Na Mwandishi wetu
BENKI ya CRDB imezindua kampeni yake ya mwaka 2026 inayoitwa ‘Benki Kimpango Wako’ inayolenga kuboresha huduma kwa wateja kwa kupunguza muda wa kukamilisha muamala na kumruhusu mteja kujihudumia vile atakavyo, kwa muda wake akiwa mahali popote duniani.
Kampeni hiyo imezinduliwa leo Februari 03, 2026 na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela ambaye amewashukuru wateja, wawekezaji, wabia wa kimkakati pamoja na wadau wote kwa ujumla kwa imani waliyonayo kwa benki hiyo.

Amesema mwaka 2025 umekuwa ni mwaka wenye mafanikio kwa Benki hiyo ambapo imefanikiwa kupata faida ya zaidi ya shilingi trilioni 1.04 kabla ya Kodi sawa na ukuaji wa asilimia 33, huku faida baada ya kodi ikifika shilingi bilioni 725 likiwa ni ongezeko la asilimia 31 ikilinganishwa na mwaka 2024.
Amefafanua kuwa, Mizania yake nayo imeongezeka na kufika shilingi trilioni 22.2 sawa na ukuaji wa asilimia 33 na ndani ya kipindi hicho imetoa mikopo kiasi cha shilingi trilioni 13.7 sawa na ukuaji wa asilimia 32.6.
“Mwaka jana tumepata faida kubwa kutokana na ushirikiano mkubwa tulioupata kutoka kwa wateja binafsi, wajasiriamali, taasisi, mashirika na serikali pamoja na wabia wetu. Ninyi ndiyo sababu ya uwepo wa Benki ya CRDB.

“Kila akaunti mliyofungua, mkopo mliouchukua, kila muamala mlioufanya, na kila mradi mlioutekeleza kupitia Benki ya CRDB vilitupa nguvu na ari ya kujituma zaidi. Ninaamini na kuomba ushirikiano huu uendelea mwaka huu pia,” amesihi Nsekela.
Amesema ukuaji huo unamaanisha uwezo mkubwa zaidi wa benki hiyo katika kufadhili miradi ya maendeleo, kusaidia kukuza mitaji ya biashara ndogo, za kati na kubwa, kuongeza uzalishaji, kutoa ajira mpya, na kuwawezesha vijana, wanawake na wajasiriamali kutimiza malengo yao ya kiuchumi.

“Mafanikio haya yana akisi ushirikiano wa wadau wetu wote. Tutaendelea kutekeleza azma yetu ya kuboresha maisha ya watu wetu na uchumi wa Taifa letu pamoja na masoko mengine ambako benki yetu inatoa huduma. Sisi ni Benki inayomsikiliza Mteja na kwa kufanya hivyo tunapata suluhisho la kila changamoto ya mteja,” amesema Nsekela.
Amesema wateja wanahitaji huduma za fedha ambazo ni rahisi, za haraka, na zinazoendana na mikakati waliyonayo ndio maana Benki ya CRDB imekuja na kampeni ya Benki Kimpango Wako ikikusudia na kuahidi kutoa kipaumbele kwa wateja na wadau wengine ambao ni sehemu ya mafanikio yake ya kibiashara.
Amebainisha kuwa jitihada hizo za kuboresha na kuimarisha huduma kwa wateja na wadau wengine wa Benki ya CRDB, zilianza mwaka jana pale walipofanya maboresho ya mfumo mkuu wa uendeshaji (core banking system) yakilenga kuiweka benki katika viwango vya kimataifa vya utoaji huduma na mapema mwaka huu wakazindua ofisi ya uwakilishi Dubai.

“Maboresho yetu ya mfumo mkuu wa uendeshaji wa yalilenga kubadilisha namna Benki inavyofanya kazi na jinsi mteja anavyopata huduma. Leo tunazindua kampeni tunayoiita Benki Kimpango Wako.
“Tunawahakikishia Watanzania na wateja wetu wengine popote duniani kuwa Benki yetu ya CRDB ni mbia wa uhakika na wa kutumainiwa katika upatikanaji wa huduma za fedha. Mwaka 2026 tunawaahidi huduma bora na za uhakika zaidi,” amesema Nsekela.
Kuhusu uzinduzi wa kampeni ya Benki Kimpango Wako, Nsekela amesema umefanyika katika kipindi muhimu kwa historia ya taifa wakati serikali ikianza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayoelekeza kuwa uchumi wa Tanzania unapaswa kuwa jumuishi, wenye huduma za fedha zilizowafikia wananchi wengi zaidi, na taasisi za fedha kuwa nguzo ya ukuaji wa uchumi, ubunifu na ustawi wa jamii.
“Benki ya CRDB ni daraja la fursa kwa wananchi wote. Kampeni ya Benki Kimpango Wako inamkumbusha kila mdau kwamba Benki ya CRDB ni mshirika wa kutumainiwa katika safari ya maendeleo kwa mpango wa mteja katika muda wake,” amesisitiza Nsekela.


