Bado denial inasuta nafsi za wengi, hatuwezi kupona

LEO ni siku ya 23 tangu risasi ya kwanza ilipofyatuliwa na kuua vijana waliokuwa wanaandamana katika miji mbalimbali nchini Oktoba 29, 2025. Baada ya risasi hiyo ya kwanza zilifuata mfululizo wa risasi nyingine zisizo na idadi. Matokeo ya tukio lile lililokuwa linaratibiwa na vijana wa nchi hii, wakitaka kuonyesha hisia zao juu ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu, liliacha maafa makubwa ya kitaifa. Hadi sasa hakuna chombo chochote cha serikali kimeweka hadharani idadi ya watu waliouawa kwa risasi za moto.

Kadhalika, hakuna chombo kimekuwa tayari kueleza walau waliojeruhiwa walikuwa ni watu wangapi. Wala kueleza ni wangapi wangali wanauguza majeraha. Vijana kwa watu wazima walikufa na kujeruhiwa kwa risasi za moto katika kadhia hii. Kwa sura ya matukio yaliyoanza Oktoba 29, 2025 na kuendelea hadi Novemba 3, 2025, yalisababisha maafa makubwa ya uhai, uharibifu mkubwa wa mali za umma na binafsi. Kwa kifupi hadi sasa mioyo ya watu ingali inavuja damu. Machungu ni makubwa mno.

Mpaka sasa mambo makubwa mawili yametokea. Kwanza ni kauli ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ya kutambua kuwako kwa vurugu na mauaji yaliyotokea Oktoba 29; Rais katika hotuba yake ya kufungua Bunge la 13 Novemba 14, 2025, aliwataka wabunge kusimama kwa dakika moja kutambua waliokufa katika vurugu hizo; pia alieleza kuhuzunishwa kwake na tukio hilo, akawapa pole wote waliopoteza wapendwa wao katika kadhia hiyo, akaomba marehemu wapumzike kwa amani, na waliojeruhiwa wapate nafuu mapema. Aliahidi kuunda Tume Huru ya Uchunguzi kuchunguza vurugu hizo.

Jambo la pili, Jumanne wiki hii, yaani Novemba 18, 2025 Rais alitangaza majina ya Tume Huru ya Uchunguzi yenye watu wanane. Tume hiyo inaongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu, Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu Mstaafu Profesa Ibrahim Hamis Juma, Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu Balozi Ombeni Yohane Sefue, Balozi Mstaafu Radhia Msuya, Balozi Mstaafu Jenerali Paul Meela, Inspekta Jenerali wa Polisi Mstaafu, Said Ally Mwema, Balozi Mstaafu David Kapya, na Dk. Stergomena Lawrence Tax aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na pia aliyewahi kuwa Katibu Mtendai wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Moses Kusiluka Jumanne wiki hii, ilisema kuwa Rais ameunda Tume hiyo kwa mamlaka aliyonayo chini ya kifungu cha 3 cha sheria ya Tume za Uchunguzi, sura ya 32 akisema kazi yake ni kufanya uchunguzi wa matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea nchini wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 29 Oktoba, 2025. Taarifa hiyo haikuingia kwa undani juu ya hadidu za rejea za Tume hiyo.

Kwa maana hiyo, hadi sasa ambacho kimewekwa hadharani na serikali kuhusu maafa ya Oktoba 29, ni salamu za pole za Rais na kuundwa kwa Tume Huru ya Uchunguzi.

Wakati haya yakiendelea, na umma ukisubiri kwa shauku kubwa kazi itakayofanywa na Tume hii, bado kuna maswali mengi sana katika jamii. Maswali haya yanajikita katika sura kuu mbili. Moja ni hali ya baadhi ya watu mbali ya Rais, wenye madaraka serikalini kuonyesha hali ya ama kukataa kuwako kwa maafa, mpaka pale Rais aliposema na kuwaomboleza waliouawa na kuwatakia uponyaji majeruhi. Pili, ni kuendelea kutaabika, kuhuzunika kwa watu wengi ambao mpaka sasa wameshindwa kupewa maelezo yoyote juu ya iliko miili ya wapendwa wao, walau wakawazike. Kuna taarifa za baadhi ya familia kuaga picha, kama ishara ya kumaliza misiba ya ndugu zao ambao taarifa walizo nazo zilithibitisha kuwa waliuawa katika kadhia hiyo.

Kwa maana hiyo, bado wapo watu ambao jamaa wanaomboleza. Wana machungu yasiyoelezeka, kwamba siyo tu ndugu zao wamepotea au wameuawa, lakini hata miili ya kuzika hakuna. Ni machungu makubwa mno.

Hali hii ya maombolezo imezidi kuigawa jamii ya Watanzania. Kuna manung’uniko na kutokuridhika kwa hatua ambazo hadi sasa zimechukuliwa katika kadhia nzima ya matukio ya Oktoba 29. Mpasuko huu unaonekana kupanuka.

Katika hali hii, kuna jambo kubwa linatunyemelea kama taifa. Ukisikiliza kauli zinazotolewa na viongozi wa kiimani kuna mgawanyiko na mpasuko mkubwa unaoakisi misimamo na mitazamo ya kiimani juu ya tukio la Oktoba 29. Maudhui ya matamko, walau lile la Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) lililotolewa wiki iliyopita na lile la Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kimtazamo, kimantiki na kimsimamo yanasigana. Hali hii ni ya hatari kubwa.

Siyo nia yangu kuchambua kwa kina kila tamko kati ya haya mawili, ila ni matamko ambayo yanatufikirisha na kwa hakika yanazidi kugawa Watanzania. Kuna dalili zisizopendeza.

Katika hali yoyote ile itoshe tu kusema kuwa tukio la Oktoba 29, 2025 ni tukio baya, la kuhuzunisha ambalo kwa mara ya kwanza limejenga taswira mbaya ya taifa la Tanzania. Ni jambo la kuhuzunisha zaidi kwamba hata baada ya siku hizi 23, yaani wiki tatu ambazo zimekwisha kupita bado ndani ya jamii kumejaa mgawanyiko, hasira, denial na roho zinazowaka kisasi. Hali hii haituashirii mema kama taifa.

Nimesema hapo juu kwamba Rais ameunda Tume Huru ya Uchunguzi, yaweza kuwa ni hatua nzuri. Yaweza kuwa ni mwanzo mwema, lakini kutokuwekwa bayana hadidu rejea za Tume hii, huku wateuliwa wote wakiwa ni wale tu waliopata kuwa na nafasi za kimadaraka serikalini, kunaacha maswali juu ya uhuru na Tume.

Sina lolote la kuwatuhumu wajumbe wa Tume hii, lakini katika kadhia ya Oktoba 29, 2025 kulikuwa na makundi mawili yaliyokuwa yanakinzana. Vijana waliokuwa wanaandamana na baadaye maandamano yale yakageuka kuwa ni vurugu zilizoonyesha makabiliano ya vijana na polisi waliokuwa wanatumia silaha za moto, kuna iweka serikali katika mtihani mkubwa. Kwamba ni kwa jinsi gani inaunda Tume ambayo imejaa ‘watu wake tu’. Kwamba uhuru huu wa Tume ni upi? Je, ni kustaafu kwa wajumbe wake ndiko kunaweza tu kuwa sababu ya kuwa huru?

Ni kwa nini uteuzi wa Tume hii haujapanua wigo na kujumisha watu kutoka nje ya waliopata kuwa ndani ya mfumo wa serikali? Kwani kwenye vyama vya kiraia, taasisi za kijamii, wanasheria wa kujitegemea na wengine wowote ambao hawajawahi kuwa watumishi katika utumishi wa umma, wasingeliweza kuwa na msaada wa kuisaidia serikali katika uchunguzi huu?

Ni dhahiri katika dunia ya sasa kuna uwezekano wa kupima hisia zilizoko ndani ya jamii kwa kufanya utafiti mdogo tu. Mitandao ya kijamii ni nyenzo muhimu, kubwa na ya haraka ya kuwezesha upatikanaji wa taarifa za namna hiyo. Swali la kujiuliza, hivi hata kabla ya kuundwa kwa Tume hii, haikuwezekana kabisa kujua ni nini hasa matarajio ya jamii baada ya ile ahadi ya Rais ya kuunda Tume Huru? Hii denial ndani ya wakubwa wetu itaondolewa na nini? Mpaka wafe wangapi?

spot_img

Latest articles

Watoto mapacha wajinyonga Zanzibar, kisa kazi za ndani

Na Mwandishi Wetu Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba linachunguza tukio la kujinyonga kwa...

Yanga yatua Zanzibar kuitengenezea dozi AS FAR Rabat

Na Winfrida Mtoi Kikosi cha Yanga kimetua visiwani Zanzibar kwa maandalizi ya kuikabili AS FAR...

Rais Samia atangaza Baraza Jipya la Mawaziri, nane watemwa

Tatu Mohamed na Winfrida Mtoi RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan,...

More like this

Watoto mapacha wajinyonga Zanzibar, kisa kazi za ndani

Na Mwandishi Wetu Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba linachunguza tukio la kujinyonga kwa...

Yanga yatua Zanzibar kuitengenezea dozi AS FAR Rabat

Na Winfrida Mtoi Kikosi cha Yanga kimetua visiwani Zanzibar kwa maandalizi ya kuikabili AS FAR...

Rais Samia atangaza Baraza Jipya la Mawaziri, nane watemwa

Tatu Mohamed na Winfrida Mtoi RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan,...