KUMEKUWA na mjadala wa wiki kadhaa sasa ukimlenga Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba, kwa kuwa tu alitoa maoni yake juu ya hali ya kisiasa ilivyo nchini. Jaji Warioba ambaye pia alipata kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wakati wa utawala wa awamu ya pili, anashambuliwa mithili ya mtu aliyetenda uovu. Anaandamwa na watu wenye mwelekeo wa siasa za kihafidhina, wanaotamani kila sauti huru inayosimama kukemea uovu, kukataza uonevu na kueleza ukweli wa mambo ulivyo katika taifa letu, afungwe jiwe kubwa shingoni na kutoshwa katika kilindi baharini.
Isivyo bahati, wahafidhina hawa wanasahau kwamba uelewa wa Watanzania katika zama za sasa ni wa kiwango cha juu kabisa. Wapo watungaji na wafinyanga uongo dhidi ya Jaji Warioba wakitamani asisikike kokote. Uongo huu ambao wanataka kuusadikisha kwa umma, nia yao ni moja tu – kutaka kuua na kufisha kila sauti huru ya kweli iliyobakia nchini kwa sasa.
Jaribio la kwanza kabisa la kutaka kubeza uadilifu, uzalendo na msimamo usiyoyumba wa Jaji Warioba katika kusimamia ukweli, ulianza siku ya mazishi ya aliyekuwa Waziri Mkuu David Cleopa Msuya. Jaribio hilo lilitengenezwa kwa mbinu za kujificha na Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete wakati anatoa salamu zake za rambirambi kwa wafiwa. Katika sifa nyingi alizozitoa kuhusu Msuya, Kikwete alidai kuwa hakuwa mtu wa kuitisha mikutano na waandishi wa habari kuisema serikali. Ila, alikuwa anakwenda kuonana na viongozi na kutoa mawazo yake. Alilisema hili la kutokuitisha mikutano na waandishi wa habari kwa hakika akiwa ni kama mtu anayetupa jiwe gizani, lakini akimlenga mtu mahususi. Kwa wale wanaojua kuunga mambo walijua kuwa kauli ya Kikwete ilikuwa ikimlenga Jaji Warioba.
Ni Jaji Warioba ambaye amekuwa muwazi kabisa kukosoa, kueleza maoni yake na kueleza kwa uwazi wa juu kabisa hali ya kisiasa na kidemokrasia na utawala ilivyo nchini, siyo sasa tu na hata hapo kabla. Amekuwa akieleza mambo haya siyo kwa uficho, wala siyo kwa nia kujitafutia uhalali au umaarufu wowote, bali ni katika kutaka kuimarishwa kwa mfumo wa utawala, uwajibikaji na demokrasia ambayo inawapa wananchi haki ya kuiwajibisha serikali yao. Warioba tangu kuumbwa kwa misingi ya dunia, hajawahi kuacha kusimama na kusema ukweli. Kueleza mambo bayana. Anasema hivyo huku akiwa ni mwanachama wa CCM. Anasema hivyo akitambua na kujua kuwa ni miongoni mwa viongozi wastaafu.
Kauli hii ya Kikwete kuhusu sifa za Msuya isivyo habati, imemezwa nzima nzima na baadhi ya watu bila kuitafakari. Baadhi yao ni makada na viongozi vijana wa kipindi cha sasa, wakiamini kwamba anachofanya Jaji Warioba ni uasi, ni chukizo, ni jambo lisilofaa kwa mtu aliyewahi kushika nafasi ya Waziri Mkuu Mstaafu na Makamu wa Rais kuikosoa serikali. Kwamba kukemea uovu wazi wazi, siyo sawa. Makada hawa wanaungana na watawala wetu kutaka watu wakemee mambo sirini, ili umma usijue. Kikubwa ili kusiwe na msukumo wa kutaka uwajibikaji. Yaishie huko huko sirini.
Ni katika dhana hiyo, mwishoni mwa wiki iliyopita Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenani Kihongosi, alizungumza na waandishi wa habari, na miongoni mwa rejea aliyoifanya ni hii ya Kikwete kuhusu Jaji Warioba. Kwamba kitendo cha Jaji Warioba katika siku za hivi karibuni kuzungumza na vyombo vya habari, kuikosoa serikali na kutaka hatua zichukuliwe hasa kutokana na matukio ya Oktoba 29, 2025 ni kama kuleta taharuki katika nchi. Kenani mwanasiasa mchanga kabisa amejipa mamlaka ya kubishana na Jaji Warioba akimtaka atulie kama mstaafu.
Ukitafakari kwa kina hoja ambayo iliasisiwa kwa mbinu ya uficho na Kikwete kwenye msiba wa Msuya, utaona jambo kubwa la kutengenezwa. Nitafafanua.
Mosi, siyo kweli kwamba Msuya alikuwa hazungumzi na vyombo vya habari. Siyo kweli. Binafsi nikiwa Mhariri Mkuu wa Gazeti la Nipashe, tulipata kufanya naye mahojiano (exclusive interview) juu ya mambo mengi, yakiwamo ya kisiasa na uchumi. Tuliomba fursa ya kukutana naye na kufanya naye mahojiano. Tulipewa. Binafsi nilifika nyumbani kwa Mzee Msuya eneo la Upanga jijini Dar es Salaam, nikiongozana timu ya Nipashe kwa kazi hiyo. Kwa maana hiyo, kwamba Mzee Msuya hakuwa anazungumza kabisa na vyombo vya habari siyo kweli. Mahojiano haya yapo kwenye kumbukumbu za gazeti la Nipashe!
Pili, dhana kwamba siyo sahihi kiongozi mstaafu kuzungumza na vyombo vya habari kueleza maoni yake juu ya utawala wa nchi, ni potofu sana. Kama kutoa maoni kwa kiongozi mstaafu ni upotofu, basi Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere atakuwa kinara kwa upotofu huu. Mwalimu Nyerere hakufanya mikutano na waandishi wa habari tu kueleza maoni yake, tena kwa sauti ya ukali sana, alifanya hivyo katika maeneo mengi.
Kwa mfano, Mwalimu Nyerere alipata kutumia sherehe ya Mei Mosi kitaifa na kueleza jinsi serikali ilivyokuwa inaendesha vibaya sera ya ubinafsishaji wa mashirika ya umma. Mwalimu hakutumia maneno mepesi kueleza kutokuridhishwa kwake na sera hiyo. Mwalimu alikuwa anasema hayo wazi bila kupindisha.
Aidha, ni Mwalimu alikuwa mtu wa kwanza kabisa kuishinikiza serikali ikubaliane na mfumo wa vyama vingi, ijapokuwa maoni ya wananchi wengi yalitaka Tanzania iendelee na mfumo wa chama kimoja. Wapo watu walimlaani Mwalimu kwa kushawishi na kuunga mkono haja ya kuwapo kwa mfumo wa vyama vingi nchini, akieleza fursa ambazo zinaweza kupatikana katika mfumo wa vyama vingi. Mwalimu alitunga hadi kitabu kuikosoa serikali na kukisambaza nchini.
Tatu, tujikumbushe hapa. Kwamba eti Msuya alikuwa hazungumzi na vyombo vya habari, na kwa maana hiyo ni sifa njema, na kwa maana hiyo kwa Jaji Warioba kuzungumzazungumza kila mara ni sifa mbaya. Hakumuonyeshi kama mstaafu mwema na mwenye hekima.
Hoja hii inashangaza sana, kama wanaweza kumshangaa na kumsimanga Jaji Warioba, hivi mawaziri wakuu wawili, Edward Lowassa na Frederick Sumaye, watawasema vipi? Mawaziri Wakuu hawa wastaafu mwaka 2015 siyo tu kwamba walikuwa wanaikosoa serikali hadharani, bali walijiengua kwenye Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga na Chama cha Demokrsaia na Maendeleo (CHADEMA).
Hawakujiunga na Chadema tu, Lowassa alipeperusha bendera ya Chadema chini ya mwavuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) akiwania urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Sumaye alikuwa ni msemaji mkuu kabisa katika kampeni hizo. Walitoa dozi kubwa tu katika kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Hawa ni viongozi wastaafu. Hawa walikuwa makada wa CCM wakatoka, wakaenda, ingawa baadaye walirejea CCM. Ukosoaji wao unaweza kupimwa je? Kwamba nao hawakuzungumza na vyombo vya habari? Kwamba hawakuwa na hekima?
Kwa hiyo, kujaribu kumbeza Jaji Warioba kwa kuwa tu anatoa maoni yake ya kutaka kuijenga nchi, ya kutaka mambo yarekebishwe, ya kutaka kujengwa kwa mfumo wa uwajibikaji unaoheshimu haki za raia, ni mbinu mbaya inayotaka kutengeneza taifa la mazezeta. Kwamba kila mtu aimbe mashangilio na kuunga mkono mambo mabaya ambayo hata shetani hayataki. Wanaotaka kutuaminisha katika mfumo na nidhamu ya namna hii hawalitakii mema taifa hili.
Mwisho, taifa lolote linalokimbia mijadala ya wazi, linalotaka mambo yaendeshwe kisirisiri, linalotaka kuziba kila sauti huru, ni taifa lisilotaka kusonga mbele. Ni taifa linalokwepa uwajibikaji. Ndiyo maana haishangazi kuona Jaji Warioba anatazamwa kwa jicho pembe, kama mtu asiyestahili heshima anayopewa na umma, kwa kuwa ni kati ya wakuu wastaafu wachache wasiosumbuliwa na tamaa zozote. Kwake uwajibikaji, utawala wa sheria na haki za wananchi ni mambo muhimu zaidi kuliko ‘bahasha’ nono za kufubaza akili yake timamu. Jaji Warioba ni mwamba.


