Na Mwandishi Wetu, Ngorongoro
KATIKA kuadhimisha Siku ya Faru Duniani, inayoadhimishwa Septemba 22 kila mwaka, Ngoteya Wild imezindua filamu ya “The Rhinos of Ngorongoro – A Conservation Story”, iliyoandaliwa kwa kushirikiana na Ngorongoro Conservation Area Authority (NCAA), ikiwa na lengo la kuangazia umuhimu wa uhifadhi wa faru na watu wanaofanya kazi kila siku kuhakikisha wanyama hao wanaendelea kuwepo katika mazingira yao ya asili.
Filamu hii inatoa mtazamo wa ndani kuhusu maisha ya faru katika Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, pamoja na juhudi za ulinzi, ufuatiliaji na huduma zinazofanyika kuhakikisha usalama na ustawi wao. Ngorongoro ina umuhimu wa kipekee katika uhifadhi wa faru, ikihifadhi faru weusi na faru weupe.

The Rhinos of Ngorongoro haiangazii faru pekee, bali inasimulia pia hadithi ya watu wanaofanya kazi kuhakikisha wanyama hawa wa kipekee wanaendelea kuwa sehemu ya mandhari ya Ngorongoro.
Filamu inaonyesha kazi ya askari wa uhifadhi, wafuatiliaji (trackers) na madaktari wa wanyamapori, ambao kwa pamoja hutumia ujuzi, uzoefu, uvumilivu na kujitolea kuwafuatilia, kuwachunguza na kuhakikisha usalama na afya ya faru. Kuanzia kutambua alama za nyayo hadi kufuatilia mienendo ya faru, kazi hii inahitaji ushirikiano wa karibu na uelewa mkubwa wa mazingira.
Simulizi hii pia inaonyesha kuwa mafanikio katika uhifadhi wa faru hayawezi kutegemea kundi moja pekee. Ni jukumu linalohitaji ushirikiano wa askari wa uhifadhi, trackers, madaktari wa wanyamapori, wataalamu wa ikolojia, viongozi, jamii na wadau wengine wa uhifadhi.

Uhifadhi wa faru ni wajibu wa kizazi cha sasa kwa vizazi vijavyo. Kwa kutambua umuhimu huo, Ngorongoro inaendelea kuweka mkazo katika ulinzi, ufuatiliaji, utaalamu, teknolojia na ushirikishwaji wa jamii ili kuhakikisha faru wanaendelea kuwa sehemu muhimu ya urithi wa Ngorongoro na dunia.
Kupitia filamu hii, Ngoteya Wild inaleta hadithi hiyo karibu na watazamaji, ikitoa fursa ya kuona kile kinachotokea nyuma ya pazia la uwepo na usalama wa faru wa Ngorongoro. Ni simulizi inayokwenda zaidi ya picha za wanyamapori, kwa kuonyesha watu, utaalamu na juhudi zinazowezesha uhifadhi kufanyika kila siku.

Muongozaji wa filamu hii ni Hans Cosmas Ngoteya, Mamlaka ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na Team nzima ya Ngoteya Wild
Filamu hii sasa inapatikana kwenye YouTube kupitia akaunti ya Ngoteya Wild.
Heri ya Siku ya Faru Duniani.


