Na Mwandishi Wetu
Benki ya CRDB Bank kupitia CRDB Bank Foundation kwa kushirikiana na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na Kampuni ya Basil Link wamezindua mpango wa kimkakati wa ‘Imbeju – SmartElite’ wenye lengo la kuwawezesha vijana wa Kitanzania, hususan wanafunzi wa vyuo vikuu, kupata ujuzi wa kidijitali, elimu ya fedha na vifaa vya kisasa kwa ajili ya kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali.
Uzinduzi huo uliofanyika jijini Dar es Salaam umeelezwa kuwa sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo inayohamasisha ujenzi wa uchumi wa kidijitali unaojumuisha vijana kama nguvu kazi kuu ya taifa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa, amesema mpango huo unalenga kuibua na kukuza vipaji vya vijana wenye mawazo bunifu lakini wanaokabiliwa na changamoto ya mtaji na vitendea kazi.

Alisema vijana wengi wamekuwa wakilalamikia ukosefu wa mitaji licha ya kuwa na mawazo mazuri ya biashara, akisisitiza kuwa sasa ni wakati wa kutumia fursa zinazotolewa kupitia mpango huo kwa nidhamu na uwajibikaji, hasa katika urejeshaji wa mikopo ili kuwapa nafasi wengine kunufaika.
“Tunataka kuona vijana wanachangamkia fursa, wanabuni, wanaanzisha biashara na hata kuajiri wengine. Hii si tu kuwasaidia kumaliza chuo, bali kuwaandaa kuingia katika uchumi wa kidijitali wakiwa tayari na ujuzi pamoja na rasilimali,” amesema Mwambapa.
Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa CRDB na Ofisa Biashara Mkuu, Fredrick Nshekanabo, amesema mpango huo utasaidia kutatua changamoto ya vitendea kazi kwa wanafunzi kwa kuwapatia kompyuta na mbinu za uendeshaji biashara, hivyo kuongeza tija katika masomo na ubunifu wao.

Naye Mkurugenzi wa Uchambuzi na Upangaji Mikopo kutoka HESLB, Dkt. Peter Mmari, amesema ushirikiano huo ni utekelezaji wa maelekezo ya Serikali yanayozitaka taasisi za umma kushirikiana na sekta binafsi kuboresha utoaji wa huduma.
“Kupitia mpango huu, wanafunzi wataongeza uwezo wa kutumia mifumo ya kidijitali na watapata fursa ya kujiajiri wakiwa vyuoni au baada ya kuhitimu. Tunaamini wataweza pia kutoa mchango katika kuwainua Watanzania wengine kielimu na kiuchumi,” amesema Dkt. Mmari.

Mkurugenzi wa Basil Link, Emmanuel Basil, amesema kampuni hiyo imebuni programu ya Imbeju – SmartElite kwa lengo la kuwapatia vijana mafunzo ya ujuzi wa kidijitali, elimu ya fedha, maarifa ya ujasiriamali pamoja na vifaa vya kidijitali vitakavyowasaidia kuanza au kukuza shughuli zao za kiuchumi.
Amesema uzinduzi huo ni mwanzo wa safari ya matumaini mapya ya kujenga kizazi kinachojiamini, chenye ubunifu na uwezo wa kushindana kimataifa huku kikichangia kikamilifu maendeleo ya Tanzania.

Washiriki wa hafla hiyo wameeleza kuwa mpango wa Imbeju – SmartElite ni mwanga mpya kwa vijana waliokuwa wakikabiliwa na changamoto za upatikanaji wa vitendea kazi na mikopo, na wametoa wito kwa wadau mbalimbali kuunga mkono jitihada hizo ili kupanua wigo wa uwezeshaji na kukuza uchumi wa kidijitali nchini.


