JUMATATU wiki hii taifa lilishuhudia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, akiwasilisha kwa Rais Samia Suluhu Hassan, taarifa ya ukaguzi wa hesabu za serikali kwa mwaka 2024/25. Kwa kifupi Kichere alisema hati zilizotolewa ‘zinaridhisha’ kwa kiwango cha asilimia 99 cha kaguzi 1,553 zilizokaguliwa kwa mwaka 2024/25.
Ukaguzi wa CAG kwa matumizi ya fedha za umma ni wajibu wa kikatiba. Ibara ya 143 ya Katiba ya Jumhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ndiyo inaunda ofisi ya CAG na majukumu yake. Kwa maneno mengine, kazi za CAG ni za kikatiba. Ni wajibu wa kuhakikisha kwamba rasilimali za umma hazitumiki kinyume cha taratibu. Na kila mwaka CAG anawajibika kuwasilisha ripoti ya ukaguzi kwa Rais kabla ya tarehe 31 ya mwezi wa Machi. Rais naye akiisha kuipokea ripoti hiyo haikakilii tu, anawajibika kuiwasilisha bungeni katika mkutano unaofuata ndani ya siku saba tangu kuanza kwa mkutano huo. Mkutano wa Bunge uliofuata baada ya CAG kuwasilisha ripoti kwa Rais mwaka huu, ulianza wiki hii Jumanne Machi 31, 2026.
Wakati sura ya ripoti ya ukaguzi ikionyesha hali njema katika matumizi ya fedha za umma, walau kwa kigezo cha hati za kuridhisha zilizotolewa, tafakari ya kina juu ya matumizi ya fedha za umma na hatua za udhibiti, inatoa picha tofauti.
Kwa mfano, ripoti ya CAG inasema kuwa kuna maamuzi ya matumizi ya fedha za umma katika miradi mikubwa ambayo hayakufuata taratibu za zabuni wala tathmini ya makadirio ya mradi katika hatua ya awali. Mfano mmojawapo uliotolewa na CAG ni ujenzi wa Uwanja wa Arusha ambao ulikadiriwa kujengwa kwa kwa Sh. bilioni 187, lakini mkataba wa ujenzi ukasainiwa ukionyesha thamani ya Sh. bilioni 338. Katika maelezo ya CAG, pia suala la kumpata mkandarasi (mzabuni) halikuwa wazi kwani kulikuwa hakuna ushindani na hakukuwa na sababu za kuonyesha mazingira ya kazi hiyo kupewa mzabuni mmoja pasi na ushindani.
Hali ya baadhi ya mashirika ya umma ambayo yanapewa ruzuku, imeelezwa kuzidi kuwa mbaya. Ama, yale yanayowasilisha ‘gawio’ serikalini ijapokuwa yanafanya hivyo, bado yanajiendesha kwa kutegemea ruzuku kutoka serikalini. Kwa maneno mafupi, mashirika haya ‘yako hoi’ hayajiendeshi kwa ufanisi.
Kama ilivyoelezwa hapo juu kwamba kazi ya CAG ni ya kikatiba, kuna changamoto kubwa ya utekelezaji wa mapendekezo yanayotolewa mwaka baada ya mwaka. Kwa tathmini ya kina, kuna ulegevu mkubwa sana wa utekelezaji wa mapendekezo ya CAG juu ya kutibu udhaifu mbalimbali unaoibuliwa na ofisi hiyo muhimu ya udhibiti wa rasilimali za umma.
CAG Kichere katika hatua hii ya ulegevu wa utekelezaji wa mapendekezo ya ripoti za ofisi yake ameamua kuwa muungwana. Amerusha mishale huku amevaa gloves za sufi ili pengine asisababishe fadhaa kubwa kwa walengwa. Aliweka wazi kwamba kuna changamoto kubwa katika utekelezaji wa mapendekezo ya CAG mwaka baada ya mwaka. Kwa mfano, kati ya mapendekezo 38,181 ya CAG katika ukaguzi wa hesabu za serikali na mashirika yake katika kipindi cha takribani miaka 20, utekelezaji wake umekuwa wa chini sana.
Alisema kuwa kati ya mapendekezo hayo, ni asilimia 36.7 sawa na mapendekezo 14,012 ndiyo yalitekelezwa kwa ukamilifu; aidha, asilimia 43.5 sawa na mapendekezo 16,608 yalikuwa katika hatua mbalimbali ya utekelezaji, huku asilimia 7.5 sawa na mapendekezo 2,863 yalikuwa hayajaguswa kabisa.
CAG alieleza bayana kwamba kushindwa kutekelezwa kwa mapendekezo hayo kunasababisha kutokutokea mabadiliko ya kiutendaji na uwajibikaji kwani mapendekezo hayo yalikuwa yanagusa chanzo hasa cha kuwapo kwa hitilafu kama zilivyofafanuliwa kwenye ripoti mbalimbali za CAG kwa miaka kadhaa sasa. Aligusia baadhi ya taasisi za umma kama Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yenye mapendekezo ambayo yamefikia miaka 17 bila kupatiwa ufumbuzi; na Bodi ya Korosho yenye mapendekezo yaliyofikia miaka 13 bila hatua kuchukuliwa. Alitaja pia Mamlaka ya Bahari yenye mashauri yaliyofikia miaka 15 bila kutatuliwa.
Katika hali inayoonyesha kama ni kukata tamaa, CAG alipendekeza kuwapo kwa chombo cha kufuatilia utekelezaji wa mapendekezo ya ofisi yake, ili kusaidia kutatua chanzo cha matatizo ya usimamizi mbaya wa rasilimali za umma.
Wakati CAG Kichere alieleza umuhimu wa kuwapo kwa chombo hicho, anakwepa kuweka wazi kwamba kikatiba chombo chenye mamlaka ya kuhakikisha mapendekezo ya ripoti ya ofisi yake yanatekelezwa bila kuacha shaka ni Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ibara ya 63 (2) inasema “Sehemu ya pili ya Bunge itakuwa ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Katiba hii.”
Madaraka haya ndiyo kiini cha ripoti ya CAG kuwasilishwa bungeni ikishawasilishwa kwa Rais, hata pale ambako Rais kwa sababu zake anaweza kuamua kutokuiwasilisha ripoti hiyo bungeni, CAG amepewa madaraka ya kikatiba kuiwasilisha ripoti hiyo kwa spika au naibu wa spika kulingana na mazingira yatakayokuwako. Haya ni masharti ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 143 (4). Bunge lina utaratibu wa kujadili ripoti ya CAG, kukagua kote alikoibua maswali na kutaka majibu kutoka serikalini. Bunge ndiyo mamlaka ya kuidhinisha bajeti ya serikali. Bila Bunge kuridhia serikali haiwezi kuibuka tu kukusanya kodi. Kila senti moja inayotumiwa na serikali ni lazima iidhinishwe na Bunge.
Nikitafakari kwa kina kauli ya CAG Kichere ananikumbusha kauli ya CAG aliyeondolewa kazini kwa hila kabla ya muda wake, Profesa Mussa Assad ambaye alipata kusema kuwa ‘Bunge ni dhaifu’ kauli iliyomsababishia mgogoro mkubwa kati yake na Spika wa zamani, Job Ndugai. Ugomvi mkubwa ulizuka kati ya Profesa Assad na Ndugai kiasi cha kumtaka ajiuzulu wadhifa wake kwa kuwa alikuwa amelidhalilisha Bunge kwa kutamka kuwa ni dhaifu. Kauli ya Prof. Assad kuwa Bunge ni dhaifu ilitokana na mahojiano aliyofanya na chombo kimoja cha habari akieleza kuwa ofisi yake inatekeleza wajibu wake, ila kama mapendekezo yake hayafanyiwi kazi, basi Bunge ambalo ndilo lenye dhima ya kuhakikisha utekelezaji wake, ni dhaifu.
Ni katika kuangalia ukweli huu, ninamuona CAG Kichere alizungumza lugha ya CAG Assad, lakini kwa mlango wa nyuma. Kimsingi wote wanataka Bunge liwajibike katika utekelezaji wa ripoti ya CAG.


