuu wa Kanisa na Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk....

TANESCO KUONGEZA UWEZO WA UPATIKANAJI WA UMEME KATAVI DISEMBA 1,2026-MD TWANGE

📌Aeleza Mpanda itakuwa na jumla ya megawati 80 na kukidhi mahitaji ya juu ya...