Na Winfrida Mtoi
Timu za Simba na Yanga leo zimeondoka nchini leo kwa ajili ya kwenda kucheza michezo yao raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Yanga imeelekea Angola, kuikabili Wiliete ya nchini humo Septemba 19, 2025, Uwanja wa 11 de Novembro, huku Simba ikitarajiwa kutua Botswana ambapo itacheza na Gaborone United Septemba 20, 2025 kwenye dimba la Obed Itani Chilume.

Vigogo hao wa soka nchini wenye maskani yao Kariakoo jijini Dar es Salaam, wameondoka baada ya jana kucheza mechi ya Ngao ya Jamii na Yanga kutwaa ubingwa huo.
Baada ya mechi hizo zitarejea nchini kujiandaa na michezo ya marudiano ambapo Yanga na Wiliete zitarudiana Septemba 27, 2025, Benjamin Mkapa. Simba itarudiana na Gaborone United Septemba 28,2025 kwenye uwanja huo huo.