Na Mwandishi Wetu
NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dkt. Jafar Seif, amesema mfumo wa One Stop Center unaotumika katika banda la Ofisi ya Waziri Mkuu kwenye Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) umeongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa kuwawezesha wananchi kupata huduma mbalimbali na ufumbuzi wa changamoto zao sehemu moja.
Dkt. Seif amesema hayo baada ya kutembelea banda la Ofisi ya Waziri Mkuu katika Viwanja vya Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, ambapo alipongeza maandalizi ya banda hilo na namna watumishi wanavyotoa huduma kwa wananchi.

Amesema kupitia mfumo huo, wananchi hawalazimiki tena kutembelea halmashauri au taasisi mbalimbali kufuatilia huduma zinazotolewa na TAMISEMI, kwani huduma nyingi zinapatikana katika eneo moja.
“Ndani ya banda moja mwananchi anapata huduma nyingi kwa wakati mmoja. Badala ya kwenda halmashauri moja hadi nyingine au ofisi mbalimbali, hapa anapata maelezo, ufumbuzi wa changamoto zake na, pale inapohitajika, anaunganishwa moja kwa moja na wataalamu waliopo katika maeneo husika,” amesema Dkt. Seif.
Amefafanua kuwa wataalamu kutoka idara na taasisi mbalimbali za TAMISEMI wanatoa ushauri na ufafanuzi kuhusu masuala ya elimu, ujenzi, uhamisho wa watumishi, vibali pamoja na huduma nyingine zinazotolewa na mamlaka za serikali za mitaa.
Aidha, amesema wananchi pia wanapata elimu na huduma kutoka taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu zinazoshughulikia masuala ya hifadhi ya jamii, watu wenye ulemavu, udhibiti wa dawa za kulevya na huduma nyingine za kijamii.
Dkt. Seif amesema ushiriki wa Ofisi ya Waziri Mkuu katika Maonesho ya Sabasaba unalenga kusogeza huduma karibu na wananchi, kuongeza uelewa kuhusu majukumu ya taasisi zake na kuhakikisha changamoto zinazowakabili wananchi zinapatiwa ufumbuzi kwa haraka na kwa ufanisi.
Amewahimiza wananchi kutumia siku zilizobaki za maonesho hayo kutembelea banda la Ofisi ya Waziri Mkuu ili kupata huduma, elimu na ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayohusu TAMISEMI na taasisi zake.
Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara yanaendelea katika Viwanja vya Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam, yakishirikisha taasisi za umma na sekta binafsi kuonesha bidhaa, huduma na fursa mbalimbali za maendeleo.


