‘Umimi’ wa viongozi unaua Jumuiya Afrika Mashariki

KATIKATI ya miaka ya 90 wakati mfumo wa vyama vingi unaota mizizi, lilitokea wazo la kuunda ushirika dhabiti miongoni mwa vyama vya siasa vya upinzani, ili kuingia katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 kwa kishindo katika kukikabili chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Katika juhudi hizo vyama vilipanga kuunda Umoja wa Demokrasia Tanzania (UDETA). Vyama vilivyokuwa katika vuguvugu hilo ni pamoja na NCCR-Mageuzi, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Chama cha Wananchi (CUF) na vingine kadhaa.

Nia ya awali ilikuwa kuwa na wagombea wa pamoja katika ngazi za urais na ubunge ili kuepuka kugawanya kura, hivyo kukipa chama tawala nafasi nzuri ya kushinda uchaguzi huo. Na isivyo bahati, nia hiyo haikufika mbali. UDETA ilikufa hata kabla ya kuota mzizi wowote wa maana wa kisiasa. Vyama vingi havikukubaliana na wazo la ushirika huo, sababu kubwa ilioenekana ni kutokuaminiana miongoni mwa vyama vyenyewe na tamaa ya kila kiongozi kutaka chama chake kipate.

Nimeikumbuka UDETA baada ya kuona maamuzi ya wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) yaliyofikiwa hivi karibuni Jijini Arusha katika kuifufua dhidi ya mzigo wa madeni. Kwamba jumuiko hili, EAC, lenye nchi wanachama nane, ni miongoni mwa majumuiko makubwa katika bara la Afrika. Jumuiko hili linaunganisha nchi zenye jumla ya wakazi wapatao milioni 340 hadi milioni 345. Hawa ni watu wengi. Ni hazina kubwa ya nguvu kazi, soko la bidhaa na huduma mbalimbali, pia ni rasilimali inayoweza kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi kwa ukanda wote.   

Jumuiko hili linaziunganisha Kenya, Uganda na Tanzania zikiwa ndizo kitovu cha jumuiya hii kihistoria na hata sasa, pia zikiwamo Rwanda, Burundi, Sudan ya Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Somalia. Hili ni eneo lenye rasilimali nyingi sana. Madini ya kila aina, uoto wa asili – misitu mikubwa, maji- maziwa makuu kama Ziwa Viktoria, Tanganyika, Nyasa, Albert, Rudolf, Kivu; na mito mikubwa.

Kwa Tanzania ipo mito mikubwa kama Rufiji, Pangani, Wami, Ruvuma na Malagarasi; Kenya ipo

Tana, Athi-Galana-Sabaki, Ewaso Ng’iro na Nzoia; Uganda ipo Nile, Albert, Kagera unaounganisha pia Tanzania na Rwanda, pia upo mto Katonga; Rwanda ipo mito ya Nyabarongo, Akanyaru na Kagera. Kwa Burundi ipo mito ya Ruvubu, Malagarasi na Kanyaru. Nchini Sudan Kusini ipo White Nile, Bahr el Ghazal na Sobat. DRC wamejaliwa utitiri wa mito kama Congo, Lualaba na Semliki. Somalia nako kuna Jubba na Shabelle. Kwa sura ya mito hii tu inaeleza kuwa eneo la jumuiko la EAC limejaa neema. Neema ya rasilimali zote. Ardhi, madini, mbuga na misitu.

Madhumuni makuu ya EAC ni kujenga nguvu ya kiuchumi ya pamoja – soko la pamoja, umoja wa forodha, na mwisho shirikisho la kisiasa.

Mambo haya ni makubwa. Ni nia kubwa. Ni Malengo makubwa ya watu makini. Isivyo bahati, nchi nyingi wanachama wa EAC zimekuwa legevu sana katika kuishi ndoto hii. Kwa miaka sasa nchi wanachama zimekuwa legevu katika kutoa michango yao ya kisheria ya kuhakikisha Jumuiya inatekeleza majukumu yake. Nchi nyingi zimelimbikiza madeni mengi. Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki wamekopwa mno mishahara yao kwa kuwa fedha za kuendesha Jumuiya hazipo. Matokeo yake hata majukumu ya sekretariati yanayumba kwa sababu ya ukata unaotokana na nchi wanachama kushindwa au kuzembea tu kupeleka ada na michango yao kwa wakati.

Ni katika kukabiliana na mgogoro huo wa nchi kutokupeleka ada kwa Jumuiya, mkutano wa Wakuu wa Jumuiya waliokutana Arusha walifanya maamuzi ya kurejesha baadhi ya wajibu wa kuhudumia majukumu ya Jumuiya kwa nchi wanachama. Miongoni mwake ni nchi wanachama sasa zitawajibika kulipa mishahara ya wabunge wake wanaoiwakilisha katika Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki. Katika maamuzi hayo, sasa Jumuiya itakuwa inalipa tu posho za wabunge.

Uamuzi huu unachukuliwa kama mbinu ya kuipunguzia Jumuiya mzigo wa madeni, kwa kufanya hivyo unaongeza wajibu kwa nchi wanachama kubeba dhima ya kuwahudumia wabunge wake kwenye Jumuiya.

Hatua hii itakuja kama suluhu ya kuondoa ugonjwa wa kuchelewesha mishahara ya wabunge, hivyo kulifanya Bunge la Jumuiya kutekeleza wajibu wake kwa wakati unaokubalika kulingana na mkataba wa kuanzishwa kwa Jumuiya hiyo.

Hata hivyo, hatua hizi zitakuwa na machungu yake. Mojawapo ni kupungua kwa nguvu ya pamoja ya Jumuiya. Kwa dhana ya mlipa zumari ndiye achaguaye wimbo, ina maana kwamba uaminifu wa wabuge hawa sasa utahama kutoka Bunge la Jumuiya kwenda serikali za nchi wanachama. Uimara wa Jumuiya sasa unakwenda kuathirika. Kwa maana hiyo Bunge hili linageuka kuwa jumuiko la wawakilishi (delegates) wa nchi wanachama na siyo Bunge halisi la Jumuiya. Kuna uwezekano mkubwa nguvu ya pamoja ya Bunge la Jumuiya inakwenda kuathirika kwa kuwa nguvu ya fedha ya Jumuiya na wajibu wake kwa wote wanaotekeleza majukumu inapunguzwa.

Wakati Wanajumuiya ya Afrika Mashariki wanapokea maamuzi haya makubwa na magumu katika uendeshaji wa EAC, yafaa pia kujiuliza swali, ni kwa nini wakuu wa nchi za Jumuiya hawaoni umuhimu wa kuhudumia chombo hiki muhimu kwa ajili ya ustawi wa wananchi wake.

Yawezekana sana roho ile ile iliyoua UDETA miaka ya katikati ya 90 kiasi cha vyama vya siasa kuona kwamba kila kimoja kinaweza kujiendesha chenyewe, kikaingia kwenye uchaguzi mkuu chenyewe, kikajipanga chenyewe na mikakati yake, kuwa kinaweza kushinda uchuguzi na kuikabili CCM, ndiyo inasumbua ndani ya Jumuiya hii. Kwamba nchi wanachama zinadhani kwa kuitazama Jumuiya kama kitu chepesi tu, kitu kisicho na nguvu, wanaweza kustawi kivyao na bila jumuiko hilo muhimu.

Hakuna ubishi kwamba nchi zote wananchama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zina rasilimali za kutosha za kuiendesha kifedha Jumuiya, kinachokosekana ni utayari na utashi tu wa kufanya hivyo. Kama vile wanasiasa wa Tanzania walivyopuuza UDETA miaka ile, wameendelea kuhangaika na siasa zisizo na kishindo kwa miaka zaidi ya 30 sasa. Ndoto yao ya kupata madaraka ya dola haionekani ikitimia katika miaka ya hivi karibuni, vivyo hivyo nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zisahau maendeleo ya kweli ya watu wao kama watapuuza nafasi ya Jumuiya kama nguzo muhimu ya kuwasukuma kwa pamoja kwa maendeleo ya kweli.

spot_img

Latest articles

Wanafunzi watatu wafariki dunia baada ya kupigwa na radi Dar

Na Mwandishi wetu WANAFUNZI watatu wa Shule ya Msingi Msongola iliyopo eneo la Msongola,...

Serikali yawataka Wakurugenzi kuongeza thamani inayopimika katika uwekezaji wa hisa chache

Na Mwandishi wetu SERIKALI imewataka wakurugenzi wa bodi za kampuni ambazo ina umiliki wa...

Tanesco yazindua ndege nyuki (Drones) kuboresha miundombinu ya umeme nchini

📌Ni sehemu ya utekelezaji wa mikakati yake kuimarisha huduma kwa wateja kwa kutumia njia...

Senegal yavuliwa ubingwa wa AFCON 2025, wapewa Morocco

Na Mwandishi Wetu SENEGAL imevuliwa ubingwa  wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 baada...

More like this

Wanafunzi watatu wafariki dunia baada ya kupigwa na radi Dar

Na Mwandishi wetu WANAFUNZI watatu wa Shule ya Msingi Msongola iliyopo eneo la Msongola,...

Serikali yawataka Wakurugenzi kuongeza thamani inayopimika katika uwekezaji wa hisa chache

Na Mwandishi wetu SERIKALI imewataka wakurugenzi wa bodi za kampuni ambazo ina umiliki wa...

Tanesco yazindua ndege nyuki (Drones) kuboresha miundombinu ya umeme nchini

📌Ni sehemu ya utekelezaji wa mikakati yake kuimarisha huduma kwa wateja kwa kutumia njia...