EWURA: Ukaguzi wa mifumo ya umeme kila baada ya miaka mitano unaweza kuzuia majanga ya moto

Na Mwandishi Wetu

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imewataka wananchi kujenga utamaduni wa kukagua mifumo ya umeme majumbani kila baada ya miaka mitano, ikisema hatua hiyo inaweza kubaini mapema hitilafu zinazoweza kusababisha moto, uharibifu wa mali na hata kupoteza maisha.

Akizungumza katika Maonesho ya Kitaifa ya Wakulima ‘Nanenane’ yanayoendelea jijini Dodoma, Meneja wa EWURA Kanda ya Kati, Hawa Lweno, amesema wananchi wengi huamini mfumo wa umeme hubaki salama baada ya kufungwa, jambo ambalo si sahihi.

“Kupata cheti cha usalama wakati mfumo wa umeme unapofungwa haimaanishi kuwa utakuwa salama maisha yote. Tunashauri mfumo ukaguliwe tena kila baada ya miaka mitano na fundi mwenye leseni ili kubaini mapema hitilafu zinazoweza kusababisha moto,” amesema.

Amebainisha kuwa, nyaya zilizochakaa, vifaa vilivyoharibika au mabadiliko ya matumizi ya umeme ndani ya nyumba ni baadhi ya sababu zinazoweza kuongeza hatari ya moto ikiwa ukaguzi wa mara kwa mara hautafanyika.

Mbali na umeme, EWURA pia imewataka wananchi kuzingatia matumizi salama ya gesi ya kupikia (LPG) kwa kuhakikisha mitungi inawekwa sehemu zenye hewa ya kutosha na vifaa vyake, ikiwemo regulator na jiko, vinakuwa katika hali nzuri.

“Baada ya kutumia gesi hakikisha unazima jiko na regulator. Pia ni muhimu kila anayehusika na matumizi ya gesi nyumbani apewe elimu ya matumizi salama ili kupunguza ajali zinazoweza kuepukika,” amesema.

Ameongeza kuwa mtungi mpya wa gesi unapaswa kuachwa kwa dakika 15 hadi 20 kabla ya kuanza kutumika ili kuruhusu gesi kutulia na kuongeza usalama wakati wa matumizi.

Katika sekta ya maji, Lweno amewataka wananchi kukagua mara kwa mara mabomba ya ndani ya nyumba ili kubaini uvujaji wa maji unaoweza kuongeza matumizi na bili zisizo za lazima.

“Kabla ya kudhani bili imeongezeka kutokana na kosa la usomaji wa mita, kwanza hakikisha hakuna uvujaji wa maji katika mfumo wa mabomba ya nyumba yako. Pia fuatilia usomaji wa mita kila unapofanyika,” amesema.

Amesema EWURA inaendelea kutumia Maonesho ya Nanenane kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi salama ya huduma za umeme, gesi na maji pamoja na haki na wajibu wa watumiaji wa huduma hizo.

Kwa mujibu wa Lweno, wananchi wameendelea kujitokeza kwa wingi kutembelea banda la EWURA, ambapo zaidi ya watu 600 walikuwa wamepata elimu kuhusu usalama wa matumizi ya nishati na maji tangu kuanza kwa maonesho hayo.

Amewahimiza wananchi kuendelea kutafuta elimu kutoka EWURA ili kuongeza usalama wa familia zao, kulinda mali na kuhakikisha matumizi bora ya huduma za nishati na maji.

spot_img

Latest articles

Msajili wa Hazina ateta na Rais wa Benki ya Biashara na Maendeleo

Na Mwandishi Wetu MSAJILI wa Hazina, Nehemiah Mchechu, amekutana na kufanya mazungumzo na Rais...

MHANDISI SWEDI: NANENANE NI FURSA YA KUIMARISHA SEKTA YA MADINI

Na Mwandishi Wetu KAIMU Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Aziza Swedi, amesema...

Mfumo wa T-CAMS ni Mageuzi ya Kidijitali Yanayojenga Uwazi, Ufanisi na Ushindani katika Sekta ya Uwakala wa Forodha Tanzania

Na Mwandishi Wetu KATIKA dunia ya sasa, ushindani wa biashara haupimwi tena kwa ukubwa...

TBA yafungua fursa za uwekezaji katika miundombinu ya kilimo na biashara

Na Mwandishi Wetu, Dodoma WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA) umewataka wawekezaji wa sekta binafsi kutumia...

More like this

Msajili wa Hazina ateta na Rais wa Benki ya Biashara na Maendeleo

Na Mwandishi Wetu MSAJILI wa Hazina, Nehemiah Mchechu, amekutana na kufanya mazungumzo na Rais...

MHANDISI SWEDI: NANENANE NI FURSA YA KUIMARISHA SEKTA YA MADINI

Na Mwandishi Wetu KAIMU Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Aziza Swedi, amesema...

Mfumo wa T-CAMS ni Mageuzi ya Kidijitali Yanayojenga Uwazi, Ufanisi na Ushindani katika Sekta ya Uwakala wa Forodha Tanzania

Na Mwandishi Wetu KATIKA dunia ya sasa, ushindani wa biashara haupimwi tena kwa ukubwa...