INEC, Msajili wa Vyama wanaweza kutupa uchaguzi huru?

WASHABIKI wa mpira wana msemo wao kwamba kila timu ishinde mechi zake. Kwa maana hii, kila timu inawajibika kujiwekea mikakati ya kujenga kikosi chake ili kiwe na uwezo wa kimpira wa kushinda mechi zake zote. Hali hii hapana shaka inahusu kuwajengea wachezaji stamina, nidhamu na maarifa ya kimpira ya kukabiliana na timu pinzani. Hii kwa Shirikisho la Mpira wa Soka la Ulimwengu (FIFA) huitwa ‘Fair Play’ kwa Kiswahili twaweza kusema ni Mchezo wa Haki.

Mchezo wa haki hauwezi kupatikana kwa mfano kwa timu pinzani kutumia mbinu chafu za nje ya uwanja. Ndiyo maana katika kuchezesha mpira kwa mfano, refa (mwamuzi) huchaguliwa katika mazingira ambayo yanamtambulisha na kumuonyesha ni mtu asiyefungamana na mojawapo ya timu shindani. Matumizi mabaya ya rasilimali – hasa fedha, na hata mahaba ama dhidi ya timu mojawapo au kuibeba nyingine, ni mambo yanayopingwa na kupigwa vita sana.

Yakijengwa mazingira rafiki, ya haki, yasiyoibeba timu yoyote, hujenga mwamko mkubwa wa ushindani na hamasa ya wapenda soka kuhamasika na kushiriki kwa wingi katika mchezo husika. Mchezo wa soka ni burudani, lakini pia ni uchumi. Siku hizi soka ni shughuli ya ukwasi uliopindukia. Umebadili maisha ya mamilioni ya watu, wachezaji na familia zao, wamiliki wa vilabu vya mpira na hata nchi kwa ujumla wake.

Kwa mfano mtandao wa Soccer Worldwide unakadiria kuwa kwa mwaka wa 2025 mapato yanayotokana na shughuli za mpira wa miguu (soka) ni kiasi cha Dola za Marekani bilioni 59.1 duniani kote. Ulieleza kwamba katika fedha hizo, vyombo vya habari kwa maana ya haki za matangazo ya mpira, vitaingiza kiasi cha Dola za Marekani bilioni 43.2. Hizi kwa fedha za Tanzania ni matrilioni mengi sana sawa na bajeti ya taifa ya miaka mitatu. Kwa maana hiyo, soka ni uchumi, ni maisha ni maendeleo ya mchezaji mmoja mmoja, klabu na taifa kwa ujumla wake.

Hapa Tanzania huu ni mwaka wa’ kipute’, yaani wa uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani. Uchaguzi unaweza kuangaliwa kama shughuli ya kiuchumi. Wapo watu wachache wanaodhani uchaguzi ni shughuli ya kisiasa tu, inayohusu wanasiasa tu na vyama vyao. Watu hawa, kwa bahati mbaya, wana uwezo wa kuona maana na nafasi ya soka katika maisha yao, lakini siyo siasa ambayo ndiyo imeshika ustawi na hatima ya maisha yao. Wanachangia klabu zao kwa kununua jezi na vitu vingine vinavyotambulisha klabu wanazoziunga mkono, bila kujali ni za hapa nchini au kokote duniani. Soka kwao kwa sasa hivi ni imani ya pili baada ya imani zao za kidini.

Katika muktadha huu, inakuwa ni vigumu mno kuelewa kwamba ni kwa nini hapa nchini hamasa, amsha amsha za kisiasa, ari na ushabiki wa kisiasa hauna nguvu kama ilivyo kwenye soka kwa mfano? Au ni kwa nini vuguvugu la kisiasa nchini limedorora sana kiasi cha kushindwa kuelewa kwa mfano kama huu ni mwaka wa uchaguzi mkuu wa kutafuta rais, wabunge na madiwani? Ni nini hasa kinakwaza mwamko, hamasa na amsha amsha ya kisiasa kiasi cha kuonekana kwamba pamoja na ukweli kwamba mwaka huu ni wa uchaguzi mkuu, kwa watu wengi ni mwaka wa kawaida tu kwao, wala hawasumbuki?

Binafsi nimepata fursa ya kupitapita mikoa kadhaa katika majukumu ya kuwajengea waandishi wa habari uelewa wa kuripoti habari za uchaguzi mkuu kwa weledi. Nimezungumza na waandishi wa viwango tofauti, wakongwe kwa wachanga. Kitu kikubwa ambacho kinaonekana kwao ni kimoja, kwamba umma umekaa kana kwamba mwaka huu siyo wa uchaguzi mkuu. Hakuna amsha amsha mitaani. Hakuna vuguvugu kubwa na hamasa ya kuona kwamba watu wengi wanausubiria kwa hamu kubwa. Ni kweli kwa takwimu watu wengi wanaonekana kuwa wamejiandikisha.

Taarifa za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) inasema kuwa, waliojiandikisha kupiga kura ni watu 37,655,559. Idadi hii ikitazamwa kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, ni wastani wa asilimia 60.9 ya Watanzania wote. Tanzania ina wakazi milioni 61.7. Kwa kuangalia taarifa za kitakwimu tu katika uandikishaji, inaweza kutoa sura ya hamasa. Hata hivyo, historia inaonyesha kwamba uandikishaji wa wapigakura huchukuliwa kama fursa kwa baadhi ya watu kupata vitambulisho kwa kuwa kitambulisho cha mpigakura ni miongoni mwa nyaraka zinazokubalika kama utambulisho katika sehemu mbalimbali nchini. Kama mahakamani, benki, kwenye usajili wa masomo nk.

Kwa muktadha huu, yafaa kujihoji kwamba watu hawajui maana ya uchaguzi wa kuwapata viongozi wa mamlaka ya dola kweli? Hawajui maana ya mamlaka na nafasi ya rais na baraza lake la mawaziri ambao hupatikana miongoni mwa wabunge? Au hawajui nafasi na mabaraza ya madiwani katika maeneo ya halmashauri zao? Kwamba wananchi hawajui kwamba vyombo hivi, yaani Ofisi ya Rais na Baraza lake la Mawaziri, Mabaraza ya Madiwani ndiyo vyombo vinavyoamua jinsi rasilimali za nchi zinatumika? Kwamba ujenzi wa miradi ya maendeleo – kama barabara, madaraja, reli, viwanja vya ndege, miradi ya maji, ujenzi wa hosipitali, shule na nyingine nyingi, upatikanaji wa fedha zake hutegemea vyombo hivyo?

Kama wananchi wana hamasa ya klabu zao za mpira kiasi cha kufanya soka kuwa mojawapo ya shughuli yenye ukwasi mkubwa duniani, ni nini kinawazuia wananchi kuelewa kwamba wana nafasi kubwa ya kuamua juu ya hatima ya nchi yao kupitia sanduku la kura? Yaani wananchi hawana hamu na rasilimali za nchi yao na jinsi ya kuwa na uamuzi juu ya matumizi yake?

Hapo juu nimesema kwamba FIFA ina taratibu, kanuni na miongozo dhabiti ya kuhakikisha kwamba timu bora ndiyo inashinda. Inashinda siyo kwa mbinu za porini, bali kwa mikakati inayoheshimu na kuzingatia uchezaji wa haki kwa kila timu. Haki inatamalaki bila upendeleo. Yeyote anayeonekana kukwaza haki katika mchezo kutotamalaki, huwekwa kando, na mara kadhaa tumeshuhudia wavunjaji wa misingi ya haki katika mchezo wakipigwa rungu zito la adhabu ikiwamo kufungiwa maisha.

Sasa kwa upande wa kipute chetu hapa nchini, ni kwa jinsi gani vyombo vilivyopewa wajibu wa kuwahakikishia Watanzania wanapata uchaguzi huru, wa haki na wa kuaminika wanatekeleza wajibu huo bila upendeleo, inda wala kupindisha kanuni? Mwaka huu kwa mara ya kwanza INEC itasimamia uchaguzi mkuu. Ni kwa kiwango gani uwepo wa INEC unawahakikishia Watanzania kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu utakuwa huru, wa haki na wa kuaminika? Je, ni kwa kiwango gani Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inatekeleza wajibu wake, ili kila chama kijione kinalindwa, kuheshimiwa na kutohujumiwa kwa ‘mbinu za porini’ ambazo zinaondoa kabisa kile katika soka kinaitwa ‘Fair Play’ kwao?

Yamkini vyombo hivi vya kimamlaka katika mchakato mzima wa uchaguzi, utendaji wao wa ‘Fair Play’ ndiyo kitu pekee tu kitakachosaidia taifa hili kufanya uchaguzi huru, wa haki na wa kuaminika. Vinginevyo, tutaendelea kuona yasiyopendeza katika muktadha wa uchaguzi huru na haki.

spot_img

Latest articles

Polisi wawili washikiliwa kwa tuhuma za wizi wa mbolea

Na Mwandishi Wetu Jeshi la Polisi mkoani Songwe linawashikilia watu saba, wakiwamo askari polisi wawili...

Wamiliki silaha haramu wapewa siku 60 kuzisalimisha

Na Mwandishi Wetu Jeshi la Polisi Tanzania limetangaza msamaha wa kutokushtakiwa kwa wananchi wote wanaomiliki...

Msanii aiombea michango Tembo Warriors, yakusanya sh. 270,000 pekee

Na Winfrida Mtoi Msanii wa Bongo Flava, Frank Humbuchi maarufu Foby amewataka watanzania na wasanii...

Timu ya Taifa kriketi ya wanawake kusaka tiketi ya kucheza Kombe la Dunia

Na Mwandishi Wetu Timu ya Taifa ya wanawake ya mchezo wa kriketi ya Tanzania inatarajiwa...

More like this

Polisi wawili washikiliwa kwa tuhuma za wizi wa mbolea

Na Mwandishi Wetu Jeshi la Polisi mkoani Songwe linawashikilia watu saba, wakiwamo askari polisi wawili...

Wamiliki silaha haramu wapewa siku 60 kuzisalimisha

Na Mwandishi Wetu Jeshi la Polisi Tanzania limetangaza msamaha wa kutokushtakiwa kwa wananchi wote wanaomiliki...

Msanii aiombea michango Tembo Warriors, yakusanya sh. 270,000 pekee

Na Winfrida Mtoi Msanii wa Bongo Flava, Frank Humbuchi maarufu Foby amewataka watanzania na wasanii...