Mkutano wa Kimataifa wa Sekta ya Madini kukutanisha washiriki zaidi ya 1,700

Na Tatu Mohamed

MKUTANO wa Saba wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini (TMIC 2026) unatarajiwa kushirikisha washiriki 1,715 kutoka ndani na nje ya nchi, ukiwa na lengo la kuvutia uwekezaji, kuimarisha uongezaji thamani wa madini na kuchochea ukuaji wa viwanda na uchumi nchini.

Mkutano huo utafanyika Novemba 19 hadi 21 mwaka huu katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, huku ukiwa na kaulimbiu isemayo ‘Madini Yaliyoongezwa Thamani: Chachu ya Ukuaji wa Viwanda na Uchumi’.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 17, 2026 jijini Dar es Salaam, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema hadi Novemba 17 mwaka huu, washiriki 1,715 walikuwa wamethibitisha kushiriki mkutano huo, wakiwemo 226 kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Amesema mkutano huo utahudhuriwa na mawaziri wa madini kutoka Afghanistan, Kenya, Uganda, Mali, Rwanda, Burundi, Saudi Arabia na Somalia, pamoja na viongozi wa kampuni za kimataifa, taasisi za fedha, wawekezaji, wachimbaji wadogo na wafanyabiashara wa madini.

Kwa mujibu wa Mavunde, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kufungua mkutano huo Novemba 19, huku Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akitarajiwa kuufunga Novemba 21, 2026.

“Kutakuwa na watoa mada zaidi ya 57 kutoka Afrika, Ulaya, Asia, Mashariki ya Mbali na Marekani, watakaowasilisha mada mbalimbali zinazohusu sekta ya madini, hususan namna ya kuongeza thamani ya rasilimali hizo nchini,” amesema.

Ameeleza kuwa mkutano huo unalenga kutumia utajiri wa rasilimali za madini zilizopo nchini kujenga uchumi wa viwanda, kuongeza ajira na kuhakikisha madini yanayozalishwa yanaongezwa thamani hapa nchini kwa manufaa ya Taifa.

Amesema miongoni mwa manufaa yanayotarajiwa kupatikana ni kuvutia uwekezaji, kuhamasisha matumizi ya utaalamu na teknolojia, kutangaza utajiri wa madini wa Tanzania, kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na kupanua masoko ya madini nje ya nchi.

Mbali na majadiliano, Mavunde amesema mkutano huo utaambatana na vikao vya pembeni vitakavyowahusisha mawaziri wa madini, mikutano ya kibiashara kati ya kampuni na kampuni (B2B), kituo cha pamoja cha huduma za Serikali kwa wawekezaji na mafunzo ya uongezaji thamani madini.

“Pia kutakuwa na maonesho ya madini yatakayoonesha mnyororo mzima wa thamani kuanzia uchimbaji hadi uzalishaji wa bidhaa ya mwisho, pamoja na hafla ya Usiku wa Madini itakayohusisha utoaji wa tuzo kwa wadau waliofanya vizuri,” amesema.

Akizungumzia mafanikio ya sekta hiyo, Mavunde amesema mchango wa madini katika Pato la Taifa uliongezeka hadi asilimia 10.3 mwaka 2025 kutoka asilimia 7.8 mwaka 2024.

Amesema thamani ya mauzo ya madini nje ya nchi iliongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 4.12 mwaka 2024 hadi bilioni 5.40 mwaka 2025, huku mapato ya Serikali yakifikia Sh1.39 trilioni katika mwaka wa fedha 2025/2026 kutoka Sh526 bilioni mwaka 2020/2021.

Aidha, amesema mchango wa wachimbaji wadogo katika uzalishaji wa madini nchini umefikia takribani asilimia 40, huku ajira rasmi katika sekta hiyo zikifikia 19,874 hadi Aprili 2025, ambapo asilimia 97.4 ya ajira hizo ni za Watanzania.

spot_img

Latest articles

WAANDISHI 64 WAFUZU TUZO ZA SAMIA KALAMU AWARDS 2026

Na Tatu Mohamed JUMLA ya Waandishi wa Habari 64 na vyombo vya habari 11 vimefuzu...

MIRADI YA UMEME KUIMARISHA GRIDI YA TAIFA NA KUCHOCHEA UKUAJI WA FURSA ZA KIJAMII NA KIUCHUMI– WAZIRI HOMERA

📌MD Twange atoa taarifa ya maendeleo ya utekelezaji wa Miradi ya kuimarisha Gridi ya...

Ndejembi ahimiza nishati safi, Lake Ges na Mama Salma wagawa mitungi ya kupikia

Na Mwandishi Wetu, Mchinga MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi,...

Ziara ya Rais Samia Uturuki yafungua milango ya uwekezaji, biashara

Na Tatu Mohamed ZIARA ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini Uturuki na ushiriki...

More like this

WAANDISHI 64 WAFUZU TUZO ZA SAMIA KALAMU AWARDS 2026

Na Tatu Mohamed JUMLA ya Waandishi wa Habari 64 na vyombo vya habari 11 vimefuzu...

MIRADI YA UMEME KUIMARISHA GRIDI YA TAIFA NA KUCHOCHEA UKUAJI WA FURSA ZA KIJAMII NA KIUCHUMI– WAZIRI HOMERA

📌MD Twange atoa taarifa ya maendeleo ya utekelezaji wa Miradi ya kuimarisha Gridi ya...

Ndejembi ahimiza nishati safi, Lake Ges na Mama Salma wagawa mitungi ya kupikia

Na Mwandishi Wetu, Mchinga MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi,...