Na Winfrida Mtoi
NYOTA wa Simba Jonathan Sowah na Allasane Kante wamefungiwa michezo mitano na faini ya Sh 1,000,000 kila mmoja kwa kosa la kufanya vitendo visivyo vya kimichezo wakati wa mechi yao dhidi ya Azam FC.
Sowah amepewa adhabu hiyo kutokana na kumpiga kiwiko mchezaji Himid Mao wa Azam, wakati Kante akimpiga teke kwa makusudi mchezaji Feisal Salum wa timu hiyo.
Wakati huo huo mchezaji Khalid Aucho wa klabu ya Singida BS, amefungiwa michezo mitano na kutozwa faini ya Sh. 1,000,000 kwa kosa la kufanya kitendo kisicho cha kiuanamichezo kwa kumpiga na kumsukuma mchezaji Adam Adam wa klabu ya TRA United.
Kwa mujibu wa taarifa ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania(TPLB), adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 41:21 ya Ligi Kuu kuhusu udhibiti wa wachezaji.
Pia mwamuzi wa kati wa mchezo wa Simba na Azam FC, Abdallah Mwinyimkuu kutoka Singida ameondolewa kwenye orodha ya waamuzi kwa mizunguko mitano kwa kosa la kushindwa kutafsiri vema sheria za mpira wa miguu na kushindwa kuchukua hatua kwa vitendo vya ukiukwaji wa sheria za mpira vilivyofanywa na wachezaji Sowah na Kante katika mchezo huo.
Naye mwamuzi wa kati wa mechi ya Singida na TRA, Alex Pancras kutoka Dar es Salaam amepewa onyo kali kwa kosa la kushindwa kutafsiri vema sheria za mpira wa miguu na kushindwa kuchukua hatua stahiki kwa kitendo cha ukiukwaji wa sheria za mpira kilichofanywa na mchezaji Khalid Aucho.
Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42:1(1.6) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Waamuzi.
Aidha klabu ya Yanga imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 kwa kosa la shabiki wake kuruka uzio na kuingia kwenye eneo la kuchezea (pitch), ambapo shabiki huyo alionekana kufika hadi kwenye goli la timu ya Coastal Union na kuinama kama Ishara ya kutafuta, kuchukua ama kuweka kitu.
Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 47:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.


