Na Tatu Mohamed
MFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeweka mkakati wa kuongeza idadi ya wanachama wachangiaji kutoka 2,144,906 waliopo Juni 2026 hadi 6,609,403 ifikapo mwaka 2030/31, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Nane wa Mfuko.
Aidha, NSSF inalenga kuongeza thamani ya Mfuko kutoka Sh11.42 trilioni iliyofikiwa Juni 2026 hadi Sh24.75 trilioni ifikapo Juni 2031, huku thamani ya uwekezaji ikitarajiwa kuongezeka kutoka Sh9.61 trilioni hadi Sh20.35 trilioni katika kipindi hicho.
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba, amesema hayo leo Jumatatu Septemba 21, 2026, wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu na mafanikio ya Mfuko katika mkutano na wahariri wa vyombo vya habari ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina jijini Dar es Salaam.

Amesema lengo la kuongeza wanachama hadi zaidi ya milioni 6.6 ni ongezeko la asilimia 209 kutoka idadi iliyofikiwa Juni 2026, hatua inayolenga kupanua wigo wa hifadhi ya jamii nchini.
“Katika Mpango Mkakati wetu wa Nane, tunalenga kuongeza idadi ya wanachama wachangiaji hadi 6,609,403 ifikapo mwaka 2030/31. Hili ni ongezeko kubwa ambalo linakwenda sambamba na jitihada za kupanua wigo wa hifadhi ya jamii nchini,” amesema Mshomba.
Amesema NSSF imejenga msingi wa kufikia lengo hilo kutokana na ukuaji wa idadi ya wanachama katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020/21 hadi 2025/26, ambapo wanachama wachangiaji waliongezeka kwa asilimia 130 kutoka 932,112 hadi 2,144,906.
“Katika kipindi hiki tumeweza kuandikisha wanachama wapya 1,486,930. Ongezeko hili limechangiwa na mazingira ya biashara kuendelea kuboreshwa, kuongezeka kwa uwekezaji na ajira, pamoja na mikakati mbalimbali ya Mfuko katika kuongeza uandikishaji wa wanachama,” amesema.
Mshomba amesema katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Nane, NSSF inalenga pia kukusanya michango yenye thamani ya Sh21.12 trilioni na kupata mapato ya uwekezaji ya Sh5.28 trilioni katika kipindi cha Julai 2026 hadi Juni 2031.

“Tunatarajia pia kuongeza thamani ya Mfuko kutoka Sh11.42 trilioni tuliyofikia Juni 2026 hadi Sh24.75 trilioni ifikapo Juni 2031,” amesema.
Amesema malengo hayo yanatokana na mwenendo wa ukuaji wa Mfuko katika kipindi kilichopita, ambapo thamani ya vitega uchumi iliongezeka kwa asilimia 108 kutoka Sh4.62 trilioni mwaka 2020/21 hadi Sh9.61 trilioni mwaka 2025/26.
Kwa upande wa makusanyo ya michango, amesema nayo yaliongezeka kwa asilimia 147 kutoka Sh1.17 trilioni mwaka 2020/21 hadi Sh2.90 trilioni mwaka 2025/26.
“Ongezeko la makusanyo limechangiwa na kuongezeka kwa wanachama, kuimarika kwa mazingira ya ufanyaji biashara, mwitikio wa waajiri pamoja na maboresho ya mifumo ya ukaguzi na ufuatiliaji wa michango,” amesema.
Mshomba amesema NSSF pia itaendelea kupanua wigo wa hifadhi ya jamii kwa kuwafikia wananchi waliojiajiri, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuongeza idadi ya Watanzania wanaonufaika na huduma za hifadhi ya jamii.
“Februari 2026 tulizindua Skimu ya Hifadhi ya Jamii kwa wananchi waliojiajiri. Lengo ni kuwawezesha nao kupata huduma za hifadhi ya jamii kama ilivyo kwa walio katika ajira rasmi,” amesema.
Amesema skimu hiyo inahusisha makundi mbalimbali yakiwamo wakulima, wavuvi, waendesha bodaboda na bajaji, mamalishe na babalishe, wachimbaji wadogo wa madini, machinga na makundi mengine ya waliojiajiri.
“Hadi Juni 30, 2026 tulikuwa na wanachama 592,791 katika skimu hii na katika mwaka wa fedha 2026/27 tunalenga kuandikisha wanachama wapya 279,371,” amesema.
Kwa upande wa mafao, Mshomba amesema NSSF itaendelea kuhakikisha ukuaji wa Mfuko unaenda sambamba na kuboresha huduma na mafao kwa wanachama.
Amesema katika kipindi cha 2020/21 hadi 2025/26, malipo ya mafao yaliongezeka kutoka Sh594.33 bilioni hadi Sh1.16 trilioni, sawa na ongezeko la asilimia 96.

“Tumeboresha kiwango cha mkupuo kutoka asilimia 25 hadi asilimia 35, wakati kiwango cha chini cha pensheni ya kila mwezi kimeongezeka kutoka Sh100,000 hadi Sh150,000,” amesema.
Amesema NSSF pia imeendelea kutumia teknolojia katika kuboresha huduma, hatua ambayo imewawezesha wanachama na waajiri kupata baadhi ya huduma bila kufika katika ofisi za Mfuko.
“Tumeboresha mifumo yetu ya TEHAMA na hatua hii imeongeza ufanisi wa utoaji huduma na kupunguza malalamiko ya wateja. Kwa sasa asilimia 99 ya madai ya mafao yaliyofunguliwa yanalipwa ndani ya muda wa kisheria wa siku 60,” amesema.
Akizungumzia uwekezaji, Mshomba amesema miradi mbalimbali ya Mfuko imeendelea kuchangia katika uchumi wa nchi, ikiwamo Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi na Daraja la Nyerere Kigamboni.
Amesema Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi katika misimu miwili ya uzalishaji kimetengeneza tani 45,594 za sukari ya majumbani na tani 256 za sukari ya viwandani, huku kikifikisha faida ya Sh4.56 bilioni katika mwaka wa fedha 2025/26.
“Uwekezaji huu unatarajiwa kurejesha fedha zilizowekezwa ndani ya miaka saba baada ya kuanza uzalishaji. Pia umetoa ajira 2,172 za moja kwa moja na zaidi ya 8,000 zisizo za moja kwa moja,” amesema.
Kwa upande wa Daraja la Nyerere Kigamboni, amesema NSSF imekusanya Sh150.04 bilioni kutokana na tozo za matumizi ya daraja hilo hadi Juni 2026, huku Sh25.81 bilioni zikitumika kwa gharama za uendeshaji na matengenezo tangu lilipoanza kutumika Mei 2016.
Hata hivyo, Mshomba amesema pamoja na mafanikio hayo, bado kuna changamoto zinazohitaji kushughulikiwa ili kufikia malengo yaliyowekwa katika Mpango Mkakati wa Nane.
Ametaja baadhi ya changamoto kuwa ni ukiukwaji wa taratibu za usajili wa wanachama na uwasilishaji wa michango kwa baadhi ya waajiri, pamoja na uelewa mdogo wa umuhimu wa mafao ya pensheni.
“Bado tunakutana na changamoto ya baadhi ya wanachama kuchukua michango yao baada ya ajira kukoma na hivyo kukosa sifa za kupata pensheni ya uzee. Pia mwitikio wa baadhi ya Watanzania waliojiajiri kujiunga na kuchangia katika mifumo ya hifadhi ya jamii bado ni mdogo,” amesema.


