DAR ES SALAAM
Chama cha Waandishi wa Habari cha Oman (OJA), kwa kushirikiana na Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), kimeandaa kongamano la pamoja la wanahabari kutoka Oman na Tanzania, litakalofanyika Oktoba 1, 2026, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kuhusu kongamano hilo, Mwenyekiti wa OJA, Dkt. Mohammed Mubarak Al-Araimi, amesema ni fursa muhimu ya kuimarisha ushirikiano miongoni mwa wanahabari na kudumisha uhusiano wa kihistoria, kiuchumi na kitamaduni kati ya Oman na Tanzania.
Dkt. Al-Araimi, ambaye amezuru Tanzania kwa mara ya kwanza, amesema ujio wake pamoja na ujumbe wa wanahabari kutoka Oman ni hatua muhimu katika kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili. Amesema jukwaa hilo halilengi tu kuwakutanisha wanahabari, bali pia linatumika kama daraja la kuendeleza uhusiano wa muda mrefu wa kihistoria, kiuchumi na kitamaduni uliopo kati ya Oman na Tanzania.

Amesema kongamano hilo litawakutanisha takriban wanahabari 40 kutoka Oman, ambao watajadili mada zinazohusu sekta ya habari, uchumi, uwekezaji, utalii na biashara, kwa lengo la kutafuta fursa zitakazonufaisha pande zote mbili kupitia vyombo vya habari.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa JOWUTA, Suleiman Msuya, amesema mchakato wa ushirikiano kati ya JOWUTA na OJA ulianza mwaka 2022 wakati wa Mkutano Mkuu wa 31 wa Shirikisho la Wanahabari Duniani (IFJ), na kwamba umeendelea kukua hadi kufikia hatua ya kuandaliwa kwa kongamano hilo, ambalo amesema ni la kwanza kufanyika katika ukanda wa Afrika Mashariki na SADC baada ya OJA kufanya kongamano kama hilo nchini Misri.
Msuya amesema kongamano hilo litakuwa na mada kuu nane, nne kutoka Tanzania na nne kutoka Oman, zitakazojadili masuala ya habari na ushirikiano wa wanahabari, uchumi na biashara, uwekezaji pamoja na utalii. Amesema mjadala huo unalenga kutumia sekta ya habari kama daraja la kufungua fursa na kuimarisha uhusiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Oman.

Amesema ushirikiano huo pia unaunga mkono juhudi za Serikali katika kutangaza fursa za uwekezaji nchini, huku akieleza kuwa wanahabari wanapaswa kutumia nafasi hiyo zaidi ya kuandika habari kwa kujenga uhusiano wa kisekta utakaosaidia kuvutia wawekezaji kutoka Oman kuja Tanzania na pia kutoa fursa kwa Watanzania kwenda kuwekeza Oman.
Pia amesisitiza kuwa wanahabari sasa wanaipambania nchi si kwa kuandika habari pekee, bali pia kwa kutumia taaluma yao kujenga mahusiano ya kisekta, kutangaza fursa za uwekezaji, biashara na utalii, pamoja na kuwaunganisha wawekezaji wa Oman na Tanzania na Watanzania wanaotaka kuwekeza Oman.
Msuya amesema siku ya kongamano hilo, JOWUTA na OJA zinatarajiwa kutia saini Hati ya Makubaliano (MoU), itakayofungua ukurasa mpya wa ushirikiano na kuwezesha ubadilishanaji wa wanahabari, mafunzo pamoja na kubadilishana uzoefu kati ya wanahabari wa pande zote mbili.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, amesema jukwaa hilo litachangia kuimarisha diplomasia ya habari na uhusiano wa kihistoria na kitamaduni kati ya Tanzania na Oman, huku likitoa fursa ya kutangaza uwekezaji, biashara na utalii uliopo Tanzania Bara na Zanzibar kwa wananchi na wawekezaji wa Oman pamoja na mataifa mengine ya Kiarabu.
Balile amesema ushirikiano huo utaimarishwa zaidi kupitia MoU hiyo, itakayowezesha mafunzo, kubadilishana uzoefu, kukuza taaluma ya habari na kujenga uwezo wa wanahabari wa pande zote mbili. Amewataka wanahabari wa Tanzania kutumia fursa hiyo kuripoti habari zitakazoongeza uelewa kuhusu uhusiano na fursa zilizopo kati ya nchi hizo.
Msuya amewataka wanahabari na vyombo vya habari kutoa taarifa za kutosha kuhusu kongamano hilo, akieleza kuwa ni muhimu viongozi wakuu wa Serikali, wakiwemo Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na mawaziri wa sekta husika, kutambua mchango wa sekta ya habari katika kukuza uhusiano, uwekezaji, biashara na maendeleo ya taifa.


