Na Mwandishi Wetu
Rais wa klabu ya Yanga, Injinia Hersi Saidi ameshindwa kupenya katika uteuzi wa awali wa wagombea ubunge Jimbo la Kigamboni kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku wadau wengine wa michezo wakiwamo wachambuzi wa soka, Shafii Dauda na Jemedali Said wakipita.
Injinia Hersi jina lake halikuwepo kati ya wagombea sita walioteuliwa kwa jimbo la Kigamboni ambao ni Ponela Matei, Habib Mchange, Allan Sanga, Henjelewe, Ally Mandai na Francis Elias.

Kwa upande wa Jemedali ametishwa na Chama hicho katika Jimbo la Mtama, mkoani Lindi akiwa pamoja na Nape Nnauye, Jabir Chilumba na Meta Nahonyo wakati Shafii Dauda akiteuliwa Jimbo la Temeke, jijini Dar es Salaam akiwa na Mariam Nassoro, Dorothy Kilave, Bernard Mwakyembe, Fadhil, Leah Mwampishi na Mussa Ntulia.
Wanamichezo wengine walipita katika uteuzi huo wa awali, ni Msemaji wa Azam Fc, Hasheem Ibwe, Jimbo la Mwanga, wakati Revocatus Chiponda ‘Baba Levo’ akipenya Jimbo la Kigoma.
Majina ya wateule katika majimbo mbalimbali wa CCM, yamewasilishwa kwa waandishi wa habari leo Julai 29,2025 jijini Dodoma na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa chama hicho, Amos Makalla.