WAZIRI WA FEDHA AITAKA SEKTA ZA SERIKALI KUSHIRIKIANA KUONGEZA UZALISHAJI

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Fedha amezitaka sekta mbalimbali za Serikali kushirikiana kwa karibu katika kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi, akisisitiza kuwa maendeleo ya sekta hizo hayawezi kufikiwa kwa kila taasisi kufanya kazi kivyake.

Amesema hayo leo wakati wa ziara katika Maonesho ya Nane Nane jijini Dodoma, ambapo ametembelea mabanda mbalimbali yanayohusisha wadau wa kilimo, mifugo, uvuvi na sekta zinazohusiana na uzalishaji.

Amesema pamoja na mafanikio yanayoonekana katika sekta hizo, bado kuna umuhimu wa Serikali kuendelea kuunganisha nguvu katika maeneo ya uzalishaji, usindikaji wa mazao, upatikanaji wa mitaji na masoko.

Ameongeza kuwa, wizara na taasisi zinazohusika na fedha, kilimo, mifugo, uvuvi, viwanda pamoja na sekta nyingine zinapaswa kufanya kazi kwa pamoja ili kuongeza tija na kuhakikisha uzalishaji unakuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa nchi.

“Badala ya kusema mimi niko kilimo, mimi niko fedha, mimi niko viwanda, tunahitaji kwenye maendeleo ya uzalishaji katika sekta ya kilimo, pamoja na mchakato wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi, pamoja na huduma ambazo zinaambatana na hili,” amesema.

Amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika utafiti ili kubaini changamoto zinazokwamisha uzalishaji na kutafuta suluhisho zinazoweza kuleta mageuzi makubwa katika sekta hizo.

Amesema baadhi ya changamoto zinazowakabili wazalishaji zinaweza kutatuliwa kupitia uwekezaji unaolenga kuongeza tija na ambao unaweza kujigharamia kwa kurejesha fedha zilizowekezwa na kuendelea kuzunguka katika shughuli za uzalishaji.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo ameeleza kuridhishwa na jitihada zinazofanyika katika ufugaji wa samaki, akisema sekta hiyo ni muhimu katika kuongeza upatikanaji wa chakula chenye protini kwa wananchi.

Amesema uzalishaji wa samaki kwa njia ya uvuvi wa asili katika bahari na maziwa umekuwa ukikabiliwa na changamoto mbalimbali, hivyo kuna umuhimu wa kuongeza uzalishaji kupitia ufugaji wa samaki.

Amesema Serikali inapaswa kuendelea kuunga mkono juhudi hizo ili kuongeza uzalishaji wa samaki na kuimarisha lishe kwa wananchi.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwaunganisha wakulima na wazalishaji na masoko, akisema uzalishaji pekee hautoshi bila kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa zinafika sokoni kwa ubora, kiasi na wakati unaohitajika.

Amesema wadau wa viwango nao wana wajibu wa kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini zinafikia viwango vinavyokubalika na kuwawezesha wazalishaji kuingia katika masoko kwa urahisi.

“Tunapaswa kuhakikisha kile ambacho kinazalishwa tunakifikisha sokoni kikiwa na kiwango kinachotakiwa, ili wazalishaji wasiishie kuzalisha bila kupata soko,” amesema.

Waziri huyo pia ametoa wito wa kuendelea kutangaza bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali wa Tanzania, akisema baadhi ya bidhaa bado hazijulikani kwa wananchi licha ya kuwa na uwezo wa kuingia sokoni.

Amesema hatua hiyo inapaswa kwenda sambamba na kuhakikisha bidhaa zinazalishwa kwa idadi na ubora unaokidhi mahitaji ya soko.

Kwa ujumla, Waziri huyo amewapongeza wadau wa kilimo, mifugo na uvuvi kwa kazi kubwa inayofanyika, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kushirikiana kwa karibu ili kuongeza uzalishaji, masoko na mchango wa sekta hizo katika maendeleo ya Taifa.

spot_img

Latest articles

RAIS SAMIA AAGIZA WAKUU WA MIKOA KUJIANDAA NA UDHIBITI WA ATHARI ZA ELNINO

Na Mwandishi Wetu RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan,...

Rais Samia azindua Kituo cha kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere

Na Mwandishi Wetu RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan,...

JNHPP kuongeza Umeme wa Gridi ya Taifa kwa asilimia 45

Na Tatu Mohamed BWAWA la Julius Nyerere (JNHPP) linatarajiwa kuongeza kwa kiasi kikubwa uwezo...

Tanzania kuandika historia leo, Rais Samia kuzindua Bwawa la Julius Nyerere

Na Tatu Mohamed TANZANIA inaandika ukurasa mpya katika historia ya sekta ya nishati leo...

More like this

RAIS SAMIA AAGIZA WAKUU WA MIKOA KUJIANDAA NA UDHIBITI WA ATHARI ZA ELNINO

Na Mwandishi Wetu RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan,...

Rais Samia azindua Kituo cha kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere

Na Mwandishi Wetu RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan,...

JNHPP kuongeza Umeme wa Gridi ya Taifa kwa asilimia 45

Na Tatu Mohamed BWAWA la Julius Nyerere (JNHPP) linatarajiwa kuongeza kwa kiasi kikubwa uwezo...