HESLB: SH800 BILIONI ZA MIKOPO BADO HAZIJAREJESHWA

Na Tatu Mohamed

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imesema wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu wanadaiwa takribani Sh800 bilioni ambazo hazijarejeshwa, huku ikiweka mikakati ya kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa madeni hayo, hususan kwa wanufaika wanaofanya kazi katika sekta isiyo rasmi.

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk. Bill Kiwia, amesema hayo leo, Oktoba 12, 2026, katika mkutano na wahariri wa vyombo vya habari uliofanyika kwa lengo la kueleza mafanikio ya bodi hiyo katika kipindi cha miaka mitano na mwelekeo wa ufadhili endelevu wa wanafunzi wa elimu ya juu.

Amesema licha ya hatua zilizopigwa katika ukusanyaji wa mikopo, bado kuna wanufaika waliomaliza masomo ambao hawajajitokeza kurejesha fedha walizokopeshwa, hali inayohitaji juhudi zaidi za kuwafikia na kuwawezesha kutimiza wajibu wao.

Kwa mujibu wa Dk. Kiwia, kuanzia mwaka wa fedha 2005/2006 hadi Juni 2026, HESLB imekusanya Sh1.91 trilioni kati ya Sh2.77 trilioni za mikopo iliyofikia muda wa kurejeshwa, sawa na ufanisi wa asilimia 69.

Amesema katika mwaka wa fedha 2023/2024, bodi ilikusanya takribani Sh177 bilioni, huku makusanyo yakiongezeka hadi Sh194 bilioni mwaka 2024/2025.

“Katika mwaka wa fedha 2025/2026, HESLB ilikusanya Sh235.5 bilioni, sawa na asilimia 107 ya lengo la kukusanya Sh220 bilioni, ikiwa ni kiwango cha juu zaidi kuwahi kukusanywa tangu kuanzishwa kwa bodi hiyo.

Katika hatua nyingine, Dk. Kiwia amesema Serikali imetenga bajeti ya Sh1.06 trilioni kwa mwaka wa masomo 2026/2027, fedha zinazotarajiwa kugharimia wanafunzi wasiopungua 300,000.

Amesema bajeti hiyo imeongezeka kutoka Sh916.7 bilioni zilizotengwa mwaka wa masomo 2025/2026, ambapo wanafunzi 289,932 walinufaika, sawa na ongezeko la asilimia 15.6.

Akizungumzia upangaji wa mikopo kwa mwaka huu wa masomo, amesema awamu ya kwanza iliyotangazwa Oktoba 10, 2026, ilihusisha wanafunzi 165,775 waliopangiwa mikopo na ruzuku zenye thamani ya Sh535.7 bilioni.

“Katika idadi hiyo, wanafunzi 74,769 wa mwaka wa kwanza wa shahada ya awali wamepangiwa mikopo ya Sh246.88 bilioni, huku wanafunzi 8,538 wa stashahada wakipangiwa Sh22.9 bilioni. Wanafunzi 873 wamepangiwa ruzuku kupitia programu ya Samia Scholarship yenye thamani ya Sh4.5 bilioni,” amefafanua.

Kwa upande wa wanafunzi wanaoendelea na masomo, amesema 79,115 wamepangiwa mikopo ya Sh252.4 bilioni, wanafunzi 1,554 wa stashahada wamepangiwa Sh3.8 bilioni na wanufaika 926 wa Samia Scholarship wamepangiwa ruzuku ya Sh5.1 bilioni.

Amebainisha kuwa, katika kipindi cha miaka mitano, HESLB imepanua wigo wa ufadhili kwa kuanza kutoa mikopo kwa wanafunzi wa stashahada mwaka wa masomo 2023/2024, sambamba na kuongeza fedha za kujikimu kwa wanafunzi wa shahada ya kwanza kutoka Sh8,500 hadi Sh10,000 kwa siku.

“Pia, bodi imeendelea kuboresha huduma kupitia mifumo ya kidijitali ikiwemo OLAMS, SIPA, HESLB App na DiDiS, pamoja na kutumia mifumo saidizi ya akili unde inayojulikana kama Bwanaboom na Bibiboom, inayolenga kutoa majibu ya haraka kwa wanafunzi na wananchi kuhusu huduma za mikopo,” ameongeza.

Naye Mkurugenzi wa Urejeshaji na Urejeshwaji wa Mikopo wa HESLB, CPA George Mziray, amesema bodi inaendelea kuweka mifumo inayowezesha wanufaika kurejesha mikopo kulingana na uwezo wao wa kifedha, hususan wale wanaojishughulisha na sekta isiyo rasmi.

Amesema changamoto ya ajira kwa wahitimu imeifanya bodi kubuni mbinu zinazozingatia ukweli kwamba si kila mnufaika ana kipato cha uhakika kila mwezi, licha ya kuwa na uwezo wa kufanya shughuli mbalimbali za kujipatia kipato.

“HESLB inaendelea kutumia kampeni za #Fichua na #Kiduchu Fresh Tunasonga kuongeza makusanyo, huku kampeni ya #Kiduchu Fresh Tunasonga ikilenga kuwawezesha wanufaika wenye kipato kidogo kuanza kurejesha mikopo yao kwa kiasi kinacholingana na uwezo wao,” amesisitiza.

Awali Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma katika Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR), Sabato Kosuri amesema vyombo vya habari vina nafasi muhimu ya kuelimisha umma kwa kutoa taarifa sahihi kuhusu utekelezaji wa majukumu ya taasisi za umma, jambo linaloweza kuongeza uwazi, uwajibikaji na ushirikiano kati ya taasisi hizo na wananchi.

spot_img

Latest articles

Wahoo yang’ara Champion Rise Swimming Development Gala

Na Winfrida Mtoi Klabu ya mchezo wa kuogelea ya Wahoo imeibuka kinara wa mashindano ya...

SERIKALI ITAENDEA KUHIMIZA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KUIMARISHA UTENDAJI KAZI- MHE LONDO

📌SERIKALI ITAENDEA KUHIMIZA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KUIMARISHA UTENDAJI KAZI- MHE LONDOAfungua kikao cha Baraza...

MAKAMU MWENYEKITI UVCCM REHEMA SOMBI ASHIRIKI KONGAMANO LA WIKI YA VIJANA KITAIFA 2026

Na Mwandishi Wetu MAKAMU Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Rehema Sombi Omary (MNEC), ameshiriki Kongamano...

MAKAMU MWENYEKITI UVCCM REHEMA SOMBI (MNEC) APOKELEWA NKASI, AHIMIZA VIJANA KUUNGANISHA SIASA NA UCHUMI

Na Mwandishi Wetu MAKAMU Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Rehema Sombi Omary (MNEC), amepokelewa kwa...

More like this

Wahoo yang’ara Champion Rise Swimming Development Gala

Na Winfrida Mtoi Klabu ya mchezo wa kuogelea ya Wahoo imeibuka kinara wa mashindano ya...

SERIKALI ITAENDEA KUHIMIZA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KUIMARISHA UTENDAJI KAZI- MHE LONDO

📌SERIKALI ITAENDEA KUHIMIZA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KUIMARISHA UTENDAJI KAZI- MHE LONDOAfungua kikao cha Baraza...

MAKAMU MWENYEKITI UVCCM REHEMA SOMBI ASHIRIKI KONGAMANO LA WIKI YA VIJANA KITAIFA 2026

Na Mwandishi Wetu MAKAMU Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Rehema Sombi Omary (MNEC), ameshiriki Kongamano...