Na Tatu Mohamed
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Balozi Waziri Salum, amelipongeza Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) kwa kazi kubwa linayofanya katika kukuza ubunifu na sekta ya viwanda nchini, huku akiiagiza kuongeza juhudi za kujitangaza ili wananchi waelewe kikamilifu huduma na fursa zinazotolewa na shirika hilo.
Akizungumza leo Februari 19, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya kikazi katika ofisi za TIRDO, amesema kuwa Shirika hilo lina jukumu muhimu la kufanya tafiti za viwanda, kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wazalishaji, pamoja na kuendeleza ubunifu unaochochea maendeleo ya sekta ya viwanda nchini.

“Tunapongeza jitihada kubwa zinazofanywa na TIRDO, lakini bado kuna haja ya kuhamasisha wananchi zaidi kuhusu shughuli hizi. TIRDO iendelee kujitangaza, itumie vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, na uwakilishe fursa hizi kwa wananchi ili kila mmoja aweze kunufaika,” amesema Balozi Salum.
Amesisitiza kuwa kuongezeka kwa uelewa wa jamii kuhusu huduma za TIRDO kutasaidia wazalishaji kuboresha ubora wa bidhaa zao na kuongeza ushindani wa bidhaa za Kitanzania soko la ndani na nje ya nchi.

Pia ameitaka TIRDO kuwa kitovu cha utafiti wa viwanda na ubunifu, huku akisisitiza umuhimu wa kuwafikia vijana zaidi ili waweze kutumia fursa zilizopo.
Aidha, Balozi Salum ametoa wito kwa watumishi na taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara wkuwa wabunifu, waaminifu na chachu ya maendeleo, badala ya kuwa vikwazo kwa waanzilishi wa viwanda na biashara nchini.
“Taasisi zetu zinafanya kazi kubwa sana, lakini hazijitangazi. Nimezielekeza zitoke nje, zitangaze kazi wanazozifanya kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, na pia zikaribishe wananchi kuja kuona ubunifu unaofanyika,” amesema.

Ameongeza kuwa Wizara itaendelea kuwasaidia wafanyabiashara wadogo na wakubwa ili waweze kutimiza ndoto zao kwa urahisi zaidi.
Katibu Mkuu pia ametoa wito kwa Wizara na Taasisi zake kufanya kazi kwa weledi ili kuhakikisha biashara zinafanyika na Viwanda vingi vinajengwa.
“Tusimame pamoja kuhakikisha biashara inafanyika na viwanda vingi vinajengwa kwa wingi. Tufanye kazi kwa weledi, kwa utu, lakini kikubwa zaidi tuchape kazi na tubadilike,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TIRDO, Prof. Mkumbukwa Mtambo, amesema Shirika limefarijika na maelekezo yaliyotolewa na Katibu Mkuu, huku akiahidi kuongeza jitihada za kujitangaza ili wananchi waelewe kikamilifu kazi za TIRDO na fursa za ubunifu zinazopatikana.

“Ziara hii imetupa motisha kubwa. Tutaendelea kuhakikisha wananchi, hususan vijana, wanajua tunachofanya na jinsi wanavyoweza kushirikiana nasi ili kukuza sekta ya viwanda nchini,” amesema Prof. Mtambo.


