MKUTANO Mkuu wa Baraza la Umoja wa Mataifa wa 80 ulimalizika jijini New York, Marekani, wiki iliyopita ambako nchi za bara la Afrika zilikaza kusukuma ajenda yake ya kupata viti viwili vya kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja huo. Hii ni ajenda ambayo kwa muda sasa imekuwa ikisukumwa na nchi za Afrika. Imekuwa ni miongoni mwa ajenda za Umoja wa Afrika kwa Umoja wa Mataifa.
Safari hii, mbali na nchi zinazoitwa Kamati ya Nchi 10 (C -10) ambazo ndizo zinazoongoza harakati hizo – Nigeria, Afrika Kusini, Kenya, Sierra Leone, Senegal, Zambia, Algeria, Equatorial Guinea, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Libya, Tanzania nayo iliendelea kupaza sauti juu ya umuhimu wa kufanyika kwa mageuzi katika mfumo wa Umoja wa Mataifa ikiwa ni pamoja na kuipa Afrika nafasi katika viti vya kudumu vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Kwa sasa nchi zenye viti vya kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja huo ambazo pia huwa na kura ya turufu, ni Marekani, Uingereza, Ufaransa, Urusi na China.
Msukumo huu ni wa umuhimu wa kipekee kwa Afrika ili kuiongezea sauti katika maamuzi mengi makubwa yanayohusu ulimwengu. Mara nyingi, nchi zenye kura ya turufu zimekuwa ndizo zinazoamua mwelekeo wa masuala mengi yanayojadiliwa na kuamuliwa kwa kura katika Umoja huo. Maazimio mengi kama hayataungwa mkono na nchi zenye viti vya kudumu katika Baraza la Usalama, ni sawa na kusema kuwa hayawezi kupita.
Nimetafakari kwa kina msukumo huu wenye umuhimu wa kipekee kwa bara la Afrika ambalo kwa miaka mingi, limepuuzwa na kunyimwa fursa inayostahili kulingana na ukubwa wake na idadi ya watu inayobeba. Kwa sasa Afrika inakadiriwa kuwa na watu bilioni 1.4. Kwa maana hiyo siyo haki wala haipendezi kuona kuwa wanachama wa Umoja wa Mataifa sawa na asilimia 18, kwa miaka 80 sasa tangu kuundwa kwa chombo hicho, wao ni watu wa kuburuzwa tu. Kimantiki, Afrika yenye watu bilioni 1.4 (18%) inaizidi Amerika Kusini na Kaskazini yenye watu bilioni 1.05 (13%) na Ulaya yenye watu milioni 746 (9%). Inazidiwa na bara la Asia tu lenye watu bilioni 4.7 sawa na asilimia 58. Ni halali kwa Afrika kutafuta nafasi ya kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Hata hivyo, pamoja na matamanio haya mazuri na harakati zinazosukuma ajenda hii, bado kuna swali gumu la kujibiwa na Waafrika wenyewe. Hili, ni je, Afrika inavyojiangalia inafahamu changamoto za kiusalama ambazo zimo ndani ya mipaka yake. Ukiacha suala la ni nchi zipi zitastahili kupewa hadhi hiyo ya ujumbe wa kudumu kwenye Baraza la Usalama, kuna changamoto kubwa sana ya kiusalama inayokabili bara hili. Sasa hivi ni kama vita ama ya wenyewe kwa wenyewe au baina ya mataifa au vurugu za ndani ya nchi za Afrika vimeota mizizi. Na kwa bahati mbaya, ni kama nchi hizi zimeshindwa kutatua migogoro hii kwa miongo kadhaa sasa.
Vyanzo vya habari mbalimbali duniani vinaonyesha kwamba zaidi ya nchi 10 barani Afrika zimo vitani. Hivi ni vita kamili, kama vita vya wenyewe kwa wenyewe, au mizozo kati ya mataifa, uasi wa kijeshi, n.k. Katika orodha hii zipo Sudan ambayo ipo kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya Jeshi la Sudan (SAF) na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF), pamoja na makundi mengine ya waasi.
Ipo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambao kwa miongo kadhaa imekuwa kwenye migogoro ya ndani na makundi mbalimbali ya waasi, pamoja na mgogoro wa kuvuka mipaka na Rwanda kupitia waasi wa M23; kuna Ethiopia yenye migogoro mingi ya ndani – katika majimbo ya Oromia na Amhara ambayo imekuza makundi ya kivita ya kikabila na ya kieneo; ipo Sudan Kusini ikisumbuka katika migogoro ya ndani inayojiainisha katika makundi ya kikabila baina ya Rais
Salva Kiir na kabila lake la Dinka dhidi ya Makamu wake, Riek Machar wa kabila la Nuer. Pia kuna makundi mengine mengi yenye silaha na viongozi wa mitaa yamejiunga katika mapambano.
Kuna migogoro ya Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) ambayo ni ya ndani nayo ikihusu makundi ya waasi; upo wa Mali unaohusisha makundi ya wanamgambo wa Kiislamu, uasi wa kijeshi na mapinduzi ya serikali; kuna mgogoro wa Burkina Faso unaohusu uasi wa ndani, na mashambulizi ya wanajihadi; kuna mgogoro wa Nigeria wa miongo kadhaa sasa wenye sura ya uasi wa Kiislamu kama Boko Haram na vurugu za kikabila na za kijamii.
Libya nako hali ni tete huku ikiendelea kukumbwa na mgawanyiko wa kisiasa, udhaifu wa taasisi za serikali, na upanuzi wa makundi ya kijeshi na ya kigaidi. Raia wanakumbwa na madhara makubwa, ikiwa ni pamoja na ukiukaji wa haki za binadamu na vifo vya wahamiaji. Kwa kifupi, tangu kuuawa kwa Kiongozi wao, Muammar Gaddafi Oktoba 20, 2011 wakati wa Mapinduzi ya Libya ya Arab Spring, mpaka leo nchi hiyo haijapata kuwa na utulivu wa uhakika. Hapa hatujaigusa Somalia ambayo inaishia katika hali ya utata mkubwa kiusalama au Chad ambayo inakumbwa na hali ya usalama tete inayochangiwa na migogoro ya ndani, vitisho vya kigaidi, na changamoto za kibinadamu. Raia wanakumbwa na athari kubwa, na serikali inahitaji juhudi za pamoja na msaada wa kimataifa ili kurejesha amani na utulivu.
Orodha hii ya migogoro, vurugu, vita na kukosekana kwa utulivu wa kuaminika na wa kutosha kwa zaidi ya nchi 10 za Afrika, ni moja ya mambo ambayo kwa hakika yanafaa kuifikirisha sana AU. Kwamba ni kwa kiwango gani bara hili, pamoja na ukubwa wa idadi yake ya watu, nchi zake zinamudu kujiendesha, kujisimamia na siyo tatizo la amani ndani ya nchi zao na duniani kwa ujumla.
Swali kuu la kujiuliza kwa zaidi ya miongo sita sasa, ni kwa nini bara la Afrika limekwama kabisa kutatua changamoto za kiusalama ndani ya bara hilo? Jaribu kutafakari mgogoro wa DRC ambao unaleta pamoja nchi mbili wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), lakini haziwezi kuaminiana. Zinashutumiana, kutuhumiana na kudhalilishana mbele ya jumuiya ya kiataifa. EAC imeshindwa kabisa kusaidia nchi hizi jirani kumaliza mzozo ambao umeota mizizi mashariki mwa DRC.
Kwa mfano, serikali ya DRC ambayo kiuhalisia imeshindwa kutawala eneo lote la nchi hiyo kwa uhakika, ni miongoni mwa nchi zinazotaka kufikiriwa kuwa mjumbe wa kudumu wa Baraza la Umoja wa Mataifa. Au serikali ya Nigeria ambayo kwa miongo kadhaa sasa inatolewa jasho na Boko Haram nayo inataka kiti hicho; Afrika Kusini nayo ambayo Weusi wameamua kuunda makundi ya wanamgambo wa kuwasaka na kuwaua wageni kutoka nchi za Kiafrika kwa kisingizio chochote, nao wanataka kiti hicho.
Katika tafakari yoyote, mtu anayesikiliza ajenda ya viti vya kudumu kwenye baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa Afrika, anapaswa kujiuliza utayari wetu uko je? Isivyo bahati, ajenda hii inasukumwa katika nyakati ambazo mataifa mengi ya Afrika siyo tu yanahuzunisha watu wake, bali tawala zake nyingi zimezidi kuzama katika mashaka na kushindwa kuwahakikishia wananchi wake usalama. Yafaa mataifa ya Afrika kujihoji kwa kina zaidi juu ya kuendelea kutetereka kwa amani na utulivu katika bara hilo huku chombo muhimu na kikubwa kama AU kikishindwa kufanya lolote la maana kukomesha hali hii.