Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Taifa Gas imetangaza kuwa haitapandisha bei ya gesi ya majumbani (LPG), licha ya ongezeko la takribani asilimia 43 la bei ya nishati hiyo katika soko la kimataifa.
Uamuzi huo unalenga kulinda watumiaji dhidi ya athari za mabadiliko ya bei duniani na kuendeleza upatikanaji wa nishati nafuu nchini.
Bei ya gesi ya kupikia imeongezeka kwa kiasi kikubwa katika wiki za hivi karibuni kwenye soko la dunia, hali iliyosababisha gharama za ununuzi na usambazaji kupanda katika minyororo ya ugavi.
Akizungumza kuhusu uamuzi huo, Meneja Mkuu wa Taifa Gas, Devis Deogratius, alisema kampuni imejipanga kubeba mzigo wa ongezeko hilo ili kuwasaidia wateja wake.

“Katika mazingira haya ya sasa, tunayo dhamira ya dhati ya kuwasaidia wateja wetu kwa kubeba athari za ongezeko la gharama ya nishati ya kupikia kwa kutokuongeza bei, huku tukihakikisha upatikanaji endelevu wa gesi safi na ya kuaminika,” alisema.
Alibainisha kuwa kipaumbele cha Taifa Gas ni kuhakikisha bei ya gesi inaendelea kuwa nafuu, kutokana na umuhimu wake katika maisha ya kila siku ya wananchi na shughuli za kiuchumi, hasa kwa kaya na biashara ndogo ndogo.
Deogratius alisisitiza kuwa lengo kuu ni kudumisha upatikanaji wa gesi kwa gharama nafuu huku usambazaji ukiendelea kuwa wa uhakika kote nchini.

“Tunatambua kuwa gesi ya kupikia ni nishati muhimu kwa Watanzania wengi, hivyo tunajitahidi kuhakikisha inapatikana kwa bei nafuu bila kuathiri upatikanaji wake,” aliongeza.
Alifafanua kuwa, Kampuni hiyo ina mtandao wa maghala 25 nchini kote, unaowezesha kusambaza gesi katika maeneo ya mijini na vijijini ambapo uwekezaji huo wa miundombinu unalenga kuhakikisha hakuna upungufu wa nishati hiyo muhimu.
“Tanzania ni nchi kubwa yenye mahitaji tofauti, hivyo upatikanaji wa nishati hii ni kipaumbele chetu. Tumewekeza katika miundombinu itakayowezesha usambazaji wa uhakika,” alisema Deogratius.

Aliongeza kuwa, Taifa Gas inaendelea kuunga mkono juhudi za kitaifa na kimataifa za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, ikiwa ni pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).
“Jukumu letu ni kuwalinda na kuwaunga mkono Watanzania kwa kutoa huduma bora, uendeshaji wenye uwajibikaji na kuhakikisha upatikanaji wa nishati safi kwa muda mrefu,” alisisitiza Deogratius.


