RIBA YA BENKI KUU YAENDELEA KUBAKIA ASILIMIA 6.25

Na Tatu Mohamed

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imeendelea kubakiza Riba ya Benki Kuu (CBR) katika asilimia 6.25 kwa robo inayoishia Desemba 2026, ikisema msimamo huo unalenga kuendelea kudumisha utulivu wa uchumi na kuwezesha ukuaji endelevu.

Uamuzi huo umefikiwa na Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) iliyokutana Oktoba 7, 2026, huku BoT ikisema msimamo wa sasa wa sera ya fedha unaendelea kuwa sahihi kutokana na mwenendo wa uchumi wa ndani na mazingira ya uchumi wa dunia.

BoT imesema mfumuko wa bei unatarajiwa kuendelea kubaki ndani ya lengo la asilimia 3 hadi 5, ingawa kuna hatari zinazoweza kuathiri mwenendo huo, ikiwemo kupanda kwa bei za mafuta kutokana na mgogoro wa Mashariki ya Kati na uwezekano wa mvua za El Niño.

Kwa mujibu wa BoT, hatua zinazochukuliwa na Serikali kudhibiti mfumuko wa bei na kuimarisha ukuaji wa uchumi zinaendelea kusaidia uchumi wa Tanzania kukabiliana na changamoto hizo.

BoT imesema uchumi wa dunia unaendelea kukabiliwa na changamoto kutokana na mgogoro wa Mashariki ya Kati, unaoweza kuathiri upatikanaji wa mafuta na mbolea pamoja na minyororo ya usambazaji, huku bei ya mafuta ikipanda zaidi ya dola 100 kwa pipa.

Aidha, Shirika la Fedha Duniani (IMF) linakadiria ukuaji wa uchumi wa dunia kuwa asilimia 3, kutoka makadirio ya awali ya asilimia 3.5, wakati Benki ya Dunia inakadiria ukuaji wa asilimia 2.5, ikilinganishwa na asilimia 2.9 iliyokadiriwa awali.

BoT pia imesema mfumuko wa bei duniani umeendelea kuwa juu ya asilimia nne, hali iliyofanya benki kuu nyingi kusitisha hatua za kupunguza sera za fedha, huku bei ya dhahabu ikiwa juu na ikitarajiwa kuendelea kuongezeka, jambo linaloweza kuongeza mapato ya fedha za kigeni na akiba ya taifa.

Katika uchumi wa ndani, BoT imesema zoezi la kubadili mwaka wa msingi wa Pato la Taifa kwa Tanzania Bara kutoka 2015 hadi 2019 limeonesha kuwa Pato la Taifa kwa mwaka 2025 lilifikia Sh234.104 trilioni, sawa na dola bilioni 92.3, kutoka Sh230.073 trilioni, sawa na dola bilioni 90.7, kwa makadirio ya awali.

Kwa Zanzibar, Pato la Taifa kwa mwaka 2025 lilifikia Sh9.242 trilioni, sawa na dola bilioni 3.6, kutoka Sh7.029 trilioni, sawa na dola bilioni 2.8, huku takwimu hizo zikilenga kuwezesha ulinganishaji na uelewa wa pamoja wa mwenendo wa uchumi.

BoT imesema uchumi wa Tanzania Bara ulikua kwa asilimia sita katika robo ya kwanza ya mwaka 2026, huku robo ya pili na ya tatu zikitarajiwa kukua kwa zaidi ya asilimia sita, zikichochewa na huduma za fedha, uzalishaji viwandani, miundombinu na huduma za kijamii.

Kwa upande wa Zanzibar, uchumi ulikua kwa asilimia 6.7 katika robo ya kwanza ya mwaka 2026 na unatarajiwa kukua kwa zaidi ya asilimia saba katika robo ya pili na ya tatu, ukichochewa na sekta za utalii, ujenzi na umwagiliaji.

BoT imesema mfumuko wa bei Tanzania Bara ulifikia asilimia 4.3 mwezi Agosti 2026, kutoka asilimia 4.1 katika robo iliyoishia Juni, ukichangiwa zaidi na ongezeko la bei za mafuta, nishati na usafiri.Zanzibar, mfumuko wa bei ulikuwa asilimia 5.6 mwezi Agosti, ukishuka kutoka asilimia sita mwezi Julai, lakini ukiendelea kuwa juu ya lengo la asilimia tano.

Katika sekta ya fedha, BoT imesema mikopo kwa sekta binafsi ilikua kwa asilimia 32.5 katika robo iliyoishia Septemba 2026, huku hali ya sekta ya benki ikiendelea kuwa imara na mikopo chechefu ikiwa asilimia 2.5 mwezi Agosti, chini ya kiwango cha juu cha asilimia tano.

BoT pia imesema mifumo ya malipo imeendelea kuwa imara na yenye ufanisi, huku sekta ya nje ikiendelea kuwa katika hali nzuri. Nakisi ya akaunti ya kawaida ilikuwa asilimia 2.5 ya Pato la Taifa kwa mwaka ulioishia Septemba, ikilinganishwa na asilimia 2.4 mwezi Juni.

Kwa mujibu wa BoT, mauzo ya nje ya dhahabu, bidhaa zilizotengenezwa viwandani na huduma za utalii yameendelea kusaidia kukabiliana na mahitaji ya bidhaa kutoka nje na gharama za usafirishaji.

Akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa zaidi ya dola bilioni sita, ikiwa na uwezo wa kugharamia uagizaji wa bidhaa na huduma kwa miezi 4.3, zaidi ya lengo la miezi minne.

Katika upande wa Serikali, BoT imesema mapato ya ndani kupitia kodi yamezidi malengo, huku matumizi yakilingana na rasilimali zilizopo na nakisi ya bajeti ikiendelea kuwa chini ya asilimia tatu ya Pato la Taifa.

spot_img

Latest articles

TRANSFOMA NNE ZASAFIRISHWA KWENDA MRADI WA TAZA

📌 Utekelezaji wa agizo la MD Twange la kukamilisha TAZA ifikapo Novemba 15, 2026 📌...

MAKAMU MWENYEKITI UVCCM, SOMBI KUZINDUA WIKI YA VIJANA WA CCM

Na Mwandishi Wetu MAKAMU Mwenyekiti wa UVCCM, Ndugu Rehema Sombi Omary (MNEC) atazindua Wiki...

BANDA LA DAWASA LAVUTIA USHIRIKI VIONGOZI NA WAGENI COP12

Na Mwandishi Wetu MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar Es Salaam (DAWASA)...

KABUDI: VYAMA VYA SIASA VIENDELEE KUJENGA UTAMADUNI WA MAZUNGUMZO

Na Tatu Mohamed WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu,...

More like this

TRANSFOMA NNE ZASAFIRISHWA KWENDA MRADI WA TAZA

📌 Utekelezaji wa agizo la MD Twange la kukamilisha TAZA ifikapo Novemba 15, 2026 📌...

MAKAMU MWENYEKITI UVCCM, SOMBI KUZINDUA WIKI YA VIJANA WA CCM

Na Mwandishi Wetu MAKAMU Mwenyekiti wa UVCCM, Ndugu Rehema Sombi Omary (MNEC) atazindua Wiki...

BANDA LA DAWASA LAVUTIA USHIRIKI VIONGOZI NA WAGENI COP12

Na Mwandishi Wetu MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar Es Salaam (DAWASA)...