TANZANIA YAZIDI KUIMARISHA NAFASI YAKE KATIKA BIASHARA YA UMEME KIKANDA

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

TANZANIA imeendelea kuimarisha nafasi yake katika biashara ya umeme kikanda, huku Mradi wa Kuunganisha Gridi za Umeme Tanzania na Zambia ukifikia asilimia 90 ya utekelezaji na kutarajiwa kukamilika Februari 2027, hatua itakayoiunganisha Tanzania na soko la umeme la Kusini mwa Afrika na kuongeza fursa za biashara ya umeme kuvuka mipaka.

Akizungumza, Septemba 11, 2026, katika ufunguzi wa Mkutano wa 67 wa Kamati ya Usimamizi ya Jumuiya ya Umeme ya Kusini mwa Afrika (SAPP), Naibu Waziri wa Maji, Nishati na Madini wa Zanzibar, Mhe. Seif Kombo, amesema kuimarisha biashara ya umeme kuvuka mipaka ni muhimu katika kuongeza upatikanaji wa nishati, kuimarisha usalama wa gridi na kupunguza gharama za umeme katika ukanda huo.

Ameeleza kuwa Tanzania, kupitia Serikali na TANESCO, inaendelea kuwekeza katika kuimarisha miunganisho ya gridi, ikiwemo Mradi wa Tanzania-Zambia wa msongo wa kilovoti 400 ambao, utakapokamilika, utaongeza uwezo wa Tanzania kushiriki katika biashara ya umeme ndani ya SAPP.

“Kuimarisha biashara ya umeme kuvuka mipaka kutaziwezesha nchi kutumia kikamilifu rasilimali za nishati zilizopo, kuongeza upatikanaji wa umeme na kuimarisha usalama wa gridi,” amesema Mhe. Kombo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi ya SAPP, Andrew Etzinger, amesema ushirikiano wa kikanda ni muhimu katika kuimarisha usalama wa nishati, hususan wakati mabadiliko ya tabianchi, ukame na matukio ya hali ya hewa yanapoendelea kuathiri mifumo ya uzalishaji wa umeme.

Amesema kukamilika kwa muunganisho wa Tanzania na Zambia kutakuwa hatua muhimu katika kuunganisha SAPP na Jumuiya ya Biashara ya Umeme Mashariki mwa Afrika (EAPP), hivyo kupanua wigo wa ushirikiano na biashara ya umeme kati ya nchi za Afrika Mashariki na Kusini.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Usafirishaji Umeme wa TANESCO, Mha. Zakaria Mgalama, amesema mkutano huo umetoa fursa kwa nchi wanachama na wadau wa sekta ya umeme kujadili namna ya kuimarisha biashara ya umeme, miundombinu na usalama wa nishati katika ukanda huo.

“Kwa Tanzania, kukamilika kwa Mradi wa Tanzania-Zambia kutakuwa hatua muhimu katika kuongeza uwezo wa nchi kushiriki kikamilifu katika biashara ya umeme ya kikanda, ikiwemo kuuza umeme katika masoko ya nchi wanachama wa SAPP,” amesema Mha. Mgalama.

Muunganisho huo pia utaimarisha nafasi ya Tanzania katika mtandao mpana wa biashara ya umeme unaounganisha Afrika Mashariki na Kusini, na kuongeza fursa za matumizi bora ya uwezo wa uzalishaji na miundombinu ya umeme iliyopo.

Mikutano ya 67 ya SAPP, iliyofanyika Zanzibar kuanzia Septemba 7 hadi 11, 2026, imejadili masuala ya mipango ya mifumo ya umeme, miundombinu ya usafirishaji, biashara ya umeme na hatua za kuimarisha usalama wa nishati katika ukanda wa Kusini mwa Afrika.

spot_img

Latest articles

MAAMBUKIZI MAPYA YA VVU YAPUNGUA KUTOKA 98,754 HADI 33,511

Na Tatu Mohamed MAAMBUKIZI mapya ya Virusi vya Ukimwi (VVU) nchini yamepungua kutoka watu 98,754...

MRADI WA UPANUZI WA KITUO CHA KUPOZA UMEME DEGE KUIMARISHA HALI YA UPATIKANAJI WA UMEME KIGAMBONI

📌Wafikia Asilimia 90 katika utekelezaji wake 📌 Kukamilika Mwisho wa Mwezi Disemba 2026 Na Mwandishi Wetu...

GBT yaikaribisha BetSasa sokoni, yaitaka kuzingatia maadili

Na Mwandishi Wetu MKURUGENZI Mkuu wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha (GBT), James Mbalwe ameikaribisha...

DKT. YONAZI AHIMIZA UIMARISHWAJI WA MIFUMO YA KITAASISI YA UFUATILIAJI NA TATHMINI NCHINI

Na Mwandishi Wetu- Morogoro. KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge Uratibu na Wenye...

More like this

MAAMBUKIZI MAPYA YA VVU YAPUNGUA KUTOKA 98,754 HADI 33,511

Na Tatu Mohamed MAAMBUKIZI mapya ya Virusi vya Ukimwi (VVU) nchini yamepungua kutoka watu 98,754...

MRADI WA UPANUZI WA KITUO CHA KUPOZA UMEME DEGE KUIMARISHA HALI YA UPATIKANAJI WA UMEME KIGAMBONI

📌Wafikia Asilimia 90 katika utekelezaji wake 📌 Kukamilika Mwisho wa Mwezi Disemba 2026 Na Mwandishi Wetu...

GBT yaikaribisha BetSasa sokoni, yaitaka kuzingatia maadili

Na Mwandishi Wetu MKURUGENZI Mkuu wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha (GBT), James Mbalwe ameikaribisha...