Matendo ya Polisi ni hujuma dhidi ya utawala bora, demokrasia

MFUMO wa uchumi wa soko huru una kanuni zake. Miongoni mwake ni kuruhusu ushindani. Ushindani kwenye kila uwanda. Ni mfumo unaotaka kile kinachostawi na kutamalaki kitokane na juhudi ya kazi bora, kujitoa na kuwekeza ili umma uamue.

Kwa mfano, soko huru halipaswi kuzuia mwenye nia ya kuwekeza katika sekta yoyote kufanya hivyo. Kanuni za mfumo wa uchumi wa soko zinaeleza bayana kuwa kutakuwa na sheria, kanuni na taratibu za kushiriki kwa mtu yeyote katika nyanja zote za kiuchumi, kisiasa na kijamii bila kubaguliwa.

Ni kwa minajili hiyo, uwekezaji katika sekta ya uchumi haumbagui yeyote mwenye kutaka kuwekeza, almradi anafuata sheria, kanuni na taratibu zilizokubalika. Vivyo hivyo katika uwanja wa kisiasa. Kila raia ana haki ya kuungana na wenzake kuanzisha chama cha siasa kwa mujibu wa sheria ya kuanzishwa kwa vyama vya siasa nchini.

Chama cha siasa kikishaandikishwa ni taasisi halali ya umma. Kina uhuru wa kufanya shughuli za kisiasa bila kuzingwa na kuwekewa mizengwe na yeyote. Chama cha siasa kinapaswa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizokubalika tu.

Ni jambo lisilokubalika na kwa kweli lisiloweza kueleweka kwa yeyote kwamba nchi iliyokubali kuingia katika mfumo wa ushindani katika uchumi na siasa, ikatunga sheria za namna ya kuenenda katika mfumo huo, inafika mahali inatumia mbinu ambazo siyo halali kuzuia wenye nia ya kufanya siasa halali kwa mujibu wa sheria kutekeleza azma yao.

Wahenga walituasa, ukipenda boga huna budi kulipenda na ua lake. Kwamba Tanzania kama taifa tangu tulipoanza mageuzi ya kiuchumi na kisiasa miaka ya 90, tuliamua kwa dhati kabisa kwamba nchi yetu itakuwa ni ya kidemokrasia inayoongozwa kwa ushindani wa vyama vingi; inayoendesha uchumi wake katika ushindani wa soko; unaoruhusu mawazo huru kwa kila raia wake; inayoheshimu sheria, kanuni na taratibu zilizokubalika.   

Ni katika uelewa huo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ilifanyiwa marekebisho ili kuruhusu mazingira ya kisheria ya kuwako kwa mfumo huo. Kimsingi, mwaka 1992 ndipo mabadiliko haya yalifanyika, huku mabadiliko ya sera na sheria za kiuchumi yakiwa yamekwisha kuanza mapema zaidi kwa kuruhusu mfumo wa soko huru katika uchumi kufanya kazi, mfumo wa uchumi hodhi wa dola ulifungasha virago.

Leo ni mwaka 2026, miaka takribani 34 katika mfumo wa uchumi wa soko na demokrasia ya vyama vingi. Umri wa miaka 34 siyo haba. Ni umri wa kijana aliyekomaa kiasi cha kuanza kubeba majukumu makubwa yake binafsi, ya jamii na hata pengine kwa taifa lake.

Ukitafakari hali ya mfumo wa kisiasa unavyoendeshwa nchini kwa sasa, unapata hisia kwamba huenda kuna watu ndani ya mamlaka ya dola hawataki tena uwepo wa vyama vingi vya siasa nchini. Hisia hizi zinaongezewa nguvu kila uchao kwa kuangalia na kutafakari mwenendo wa Jeshi la Polisi dhidi ya vyama vya siasa vya upinzani.

Ni hivi majuzi tu Jeshi la Polisi lilifurusha mabomu ya kutoa machozi dhidi ya wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoani Mara ambao walikuwa wameamua kufanya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani kwa staili waliyoamua kuifanya wao. Hawakuishia hapo tu, majuzi tena hapa, Jeshi la Polisi Machi 15, 2026 lilizuia mkutano wa Ngome ya Wanawake wa chama cha ACT Wazalendo uliokuwa ufanyike kwenye uwanja wa Kawawa mkoani Kigoma kwa kile Polisi walichodai kuwa wenye uwanja wao, hawakuwa wametoa ruhusa ya kufanyika kwa mkutano huo.

Kwa ujumla kumekuwa na tabia ya kufanana ya Jeshi la Polisi katika mikoa yote ya Tanzania. Hii ni ya kuzuia kwa makusudi na kwa visingizio mbalimbali mikutano yote ya vyama vya upinzani. Waathirika wakuu wa tabia na maamuzi haya yanayokinzana moja kwa moja na uwepo wa mfumo wa vyama vingi nchini, ni wafuasi wa Chadema na ACT Wazalendo. Haiyumkiniki kama ipo amri au maelekezo yametoka mahali fulani kwa mwenendo huu wa Jeshi la Polisi, ila jambo moja liko dhahiri, kwamba kuna juhudi kubwa inafanyika kuuvuruga, kufisha na kuua mfumo wa siasa za ushindani ndani ya nchi hii.

Juhudi hizi zinaonekana kuwa mikononi mwa Jeshi la Polisi. Kwa kifupi ni hivi, sasa haki ya wananchi kufanya shughuli za kisiasa kama vyama vya siasa kufanya mikutano yao, kuendesha shughuli za kuhamasisha wananchi wawaunge mkono, zimepokwa na Jeshi la Polisi ambao sasa wamejipa mamlaka ya kuamua nani afanye siasa na nani asifanye. Hatari kubwa!

Sasa tunakaribia muongo mmoja tangu hila za kuhujumu mfumo wa demokrasia ya vyama vingi ulipoasisiwa rasmi mwaka 2016. Wapo watu walidhani kwamba wimbi la hujuma zile zingepita na utawala wa awamu ya tano, haikuwa hivyo. Tumeona na kushuhudia hali ya kisiasa nchini ikizorota na kufifia kila uchao. Tumeona na kuthibitisha pasi na shaka yoyote kwamba kuna njama zinasukwa sirini na pengine hadharani za kuua uzuri na manufaa yote ya ushindani wa kisiasa wa vyama vingi nchini. Mfumo ambao faida yake kubwa ni kujenga uwajibikaji na kurejesha madaraka kwa wananchi kwa mujibu wa ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Hali hii ni aibu kubwa kwa taifa letu, nchi iliyokuwa imefikia viwango vya juu kabisa vya siasa za ushindani za vyama vingi. Tuliona watu wakipingana kwa hoja. Tulishuhudia watu wakiwajibishana kwa mujibu wa sheria. Lilishuhudiwa Bunge likiwa ni chombo halisi cha uwakilishi wa wananchi na msimamizi wa kweli wa serikali kama ilivyoshuhudiwa kati ya mwaka 1995 hadi 2015. Leo hii ufuasi wa vyama vya upinzani unanasabishwa na uasi, ugaidi na uhaini. Ni aibu kwa Jeshi la Polisi lenye dhima ya kulinda raia na mali zao, kujipa jukumu la kuhujumu mfumo wa siasa za vyama vingi kwa matendo yao dhidi ya wanachama na viongozi wa vyama hivyo.

Neno moja tu lafaa kuhitimisha hapa, uchumi imara hauwezi kustawi bila mfumo imara na dhabiti wa siasa za ushindani zinazokuza uwajibikaji. Kama Jeshi la Polisi linaamini kuwa linasaidia walioko madarakani, lijue tu matendo yake ni chanzo kikuu cha chuki ya wananchi dhidi yao. Matendo ya polisi yanasaidia kubariki ulegevu na kutokuwajibika kwa wenye madaraka, kwa kuwa wanajua wananchi wamepokwa fursa ya kuwawajibisha kwenye sanduku la kura.

spot_img

Latest articles

Dkt. Mataragio: Serikali haitasita kuwachukulia hatua kali wanaoficha mafuta

Na Tatu Mohamed SERIKALI imetoa onyo kali kwa wafanyabiashara wanaojihusisha na vitendo vya kuficha...

Lukuvi afariki dunia

Na Mwandishi Wetu WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye...

Mgodi wa kihistoria wa niobium kujengwa Mbeya

Na Mwandishi Mbeya TANZANIA imepiga hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na Marekani baada...

Ndejembi ataka Ewura kukagua maghala ya mafuta kuhakikisha hakuna mafuta yanayofichwa

📌Asema nchi ina usalama mkubwa wa mafuta hivyo wananchi waendelee kupata huduma muda wote 📌Timu...

More like this

Dkt. Mataragio: Serikali haitasita kuwachukulia hatua kali wanaoficha mafuta

Na Tatu Mohamed SERIKALI imetoa onyo kali kwa wafanyabiashara wanaojihusisha na vitendo vya kuficha...

Lukuvi afariki dunia

Na Mwandishi Wetu WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye...

Mgodi wa kihistoria wa niobium kujengwa Mbeya

Na Mwandishi Mbeya TANZANIA imepiga hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na Marekani baada...