Na Tatu Mohamed
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, ameshuhudia utiaji saini na uzinduzi wa mpango wa kihistoria wa ufadhili wa uunganishaji wa umeme kwa wananchi, uliofanyika kati ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Benki ya CRDB.
Hafla hiyo ya utiaji saini imefanyika leo Oktoba 02, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, ikiwa ni hatua madhubuti ya kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Mhe. Ndejembi ameeleza kuwa ushirikiano huo unalenga kuondoa vikwazo vya kifedha vinavyowazuia wananchi kupata nishati ya umeme, akibainisha kuwa nishati ni msingi na kichocheo kikuu cha ukuaji wa uchumi wa taifa.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejielekeza kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma hiyo ya msingi.

“Umeme ni huduma inayofungamanishwa na maendeleo. Megawati 2,115 kutoka Mradi wa Bwawa la Julius Nyerere zitakuwa na maana endapo tu hazitamfikia mlaji wa mwisho hospitalini, kiwandani, majumbani na kwenye biashara,” amesisitiza Mhe. Ndejembi.
Katika mpango huo, Benki ya CRDB itagharamia ada ya uunganishaji wa shilingi 27,000 kwa wateja 500,000 wa vijijini na maeneo ya Peri-Urban kila mwaka, huku wateja wa maeneo ya mijini wakitengewa utaratibu maalum wa kulipia gharama hizo kidogo kidogo kupitia TANESCO.
Akiwasilisha takwimu za sekta hiyo, Makamu wa Rais amebainisha kuwa Tanzania hivi sasa inaongoza barani Afrika kwa kuunganisha wananchi na umeme ikifikisha wateja milioni 9.

Aidha, ameeleza kuwa vijiji vyote 12,318 nchini vimeshaunganishwa na nishati hiyo—kutoka vijiji 506 pekee mwaka 2007—huku vitongoji 33,657 kati ya 64,359 tayari vina umeme, na vilivyobaki 30,702 vikitarajiwa kukamilishwa kabla ya mwaka 2030.
Ili kuimarisha upatikanaji wa nishati hiyo, Mhe. Ndejembi amesema, Serikali imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 231 mkoani Dar es Salaam pekee, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Dege Wilayani Kigamboni na mradi wa kituo cha kisasa cha Mabibo kinachopokea umeme kutoka Kinyerezi.

Hatua hizi zote zinalenga kutimiza malengo ya Dira ya Taifa ya 2050 na utekelezaji wa Ilani ya CCM, ikiwa na lengo la kuzalisha megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030 na kufikia megawati 74,000 ifikapo mwaka 2050.


