Na Winfrida Mtoi
KIPA wa zamani wa Yanga na timu ya Taifa ya Tanzania, Peter Manyika amefariki dunia leo Januari 26, 2025, wakati akiwa anapatiwa matibabu katika hospitali ya St. Monica, jijini Dar es Salaam.
Familia kupitia mtoto wake, Manyika JR imethibitisha kuwa baba yake amefariki, mwili umehifadhiwa katika hospitali ya Mwananyamala, na msiba upo nyumbani kwao Mbezi.
Manyika atakumbukwa katika historia ya soka nchini kama miongoni mwa makipa bora waliojipatia heshima kubwa nchini akiwa na Yanga na timu ya Taifa kuanzia miaka ya mwishoni mwa miaka ya 1980 na 1990.

Mwaka 1999 aliiongoza Yanga kutwaa ubingwa wa Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati mwaka 1999 nchini Uganda.
Baada ya kustaafu soka la ushindani, hakuachana na mchezo huo, aliamua kujikita katika ukocha wa makipa na kuendeleza vipaji, akifanya kazi na klabu mbalimbali zikiwamo Ihefu, Fountain Gate na timu za taifa za vijana.
Mwaka 2019 klabu yake za zamani, Yanga ilimpa jukumu la kuwanoa makipa wa timu hiyo akichukua nafasi ya Juma Pondamali, kipindi hicho alikuwa ni Metecha Mnata, Faroukh Shikalo, Klaus Kindoki na Ramadhan Kabwili.


