Na Mwandishi Wetu
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imethibitisha kuwa Serikali ya Marekani imeiweka Tanzania katika kundi la nchi zilizowekewa vikwazo visivyokamilika vya kuingia nchini humo (partial restrictions and entry limitations), kufuatia changamoto ya baadhi ya raia wa Tanzania kutokuzingatia masharti ya viza.
Taarifa iliyotolewa leo Disemba 17, 2025 na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imeeleza kuwa uamuzi huo ulitangazwa rasmi na Rais wa Marekani, Donald Trump, kupitia mitandao yake ya kijamii mnamo Disemba 16, 2025.
Mbali na Tanzania, nchi nyingine 11 za Bara la Afrika zilizojumuishwa katika utaratibu huo ni Angola, Benin, Cote d’Ivoire, Gabon, Gambia, Malawi, Mauritania, Nigeria, Senegal, Zambia na Zimbabwe.
Kwa mujibu wa Wizara, hatua hiyo imetokana na matokeo ya Ripoti ya Wakaazi Waliopitiliza Muda wa Kukaa (Overstay Report) iliyobainisha kuwepo kwa idadi kubwa ya raia wa Tanzania wanaokaa nchini Marekani zaidi ya muda ulioruhusiwa kisheria na viza zao.
Ripoti hiyo imeonesha kuwa kiwango cha ukaaji wa zaidi ya muda kwa Watanzania ni asilimia 8.3 kwa viza za B-1/B-2 zinazotumika kwa biashara na utalii, huku viza za kundi la F, M na J zinazotolewa kwa wanafunzi, mafunzo ya ufundi na programu za kubadilishanazikionesha kiwango cha ukaaji wa zaidi ya muda cha asilimia 13.97.
Kwa mujibu wa Serikali ya Marekani, viwango hivyo vinazidi wastani unaokubalika chini ya sera zake za uhamiaji, hali iliyosababisha Tanzania kujumuishwa katika kundi la nchi zenye vikwazo vya sehemu vya viza.
Hata hivyo, Serikali ya Tanzania imesema itaendelea kushirikiana na Serikali ya Marekani kupitia njia za kidiplomasia, hususan kati ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania na Wizara ya Nje ya Marekani, ili kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa suala hilo.
Wakati huo huo, Serikali imewataka Watanzania wote wanaosafiri kwenda nchini Marekani kuzingatia kikamilifu masharti ya viza wanazopewa na kuepuka kukaa zaidi ya muda ulioruhusiwa kisheria, ili kusaidia jitihada za kuondoa vikwazo hivyo.


