Na Mwandishi Wetu
TANZANIA imepata ahadi za kifedha na fursa za uwekezaji zenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 4.7 (takribani Sh12.2 trilioni) kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo nishati safi ya kupikia, nishati jadidifu, uhifadhi wa mazingira na kuimarisha ustahimilivu wa jamii dhidi ya athari za tabianchi.
Fedha hizo ni miongoni mwa manufaa yaliyopatikana kupitia Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP31), uliofanyika Antalya, nchini Uturuki, Novemba 9 hadi 20, 2026.
Akizungumza kuhusu matokeo ya ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, amesema ahadi hizo zimetolewa na taasisi za kimataifa, washirika wa maendeleo na nchi mbalimbali, huku fedha hizo zikitarajiwa kupatikana kwa vipindi tofauti kulingana na taratibu za ufadhili.

Amesema ushiriki wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan umeiwezesha Tanzania kupata fursa hizo, ambazo zinaendana na vipaumbele vitatu alivyovitaja katika hotuba yake ya Novemba 11, mwaka huu, ambavyo ni upatikanaji wa fedha za tabianchi, mpito wa haki wa nishati na maendeleo jumuishi yanayozingatia ustahimilivu wa mazingira kwa mujibu wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Masauni amesema katika eneo la nishati safi ya kupikia, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imeahidi Dola milioni 54 kwa ajili ya kununua majiko 70,000 ya kisasa yanayotumia umeme kwa shule na vituo vya afya, huku ikitoa ahadi nyingine ya Dola milioni 26 kwa ajili ya kuhifadhi mifumo ikolojia ya pwani na kuimarisha ustahimilivu wa jamii.
“Aidha, Serikali ya Uingereza kupitia UK Aid imeahidi Pauni milioni mbili kwa ajili ya nishati safi ya kupikia na Pauni milioni mbili nyingine kwa ajili ya nishati jadidifu, sambamba na kusaidia wananchi milioni moja kupata majiko ya umeme kwa utaratibu wa kulipia gharama zake kidogo kidogo kupitia bili za umeme” amesema.

Ameongeza kuwa taasisi ya Sustainable Energy for All (SEforALL) imeahidi kuijumuisha Tanzania katika nchi zitakazonufaika na uwekezaji wa zaidi ya Dola bilioni nne kwa ajili ya nishati safi ya kupikia, pamoja na kusaidia nchi kuwa kitovu cha uzalishaji wa majiko na teknolojia zinazohusiana na nishati hiyo.
“Vilevile, kampuni ya UpEnergy imeahidi kuendeleza mradi wa nishati safi ya kupikia katika shule 3,000 za umma wenye thamani ya takribani Dola milioni 30 kupitia ushirikiano wa Tanzania na Japan katika biashara ya kaboni. Wakati huo huo, Saudi Arabia imeahidi kuendelea kufadhili miradi ya nishati jadidifu na nishati safi ya kupikia pamoja na kuunga mkono matumizi ya gesi asilia kama nishati ya mpito,” amesema.
Katika eneo la uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na athari za tabianchi, Masauni amesema Mfuko wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi umeidhinisha miradi yenye thamani ya Dola milioni 40 kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), huku Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi wa Kijani (GCF) ukiahidi Dola milioni sita kwa ajili ya kuimarisha uwezo wa Tanzania kuandaa miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Ameongeza kuwa Mfuko wa Kukabiliana na Hasara na Uharibifu (Loss and Damage Fund) umeidhinisha mchakato wa kupata Dola milioni 20 kupitia Benki ya CRDB kwa ajili ya miradi ya kusaidia jamii zinazoathiriwa na mabadiliko ya tabianchi katika visiwa vidogo, maeneo ya pwani na kanda za maziwa, hususan Pemba, Unguja, Kigoma na Pwani.
“Pia, International Solar Alliance imeiweka Tanzania katika mpango wa Dola milioni 200, huku U.S.-China Green Fund ikiwa imeijumuisha nchi katika mpango wa Dola milioni 300 unaolenga kusaidia nchi zinazoendelea katika eneo la nishati safi ya kupikia,” amesema.
Masauni amesema mafanikio hayo yanaenda sambamba na hatua za kuimarisha mifumo ya kitaasisi ili Tanzania iweze kunufaika zaidi na fedha za kimataifa, akieleza kuwa GCF imetoa ithibati kwa NEMC na kuifanya nchi kuwa miongoni mwa nchi chache za Afrika zenye taasisi mbili zilizoidhinishwa kupata fedha za mfuko huo, ambazo ni NEMC na CRDB Bank.
Amefafanua kuwa, hatua hiyo itaimarisha uwezo wa taasisi za ndani kusimamia na kupata fedha za tabianchi moja kwa moja, huku Wizara ya Fedha ikiendelea na mchakato wa kupata ithibati hiyo.
“Katika hatua nyingine, Tanzania imesaini makubaliano ya ushirikiano na Sekretarieti ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC) ili kuwa mwenyeji wa mikutano ya tabianchi, ikiwa ni nchi ya pili duniani kufanya hivyo.
“Kupitia makubaliano hayo, Tanzania inajiandaa kuwa mwenyeji wa mikutano miwili ya UNFCCC kuanzia Februari 2027, hatua inayotarajiwa kuongeza fursa za diplomasia ya tabianchi na kukuza utalii wa mikutano” amesema.
Vilevile, amesema Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC) imesaini mikataba ya ushirikiano na taasisi za kimataifa za IETA, Evercity UG na Verra kwa ajili ya kujenga uwezo, kuimarisha usimamizi wa biashara ya kaboni, usajili na uthibitishaji wa miradi pamoja na upatikanaji wa viwango vya kaboni vinavyokidhi viwango vya kimataifa.
Masauni amesema Tanzania pia imepata uthibitisho wa kuwa mwenyeji na kuanzisha Kituo cha Vijana Wajadili wa Tabianchi Afrika (Youth Negotiators Centre), kitakachojenga uwezo wa vijana kushiriki katika majadiliano ya kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, Zanzibar imetunukiwa cheti cha kutambuliwa kama Jiji Linalosimamia Taka Vizuri (Zero Waste City) na kuchaguliwa kuwa miongoni mwa maeneo 20 ya awali katika nchi 11 duniani yatakayotekeleza Mpango wa Kimataifa wa Maeneo Yasiyo na Taka.

Akizungumzia utekelezaji wa ahadi hizo, Masauni amesema Serikali itaweka usimamizi wa karibu kuhakikisha fedha na fursa za uwekezaji zilizopatikana zinafika nchini na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
“Jumla ya fedha na ahadi tulizopata ni Dola bilioni 4.7. Hizi ni fedha zinazotolewa kwa vipindi tofauti, hivyo tutahakikisha kunakuwa na usimamizi wa karibu ili fedha hizo zifike kwa walengwa na kuleta matokeo yaliyokusudiwa,” amesema.
Amesisitiza kuwa utekelezaji wa makubaliano hayo unahitaji ushirikiano wa Serikali, sekta binafsi, jamii na washirika wa maendeleo, akieleza kuwa mpito wa haki wa nishati unapaswa kuzingatia mazingira na haki ya nchi zinazoendelea kutumia rasilimali zake kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi.
Amesema Serikali itaendelea kuratibu utekelezaji wa matokeo ya COP31 kupitia wizara, idara na taasisi za Serikali, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, sekta binafsi na washirika wa maendeleo ili kuhakikisha fursa zilizopatikana zinachangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.


