Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
BENKI ya CRDB kupitia mbio za hisani za CRDB Bank Marathon msimu wa sita imefanikiwa kukusanya Sh bilioni 2, ambapo kati ya fedha hizo Sh milioni 450 zimeelekezwa kusaidia makundi mbalimbali ya jamii yenye uhitaji maalumu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Abdulmajid Nsekela, alisema msaada huo umeelekezwa kwenye Hospitali ya CCBRT (Sh milioni 100) kusaidia wakinamama wenye ujauzito hatarishi, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) (Sh milioni 100) kugharamia upasuaji wa watoto wenye matatizo ya moyo, na Sh milioni 250 kwa ajili ya uwezeshaji wa vijana.

“Kwa miaka sita mfululizo tumekuwa tukifanya mbio hizi za hisani, lakini mwaka huu tumeyafanya kwa upekee sambamba na maadhimisho ya miaka 30 ya CRDB, tukipanua wigo wake ndani na nje ya Tanzania,” alisema Nsekela.
Akizungumza wakati wa tukio hilo, Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson, aliipongeza CRDB Bank Foundation kwa ubunifu wa kutumia michezo kama njia ya kuunganisha jamii na kusaidia wenye uhitaji, akisema mbio hizo ni mfano wa vitendo vya huruma vinavyogusa maisha ya wengi.
Kwa upande wake, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi, alisema marathon hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwa jamii ikiwemo kukuza afya, mshikamano wa kijamii, na kutoa fursa za kiuchumi kwa vijana kupitia zawadi nono na ajira.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa, alisema mbio hizo msimu huu pia zimefanyika nje ya Tanzania, zikiwemo Lubumbashi, DRC ambapo zilikusanywa dola 70,000 kwa ajili ya hospitali ya Jeshi la Ruashi, na Bujumbura, Burundi ambako walikusanya Faranga milioni 175 kusaidia bima ya afya kwa zaidi ya watu 58,000 wasiojiweza.
Katika matokeo ya mbio, washindi wa kilometa 42 walikuwa Joyloyce Kemuma (Kenya) upande wa wanawake na Abraham Kiptum (Kenya) upande wa wanaume. Upande wa kilometa 21, wanawake waliongozwa na Catherine Syokau (Kenya) huku wanaume mshindi akiwa Joseph Panga (Tanzania). Washindi wa kilometa 10 walikuwa Silia Ginoka (Tanzania) kwa wanawake na Boayi Maganga (Tanzania) kwa wanaume.