Na Mwandishi Wetu
MAKAMU Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Rehema Sombi Omary (MNEC), amepokelewa kwa kishindo leo, Oktoba 9, 2026, katika Wilaya ya Nkasi, mkoani Rukwa, akiendelea na shughuli za Wiki ya UVCCM 2026.
Baada ya mapokezi, amefanya vikao vya ndani na viongozi wa Chama na Jumuiya, ambapo amepokea taarifa za utekelezaji wa shughuli mbalimbali za UVCCM wilayani humo.

Pia, Sombi amepata nafasi ya kuwasalimia mamia ya vijana na wananchi waliojitokeza kumpokea, akiwafikishia salamu za Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Ndg. Mohammed Ali Kawaida.
Amesisitiza kuwa viongozi hao wanawapenda vijana na kuthamini mchango wao katika maendeleo ya Taifa.

Akizungumza na vijana hao, Sombi amewataka kuendeleza kasi ya maendeleo katika Wilaya ya Nkasi na kuzingatia kaulimbiu ya Wiki ya UVCCM 2026 ‘Mazingira Tofauti, Fursa Sawa kwa Vijana’ akieleza kuwa inaakisi dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kupanua fursa kwa vijana.
Amesisitiza kuwa UVCCM inapaswa kuunganisha siasa na uchumi kwa vitendo, kwa kuhamasisha vijana kujiajiri, kutumia fursa zilizopo na kuimarisha shughuli zao za kiuchumi, sambamba na kutambua fursa zinazowekwa na Serikali kupitia wizara inayohusika na maendeleo ya vijana.
Aidha, akizungumzia kuelekea maadhimisho ya miaka 50 ya CCM, Sombi amesema vijana wana wajibu wa kujitathmini na kujiuliza wamekifanyia nini Chama, kwa kuangalia walikotoka, walipo na wanakoelekea.
Amewahimiza pia kujiandaa na kushiriki kikamilifu katika uchaguzi ujao kupitia Chama na jumuiya zake.


