KUMKUMBUKA MAREHEMU BALOZI JUMA VOLTER MWAPACHU
Balozi Juma Volter Mwapachu (Mwenyezi Mungu Amrehemu), mwanasheria, mwanadiplomasia, msomi na mwandishi, alizaliwa Mwanza Jumapili tarehe 27 Septemba 1942 na alifariki tarehe 28 Machi 2025 Dar es Salaam, na kuzikwa Pande, Tanga, baada miongo karibu 6 ya utumishi wa umma uliotukuka.
Sio rahisi kwangu kumwelezea Juma Volter Mwapachu, au kwa kifupi JV. Kwani alikuwa mtu wa karibu sana kwangu na kwa familia yangu. Itahitaji muda mrefu kuyaeleza na kuyaandika maisha yake. Hata hivyo nitajitahidi, ili mradi nami niwe mmoja ya wale tunaobahatika kuweka kumbukumbu ya jinsi tulivyomfahamu JV katika uhai wake. Tarehe 28 Machi 2025 Ilikuwa siku ya kawaida kwangu na mke wangu Lucy, kawaida mpaka jioni tulipopata taarifa ya kusikitisha kutoka kwa kijana wetu Max, kwamba safari ya JV hapa duniani ilikuwa imefikia tamati siku hiyo. Ni kweli tulijua hali ya afya ya JV ilikuwa si nzuri, kama ambavyo afya yangu pia ilivyo na mgogoro. Hata hivyo matumaini na dua zetu zililenga katika kumtakia heri arudi katika hali yake ya kawaida. Haikuwezekana. Tukabaki kumpa pole mkewe Rose na familia yote ya JV. Watu wa kwanza nasi ilibidi tuwataarifu ni Balozi Chirau Ali Mwakwere na mkewe Rose, wenyeji wa Matuga, Kaunti ya Kwale, Kenya, rafiki zetu wa karibu na rafiki wa familia ya JV pia.
Huwa naulizwa mlifahamiana lini na wapi na JV? Inanibidi nirudi miaka 60 iliyopita. Mwaka 1966 nikiwa kidato cha pili, Shule ya Sekondari ya Malangali, Mkoa wa Iringa, pamoja na Gwaponile George Mwanjabala (mwanadiplomasia ambaye naye alikuja kuwa Balozi), wakati huo yeye akiwa kidato cha nne, tuliteuliwa kuiwakilisha Malangali kwenye Mkutano Mkuu wa Umoja wa Wanafunzi Tanzania (National Union of Tanzania Students-NAUTS) uliofanyika Dar es Salaam. Umoja huo uliunganisha taasisi za elimu kuanzia ngazi ya sekondari mpaka Chuo Kikuu. JV alikuwa mmoja wa wajumbe wengi waliokiwakilisha Chuo Kikuu Kishirika cha Dar es Salaam, wakati huo kikiwa Chuo Kishiriki cha Chuo Kikuu cha Afrika ya Mashariki. Wajumbe wengine ninaokumbuka walihudhuria mkutano huo ni pamoja na Joseph Warioba, Samuel Sitta, Onesphoro Chawe, Julius Matiko, Nimrod Lugoe, Ali Mchumo, James Kateka, Christopher Labani, na Jenerali Ulimwengu. Mjumbe mwingine aliyehudhuria na ambaye alikuwa karibu sana na JV alikuwa si mwingine bali ni Rose Omari, na wahenga wanasema, yaliyoendelea baada ya hapo sasa ni historia.
Kitu kingine kilichotuunganisha ilikuwa ni kwamba mimi ni mwenyeji wa Wilaya ya Rungwe, na hii ndio Wilaya iliyompatia JV msingi wa elimu ambao hatimaye ulimfanya awe msomi, mwandishi bora na kiongozi makini. JV alisoma shule ya kati (Middle School) ya Ndembela kwa muda mfupi, kama miezi mitatu hivi, na baadaye akajiunga na Shule ya Kati maarufu ya Mpuguso. Kumbukumbu zangu ni kwamba alikuja huku baada ya Mzee Hamza Kibwana Bakari Mwapachu kuhamishiwa Rungwe mwaka 1955 kuwa Afisa Wilaya Msaidizi (Assistant District Officer-ADO), wakati huo ADO kikiwa ni cheo kikubwa sana kwa watumishi Waafrika katika serikali ya kikoloni. Mzee Hamza Kibwana Mwapachu alikuwa mmoja ya marafiki wa karibu sana wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, wakiwa katika mapambano dhidi ya ukoloni, kumbukumbu za ukaribu wao ziko katika maandiko mengi.
Kama nilivyoeleza awali, kabla hajahamia Mpuguso, JV alisoma kwa muda mfupi Shule ya Kati ya Ndembela. Hapo alikutana na akina Davies Mwaikambo, Emmanuel Mwambulukutu na Martin Mwakalindile.
Pale Mpuguso, JV katika nyakati tofauti alikutana na akina Ulli Mwambulukutu, Cleveland Nkata, George Kilindu, Francis Louis, David Homeli Mwakyusa, Harold Nsekela, Gibbons Mwaipopo, Kingdom Mwakyusa, Anangisye Dick Mwandetele, Hardy Mwambingu, Jimmy David Ngonya, Bernard Mwambingu, Hezekia Mwakibete, Hosiana Mwangolombe, Kakoloboji Mwandanji, Rhodes Mwaikambo, Burton Mwaikambo, Bismarck Mwansasu, na wengi wengine. Hawa ni baadhi tu ya wana Rungwe waliosoma na JV hapo Mpuguso, baadhi wakiwa mbele yake, wengine wakiwa darasa moja na wengine wakiwa nyuma. Katika kitabu alichoandika kuhusu maisha yake, A Journey: My Life, Speeches & Writings, JV aliwakumbuka pia walimu wake wa Mpuguso, Johnson Kihampa, Amran Mayagila, Moses Mwakibete, Richard Mwakibete, na Dunstan Shauri. Wengi wa hao niliowataja, kama ilivyo kwa JV, wametutangulia mbele ya haki.
Niende kwa kasi katika kumbukumbu hizi. Tulikuja kukutana tena miaka ya 1980 JV akiwa mtumishi wa umma mwandamizi na mimi nikiwa Mwalimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kwa nafasi yake kama mwanafunzi wa zamani wa Chuo, na mimi kama Mwalimu chuoni tulikuwa wajumbe wa, ‘The Convocation of the University of Dar es Salaam – Convocation’, Kongamano la Wahitimu, Wanazuoni na Watendaji Waandamizi wa Chuo Kikuu, Kongomano ambalo lilianzishwa kwa mujibu wa Sheria Na 12 ya Mwaka 1970 iliyoanzisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Alikuwa hakosi kuhudhuria Kongamano, labda iwe kwa sababu ambazo hazikuweza kuzuilika, na alitoa michango yake kwa umakini, ushawishi na ustadi mkubwa. Mwaka 1988 nafasi ya Rais wa Kongamano ikawa wazi. Ndipo Mathew Luhanga na mimi, tukiwa wajumbe wa ‘Convocation’, tulipokubaliana JV angestahili kuchukua nafasi hiyo, pamoja na kwamba hakuwepo, kwa udhuru. Tukapanga mkakati wa ushawishi ili apate kura za kutosha. Kura zikatosha na JV akachaguliwa kuwa Rais wa ‘Convocation’, nafasi ambayo aliendelea nayo kwa kipindi cha miaka 16 mfululizo. Hatukukosea hata kidogo. Kwani sifa za utumishi wake kwa umma, katika sekta binafsi, katika diplomasia, na kwenye Jumuiya ya Afrika ya Mashariki zimeandikwa kwa undani na wengine, ikiwa pamoja na mpwa wake Andrew Bomani ambaye amewahi kusema, ‘Juma Mwapachu alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje bora, lakini ambaye hakuwahi kuwa Waziri!’. Sifa alizozieleza Andrew katika kumuomboleza mjomba wake baada ya kifo chake ndizo zilizokifanya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mwaka 2005, na Chuo Kikuu cha Rwanda, mwaka 2012 kumtunuku shahada za heshima uzamivu, Udaktari. Sikumbuki hata siku moja Juma akiitwa, tukimwita, au akikubali kuitwa Daktari Juma Mwapachu. Kenya walimtambua JV na mchango wake mkubwa wa kuimarisha Jumuiya ya Afrika ya Mashariki na Mzee Emilio Mwai Kibaki akamtunuku heshima ya ‘Moran of the Order of Golden Heart-(MGH)’. Sikumbuki kama Tanzania iliwahi kufanya hivyo. Hata hivyo ‘Msaafu’ unasema, “Nabii hutambuliwa kote isipokuwa nyumbani anakotoka”.
Niongeze kasi tena ninapokaribia kuhitimisha, nikikumbuka mambo matatu mengine yaliyotunganisha tena mwishoni. Ni heshima kubwa sana mwandishi wa kitabu akikualika kuwa mgeni rasmi na msemaji mkuu katika uzinduzi wa kitabu chake. Heshima hiyo niliipokea kwa unyenyekevu mkubwa nilipozindua kitabu cha Balozi Juma Volter Mwapachu kiitwacho, ‘Tanzania in the Age of Change and Transformation’, tarehe 17 Mei, 2018, hafla iliyohudhuriwa na familia yake na wageni wengi waalikwa, akiwepo rafiki yake mkubwa, sasa marehemu pia, Reginald Abraham Mengi (Mwenyezi Mungu Amrehemu). Mwaka 2019, kama kumbukumbu zangu ni sahihi, JV alipewa heshima ya kualikwa kuwa mgeni na msemaji rasmi kwenye uzinduzi wa kitabu cha Thabo Mbeki. Watu mbalimbali wameandika jinsi wanavyo mfahamu Thabo Mbeki, katika kitabu, ‘The Thabo Mbeki I Know’. Wazo lilimjia JV kwamba tungefanya hivyo pia kumkumbuka Mwalimu Julius Nyerere. Kwani wengi waliomfahamu Mwalimu walikuwa wanapungua. Wakati huo nilikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (Kivukoni). Akanishawishi tushirikiane kuifanya kazi hiyo. Nilikubaliana naye kwa imani kwamba huo ungekuwa mchango wetu wa Kumbukumbu ya Miaka 100 ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Kwa miaka miwili mfululizo tuliifanya kazi hiyo kwa ushirikiano wa karibu. Tulizunguka sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi, tukiambatana na Rose Mwapachu, Lucy Mwandosya na Max Mwandosya. Kitabu chetu, ‘28 Reflections on Mwalimu Julius Nyerere’, kilichochapishwa na Mkuki na Nyota Publishers Ltd, ni matokeo ya mchango mkubwa wa JV.
Jambo la pili ambalo liliunganisha familia zetu mbili ni changamoto za kiafya. Katika kipindi cha miaka 10 hivi iliyopita kuna nyakati ilikuwa nikimtafuta JV naambiwa yuko Afrika ya Kusini kwa matibabu. Naye mara nyingi akinitafuta anaambiwa niko Hyderabad, India kwa matibabu. Basi ilikuwa hivyo mpaka tarehe 28 Machi 2025 alipotutangulia. Tarehe 28 Machi 2026 ni mwaka mmoja tangu JV afariki. Kwa niaba ya familia yangu, na kwa niaba yangu mwenyewe, tunaendelea kutoa pole kwa mkewe mpendwa Rose Omari Mwapachu na kwa Hamza, Hamadi, na Haddiya. Tunatoa pole pia kwa Dada Rahma Mwapachu Bomani na ukoo wote wa Hayati Mark Bomani, na kwa Tunu Bugumba na Jabe Jabir. Natoa pole pia kwa Balozi Chirau Ali Mwakwere, ‘Msemaji Mkuu wa Wadigo wote (duniani)’ na mkewe Rose, marafiki zetu wa karibu sana. Huko aliko bila shaka JV amekutana na Mzee Hamza Kibwana Bakari Mwapachu, Mama Juliana Mwapachu, Harith Bakari Mwapachu, Harith Jr, na Wendo Mtega.
Nahitimisha kwa kutoa ushuhuda kwamba hakika Juma Mwapachu alikuwa Mtu. Alikuwa Mtu katika Watu. Alikuwa Mtu wa Watu. Chirau Mwakwere, rafiki yetu, ametafsiri Chidigo (Kidigo) sifa hizo za JV ifuatavyo: Jumaa kara ni mutu, Kara ni mutu pharipo atu. Kara ni mutu wa atu.
Hakika sisi sote ni wa Mwenyezi Mungu na Kwake Yeye Tutarejea. Aendelee Kupumzika kwa Amani.
Mark Mwandosya
Lufilyo, Busokelo
Machi 2026


