KAMA kuna tume ya uchunguzi iliyopata kuundwa nchini kwa jambo mahususi, ikajikuta katika uwanja usio na mipaka, Tume ya Kuchunguza Vurugu za Oktoba 29, 2025 haiwezi kukosekana kwenye orodha hiyo.
Tume hiyo inayoongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania Mohamed Chande Othman iliundwa Novemba 18, 2025 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan. Wajumbe wengine wa Tume hiyo ni Jaji Mkuu Mstaafu Profesa Ibrahim Hamis Juma, Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu Balozi Ombeni Yohane Sefue, Balozi Mstaafu Radhia Msuya, Balozi Mstaafu Jenerali Paul Meela, Inspekta Jenerali wa Polisi Mstaafu, Said Ally Mwema, Balozi Mstaafu David Kapya, na Dk. Stergomena Lawrence Tax aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na pia aliyewahi kuwa Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Aidha, Tume hiyo iliyoundwa chini ya kifungu cha 3 cha sheria ya Tume za Uchunguzi, sura ya 32 kazi zake zilielezwa ni kufanya uchunguzi wa matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea nchini wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 29 Oktoba, 2025.
Miongoni mwa hadidu za rejea ambazo Jaji Chande alizizungumzia Jumatatu wiki Desemba mosi, 2025 alipokutana na wahariri wa vyombo vya habari ni kuchunguza na kubaini chanzo halisi cha yaliyotokea, malengo yaliyokusudiwa na waliopanga kutekeleza vitendo hivyo, madhara yaliyojitokeza ikiwemo vifo, majeruhi, uharibifu wa mali na hasara za kiuchumi zilizojitokeza.
Pia Tume itaangalia mazingira na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na serikali na vyombo vyake katika kukabiliana na vurugu hizo, kisha kupendekeza maeneo yanayohitaji kuimarishwa ili kuongeza uwajibikaji wa viongozi na raia kwa minajili ya kulinda usalama na utawala bora, utawala wa sheria, haki za binadamu na mfumo madhubuti wa majadiliano ya kisiasa na kijamii hadi kufikia maridhiano na kuhakikisha vurugu hizi hazijirudii.
Tume imepewa mamlaka ya kuchunguza jambo lolote ambalo itaona kuwa ni muhimu na linaendana na majukumu yake, kwa maana hiyo, haijafungwa mikono katika kupanua mawanda ya kazi yake kuhusiana na matukio hayo, iwe ni kwenda nyuma zaidi ya siku ya matukio au mbele zaidi.
Wakati Tume ikijipanga kufanya kazi kwa muda wa siku 90 iliyopewa, huku ikiomba ushirikiano kwa watu wote, mwelekeo wa serikali katika suala hili siyo tu unazidi kuikoroga Tume, kama siyo kuingilia moja kwa moja kazi ambazo ziko mbele yake. Jaji Chande alipoulizwa juu ya uwezekano wa Tume yake kuingiliwa, alisema hawajapokea mapendekezo yoyote na wanaanza kazi ‘kwenye karatasi nyeupe’ akimaanisha kutokuwa na shinikizo lolote.
Pamoja na maelezo haya ya kutia moya ya Jaji Chande kwamba Tume yake ni huru, mwelekeo wa viongozi wakuu serikalini umeonyesha dhahiri nia ya kutaka kuelekeza Tume kwenye hitimisho wanalotaka wao.
Kwa mfano, Novemba 25, 2025 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba alikutana na wahariri wa vyombo vya habari na kueleza kwa kina matukio yaliyotokea Oktoba 29 hadi Novemba 3, 2025 kuwa ni uhujumu uchumi. Na alisisitiza kwamba vijana walioshiriki katika matukio hayo walilipwa fedha kutoka nje. Mwigulu alisisitiza kuwa yaliyotokea hayakuwa ni maandamano bali vurugu zenye nia ovu za kuvuruga uchumi wa Tanzania.
Wiki moja baadaye, yaani Desemba 2, 2025 Rais Samia ambaye ndiye aliyeunda Tume hiyo ili imsaidie kazi na kuipa hadidu za rejea, alihutubia taifa kupitia mkutano wa wazee wa Jiji la Dar es Salaam na kusisitiza kuwa yaliyofanyika hayakuwa ni maandamano bali ni vurugu zilizokuwa zimeratibiwa mahususi kuiangusha dola. “Zilikuwa ni vurugu kwa madhumuni maalum,” alisema Rais Samia na kuongeza kuwa “walidhamiria kuiangusha dola.”
Hakuishia hapo tu, katika hotuba ambayo ilijaa maelezo ya kina kuhusu vurugu hizo alisema “lilikuwa jambo la kupangwa. Ni mradi wa uovu… una wafadhili, washitiri na watekelezaji.”
Aidha, Rais alisema kuwa nguvu iliyotumika kukabiliana na vurugu hizo iliendana na tukio lililokuwapo na kuhoji wanaodai kuwa nguvu kubwa kupita kiasi ilitumika walitaka nini kitokee, na kuwauliza kama walitaka dola ianguke. Alieleza wao wameapa kuilinda nchi. Rais alifika mbali na kuwauliza wakosoaji wa mbinu zilizotumiwa na serikali kuwakabili washiriki wa matukio hayo kwa kusema:
“Kama wanavyofanya wao, nasi tutafanya hivyo.” Akimaanisha mataifa ya nje yanayoikosoa Tanzania kwa jinsi ilivyoshughulikia matukio hayo, nao hufanya hivyo wanapokabiliana na vurugu kama hizo huko kwao. Alisema Tanzania kama nchi huru haitapokea maelekezo ya mtu yeyote na kuwauliza “who are you (nyinyi ni nani)” kiasi cha kujipa mamlaka ya kuipangia Tanzania cha kufanya.
Katika hotuba hiyo ya kwanza ya kina kuzungumzia matukio ya Oktoba 29 hadi Novemba 3, 2025 Rais Samia aliainisha makundi makuu manne yanayohusika katika kadhia hiyo. Alitaja kuwa ni taasisi za dini na hakusita kulitaja Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC) alilitaja kuwa chini ya utawala wake wametoa matamko manane. Huku akiwaambia kama hawamtaki iwe ni kwa sababu ya dini yake, au anakotoka au alivyo, wasubiri amalize uongozi wake kwa mujibu wa katiba atakuja mtu mwingine wanayemtaka.
Alitaja kundi jingine kuwa ni la vijana akieleza kuwa wengi walirubuniwa na kuingia katika mkumbo wa maandamano huku wakiwa hata hawajui walichokuwa wanadai. Alisema vijana hao walibebeshwa ajenda ya ugumu wa maisha, ilihali hawajui chochote hasa hali ya kiuchumi ya Tanzania inapolinganishwa na nchi nyingine jirani. Alieleza kuwa vijana wamekosa uzalendo na kuomba wazazi wawafunde vijana wao.
Rais alitaja kundi la tatu lililohusika na vurugu hizo kuwa ni wanasiasa ambao wamekuwa wanaharakati na kwamba kushindwa kwao kuendesha siasa safi ndiko kuliwasukuma kuvuruga nchi siku ya uchaguzi ili kuficha aibu yao. Kundi la nne ni watu walioko nje wanaomezea mate rasilimali za Tanzania, hasa madini adimu ambayo kwa sasa yanahitajika sana ulimwenguni.
Hotuba ya Rais Samia ilibeba mambo mengi ikiwa ni pamoja na onyo kwa mawaziri wake kujiepusha na safari ya mwaka 2030 kwani hatamvumilia yeyote mwenye matamanio ya urais 2030 kwa kutumia fursa katika serikali yake.
Kwa mawanda ya hotuba ya Rais ni dhahiri kwa sasa mtu anawaza kama Tume ya Jaji Chande imebakiwa na nini ambacho viongozi wakuu wa nchi hawajatolea maoni na hitimisho ya kiini hasa cha matukio ya Oktoba 29 hadi Novemba 3, 2025.
Swali linalosumbua mpaka sasa ni kwa nini Rais Samia na hata Waziri Mkuu wake wameshindwa kujizuia kuzungumzia matukio haya ili walau kutoa fursa kwa Tume aliyoiunda yeye mwenyewe kufanya kazi yake? Je, ni kwa kiwango gani Tume hii inaweza kufumba macho na kuziba masikio juu ya haya yaliyosemwa na Rais kwa kina kiasi hicho yasishawishi utendaji kazi wao katika kazi hii waliyopewa?
Je, katika hatua ya aina ya hotuba ya Rais Samia Jumanne wiki hii, ameamua kuwa kocha mchezaji kwa wakati mmoja? Katika tafakari ya namna hii mtu anashindwa kujizuia kuona mlima wenye utelezi ambao Tume ya Jaji Chande inasubiriwa kuupanda ili matokeo ya kazi yake yakonge mionyo ya Watanzania.


