Na Mwandishi Wetu
WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imeweka kambi ya huduma za papo kwa papo katika Maonesho ya Kimataifa ya Utalii wa Sanaa na Utamaduni yanayofanyika katika viwanja vya General Tyre, Njiro, jijini Arusha, leo Oktoba 07, 2026, kwa lengo la kuwafikia wabunifu na wadau wa uchumi wa ubunifu na kuwawezesha kupata huduma za usajili na leseni kwa urahisi.
Maonesho hayo yalifunguliwa rasmi na Mkurugenzi Msaidizi wa Sanaa za Ufundi kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Bi. Bona Masenge, ambaye alisema maonesho hayo si tu mahali pa kuonesha bidhaa, bali pia ni fursa ya kuonesha uzoefu na uwezo wa Watanzania, pamoja na kujenga soko la bidhaa na huduma za ubunifu ndani na nje ya nchi.

Bi. Masenge alieleza kuwa vijana na wanawake ni sehemu muhimu ya uchumi wa ubunifu, hivyo amewataka wadau kutotazama sanaa na ubunifu kama burudani pekee, bali kama fursa ya biashara, ajira na kujiajiri.
“Kwa vijana waliopo mijini na vijijini, tunataka kuona uchumi wa ubunifu ukiwa sehemu ya fursa za ajira na kujiajiri,” alisema Bi. Masenge.

Aidha, Msaidizi wa Usajili Mkuu kutoka BRELA, Bw. Nassoro Mtavu, alisema shughuli zote zinazoendelea katika maonesho hayo zinapaswa kurasimishwa, hivyo wabunifu na wadau wote wanakaribishwa katika banda la BRELA kupata huduma za usajili, ikiwemo usajili wa kampuni, usajili wa majina ya biashara, usajili wa alama za biashara na huduma, utoaji wa hataza, utoaji wa leseni za biashara Kundi A, utoaji wa leseni za viwanda pamoja na vyeti kwa viwanda vidogo.
Kwa upande wake, Bi. Upendo Halisi, mshiriki wa maonesho hayo, amewashauri wadau wengine kutembelea banda la BRELA ili kupata huduma za usajili wa papo kwa papo, elimu kuhusu huduma za BRELA na kusaidiwa kutatua changamoto mbalimbali za usajili.

BRELA itaendelea kushiriki kikamilifu katika Maonesho ya Kimataifa ya Utalii wa Sanaa na Utamaduni kuanzia Oktoba 06 hadi 11, 2026 na yamewakutanisha wadau mbalimbali, wakiwemo Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).


