Na Mwandishi Wetu
Kaimu Kocha Mkuu wa timu ya Taifa, Taifa Stars Miguel Gamondi amemrudisha katika kikosi mshambuliaji Kelvin John, anayechezea Aalborg BK ya Denmark ambaye mara ya mwisho kuitwa katika kikosi hicho ilikuwa Machi, 2025.
Kelvin ni kati ya nyota wa Tanzania wanaofanya vizuri nje ya nchi hasa katika ufungaji mabao, hivyo anaungana na wachezaji wengine 22 kujiandaa na mchezo wa kirafiki wa kalenda ya FIFA dhidi ya Kuwait utakaochezwa Novemba 14 jijini Cairo, Misri.
Gamondi ambaye ni Kocha Mkuu wa Singida Bs, pia aliwahi kuhudumu Yanga kwa mafanikio, amepewa majukumu ya kuinoa Taifa Stars baada ya Shirikisho la Soka (TFF) kuvunja mkataba na Hemed Suleiman ‘Morocco’.



