Na Winfrida Mtoi
KATIBU Mkuu Kiongozi, Balozi Dk. Moses Kusiluka amewataka Maofisa Habari wa Serikali kuhakikisha wanajiimarisha kiutendaji ili kukabiliana na matumizi hasi ya teknolojia ya habari na mawasiliano.
Balozi Dk. Kusiluka ametoa wito huo leo Desemba 17, 2025 wakati akifungua Kikao Kazi cha Kitaifa cha Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais na Maafisa Habari wa Serikali kinachofanyika hoteli ya Johari Rotana, jijini Dar es Salaam.
Amesema ni muhimu kubadilika kutokana na kuishi katika wakati ambao mawasiliano yametawaliwa na teknolojia ambayo ikitumika vizuri ni fursa na ikitumika vibaya ni hatari kwa usalama wa nchi.

“Teknolijia ni fursa kubwa endapo itatumika vizuri lakini pia ni hatari kubwa endapo itatumika vibaya. Watanzania tumeshuhudia jinsi teknolojia ya habari inavyoweza kutumiwa na maadui kuhatarisha usalama wa nchi”
Amesema kupitia kikao hicho, maofisa hao wanatarajiwa kuonesha umahiri mkubwa wa katika tasnia hiyo na kuisaidia serikali kuleta maendeleo kutokana na wingi wao.

“Hapa tupo zaidi ya 500, ni wazi kuwa serikali ndiyo yenye wataalamu wengi wa habari na mawasiliano kuliko taasisi nyingine yoyote nchini. Lakini ukweli ni kwamba bado hatupo vizuri sana katika matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano.
“Hatujafanya kazi nzuri ya kuwaunganisha wananchi na serikali kwa maana yakutoa taarifa sahihi ya mipango na kazi, kutoa ufafanuzi wa haraka inapotokea habari za upotoshaji.
“Aidha hatujafanya vizuri katika kukabiliana na mashambulizi kutoka kwa watu wasioitakia mema nchi yetu. Hivyo tutumie teknolojia ya habari inayoendana na wakati, mazingira ili kuwafikishia wananchi habari sahihi na kwa wakati,” amesisitiza Balozi Dk. Kusiluka.


Naye Mshauri wa Rais, Habari na Mawasiliano. Tido Mhando amesema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa na maono ya kuhakikisha anawezaje kuboresha tasnia ya habari na wameanza muda mrefu kupitia vikao walivyokuwa wanakutana.
Amesema lengo la kuwakutanisha maofisa habari hao ni kutaka wajue ni nini wanachohitaji wakifanye katika maeneo yao.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Bakari Machumu amewahimiza maofisa hao kufanya kazi weledi kwa kuwa mawasiliano serikalini ndio nyenzo ya maendeleo.
Kikao hicho chenye kaulimbiu: “Utu na Mawasiliano Yenye Uwajibikaji” kimeandaliwa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu kwa kushirikiana na Idara ya Habari (Maelezo).


