TEKNOLOJIA YA NYUKLIA NI NYENZO YA MAENDELEO AFRIKA

Na Tatu Mohamed

IMEELEZWA kuwa Sayansi na teknolojia ya nyuklia vinapaswa kutazamwa kama nyenzo za maendeleo badala ya kuhusishwa pekee na matumizi ya kijeshi na hatari zinazoweza kujitokeza.

Mkurugenzi Msaidizi wa Sayansi na Teknolojia wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Harun Makandi, amesema teknolojia hiyo ina fursa kubwa za kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi zinazoikabili Afrika, ikiwemo kuboresha huduma za afya, upatikanaji wa maji safi na nishati ya umeme.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Carolyne Nombo, katika Jukwaa la Wanawake wa Afrika na Urusi katika Sekta ya Nyuklia la mwaka 2026 lililofanyika jijini Dar es Salaam, Dk. Makandi amesema ni muhimu kuimarisha matumizi ya teknolojia hiyo kwa manufaa ya jamii.

“Ni wakati mwafaka kwa wanasayansi, watunga sera, wahandisi wa nyuklia na washirika wa maendeleo wa kimataifa kubadilishana maarifa, uzoefu na mbinu bora ili kukuza maendeleo ya teknolojia ya nyuklia na matumizi yake barani Afrika,” amesema.

Amesisitiza kuwa maarifa na ujuzi utakaopatikana katika jukwaa hilo vinapaswa kutafsiriwa katika suluhisho halisi zinazoweza kutekelezwa katika ngazi za ndani, kikanda na kimataifa, akieleza kuwa hatua hiyo inaendana na Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) na Rais wa Mtandao wa Wanawake katika Sekta ya Nyuklia Tanzania (WiN Tanzania), Profesa Najat Mohammed, amesema maendeleo ya sekta hiyo yanahitaji uwekezaji katika teknolojia, miundombinu na rasilimali watu wenye ujuzi.

Amesema Tanzania inaendelea kuchunguza uwezekano wa kutumia nishati ya nyuklia huku ikipanua matumizi ya tiba ya nyuklia, teknolojia ya mionzi na utafiti wa kisayansi, hali inayoongeza mahitaji ya wahandisi, wanafizikia, watafiti na wataalamu wa usalama wa mionzi.

Profesa Mohammed amesema Mtandao wa Wanawake katika Sekta ya Nyuklia Tanzania umeongezeka kutoka wanawake takribani 70 ulipoanzishwa mwaka 2025 hadi kufikia 160, akisisitiza umuhimu wa kuwawezesha wanawake kupata ujuzi na kushiriki katika nafasi za uongozi na maamuzi.

Naye, Balozi wa Urusi nchini Tanzania, Andrey Avetisyan, amesema ushirikiano kati ya Urusi na nchi za Afrika ni muhimu katika kuendeleza sayansi na teknolojia ya nyuklia kwa ajili ya kutatua changamoto katika sekta za afya, kilimo na maeneo mengine ya maendeleo.

Wakati huo huo, Mkuu wa Jumuiya ya Wanawake ya Rosatom, Aleksandra Ryabykh, amesema shirika hilo la nishati ya nyuklia la Urusi liko tayari kushirikiana na Tanzania na nchi nyingine za Afrika kuwaendeleza wanawake kupitia mafunzo, programu za ulezi wa kitaalamu na ujenzi wa uwezo.

Jukwaa hilo lililofanyika chini ya kaulimbiu ya “Mazungumzo ya Mabara: Nishati ya Nyuklia kwa Mustakabali wa Baadaye” lilishirikisha wataalamu kutoka Tanzania, Urusi, Misri, Uganda, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Ethiopia na Afrika Kusini kwa lengo la kubadilishana maarifa na kujadili mchango wa teknolojia ya nyuklia katika maendeleo endelevu ya Afrika.

spot_img

Latest articles

DKT. KIKWETE APONGEZA HUDUMA YA MAJI CHALINZE, AIPA USHAURI DAWASA

Na Mwandishi Wetu RAIS Mstaafu, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ameishauri Mamlaka ya Majisafi...

DAWASA YAREJESHA MAJI KIKONGO BAADA YA MIAKA MIWILI

Na Mwandishi Wetu WAKAZI takribani 1,500 wa Vijiji vya Lupunga, Videte na Kwa Mkino,...

STAMICO YAONGEZA MAPATO HADI SH BILIONI 147.8

Na Tatu Mohamed SHIRIKA la Madini la Taifa (STAMICO) limeongeza mapato yake ya ndani kutoka...

SERIKALI KUANZA UTAFITI WA MADINI ENEO KUBWA LA NCHI KWA KUTUMIA FEDHA ZA NDANI

Ni kupitia mfuko wa utafiti wa Madini ▪️Rais Samia apongezwa kwa dhamira ya kukuza sekta...

More like this

DKT. KIKWETE APONGEZA HUDUMA YA MAJI CHALINZE, AIPA USHAURI DAWASA

Na Mwandishi Wetu RAIS Mstaafu, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ameishauri Mamlaka ya Majisafi...

DAWASA YAREJESHA MAJI KIKONGO BAADA YA MIAKA MIWILI

Na Mwandishi Wetu WAKAZI takribani 1,500 wa Vijiji vya Lupunga, Videte na Kwa Mkino,...

STAMICO YAONGEZA MAPATO HADI SH BILIONI 147.8

Na Tatu Mohamed SHIRIKA la Madini la Taifa (STAMICO) limeongeza mapato yake ya ndani kutoka...