Na Mwandishi Wetu
Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tundu Lissu imeahirishwa leo Oktoba 24 hadi Novemba 3, 2025,.
Kesi hiyo iliyoanza kusikilizwa mfululizo tangu Oktoba 6, 2025 imeahirishwa baada ya upande wa Jamhuri kuomba kuahirisha shauri hilo ili kupisha uchaguzi mkuu ambao upo kwa mujibu wa Katiba.
Awali, mshitakiwa Tundu Lissu, aliiomba Mahakama kutoahiriahwa kwa kesi hiyo na kama Mahakama itakubali ombi la upande wa Jamhuri basi yeye apewe dhamana kwa mujibu wa kifungu 302(3) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA), hadi tarehe iliyopangwa kwenye ratiba ya usikilizaji wa kesi hiyo.
Lissu aliwasilisha ombi hilo leo Ijumaa, Oktoba 24, 2025, mara baada ya Jamhuri kuiomba Mahakama kuahirisha usikilizwaji wa kesi hiyo hadi Novemba 3, 2025, kwa maelezo kuwa mashahidi waliopangwa kutoa ushahidi wao leo wanahusiana na vielelezo vilivyokataliwa wiki hii.

Baada ya kusikiliza ombi la pande zote mbili, Jopo la majaji likiongozwa na Dustan Nduguru limekuja na maamuzi ya kuahirisha kesi hiyo huku wakisema ombi la mshitakiwa kuomba dhamana haliwezekani kwani kesi inayomkabili (Uhaini), haina dhamana.


