Na Mwandishi Wetu
CHUO Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimebuni mfumo wa kidijitali unaowezesha wakulima kufuatilia ubora wa mazao yao baada ya kuvuna, hatua inayolenga kupunguza upotevu wa mazao, kuongeza thamani ya mazao yanayohifadhiwa na kuimarisha kipato cha wakulima.
Akizungumza katika Maonesho ya Kitaifa ya Wakulima ‘Nanenane’ yanayoendelea jijini Dodoma, Mhadhiri Msaidizi kutoka UDOM, Jospeter Jonathan, amesema ubunifu huo umetokana na changamoto ya wakulima wengi kupoteza sehemu ya mazao yao wakati wa kuhifadhi kutokana na kushindwa kubaini mapema mabadiliko yanayotokea ndani ya maghala au vihenge.

Amesema mfumo huo hukagua ubora wa mazao yanapoingizwa kwenye hifadhi kwa kupima hali yake, ikiwemo unyevunyevu na viashiria vinavyoweza kusababisha kuharibika kwa mazao, kisha huendelea kuyafuatilia kila siku hadi yatakapouzwa.
“Mfumo huu unampa mkulima taarifa kila siku kuhusu hali ya mazao yake. Ukibaini kuna wadudu, unyevunyevu mkubwa au changamoto nyingine, mfumo unatoa tahadhari na kuelekeza hatua zinazopaswa kuchukuliwa mapema kabla hasara haijatokea,” amesema.
Ameongeza kuwa, ubunifu huo utawasaidia wakulima kuhifadhi ubora na uzito wa mazao yao kwa muda mrefu, tofauti na ilivyo sasa ambapo baadhi yao hupoteza sehemu ya mazao kutokana na wadudu, unyevunyevu au mazingira yasiyofaa ya uhifadhi.
“Mkulima anayehifadhi magunia 10 analenga kuuza magunia hayo hayo yenye ubora uleule. Mfumo wetu unamsaidia kuhakikisha mazao yake yanabaki katika kiwango alichokusudia na kumpunguzia hasara zinazotokea baada ya kuvuna,” amesema.
Amefafanua kuwa, wakati wa kubuni teknolojia hiyo, watafiti wa UDOM walishirikiana na wadau wa sekta ya kilimo ili kubaini changamoto zinazowakabili wakulima katika hatua ya uhifadhi wa mazao, jambo lililowasaidia kuandaa suluhisho linalokidhi mahitaji halisi ya watumiaji.

Mbali na sekta ya kilimo, amesema UDOM pia imebuni kifaa kinachoitwa Maxwell Track Device, kinacholenga kuboresha usalama wa usafirishaji na kurahisisha ushughulikiaji wa madai ya bima za magari.
Amesema kifaa hicho hufuatilia mwenendo wa gari wakati wote, ikiwemo kasi, namna lilivyoendeshwa na taarifa za ajali endapo itatokea, hivyo kutoa ushahidi sahihi kwa kampuni za bima na mmiliki wa gari.
“Kifaa hiki kinafanya kazi kama ‘black box’ ya ndege. Kinarekodi taarifa zote muhimu kuhusu safari ya gari, hivyo ajali inapotokea kampuni ya bima na mmiliki wa gari wanakuwa na taarifa sahihi zinazorahisisha uchunguzi na kuharakisha malipo ya madai ya bima,” amesema.
Ameongeza kuwa ubunifu huo unapunguza migogoro inayoweza kujitokeza kati ya kampuni za bima na wateja kutokana na ukosefu wa taarifa sahihi kuhusu chanzo cha ajali.
UDOM imetumia Maonesho ya Nanenane kuonesha ubunifu huo ikiwa ni sehemu ya jitihada za kutumia teknolojia kutatua changamoto katika sekta za kilimo, usafirishaji na huduma za bima, huku ikiwahimiza wadau kushirikiana na taasisi za elimu ya juu katika kuendeleza bunifu zinazochochea maendeleo ya uchumi.


