Na Mwandishi Wetu
CHAMA Cha Ukombozi wa Umma (CHAUMA) kimeendelea kuvunja ngome ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) baada ya Sigrada Mligo kujiunga rasmi na chama hicho.
Sigrada kabla ya kujiunga Chauma, alikuwa ni Katibu Mwenezi wa Baraza la Wanawake Taifa (BAWACHA) ingawa pia alishawahi kushika nyadhifa mbalimbali akiwa Chadema ikiwemo Udiwani Viti Maalumu.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa kadi ya Chauma na Katibu Mkuu wa chama hicho, Salum Mwalimu, Sigrada amesema ameamua kuondoka Chadema baada ya kudaiwa kutumika na anataka kukiua chama hicho alichokitumikia kwa jasho na damu tangu mwaka 2011 akiwa chuoni.

“Haikuwa kazi rahisi kufanya maamuzi haya, nimetafakari sana baada ya kupigwa na kuumizwa vibaya nje ya mkutano huku baadhi ya viongozi wakiaminika ndio waliopanga njama hizo na hatimaye kumtorosha mtuhumiwa.
“Pia hawakuhusika katika matibabu yangu hata kidogo, huku Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakachukua nafasi hiyo kwa kunikodishia gari ya wagonjwa na kunipatia Shilingi 1,500, 000 za matitabu ambazo baadhi nilizitumia kulipa deni la hoteli ambalo Chadema walikuwa wakidaiwa na baadhi nililipia gharama za matibabu.
“Chadema nimekifanyia mengi ikiwemo ujenzi chama kwa fedha zangu, wageni wote wa chama waliokuwa wakifika Njombe,Mimi nilikuwa nawagharamia kila kitu lakini leo thamani yangu haionekani, natuhumiwa kukihujumu chama na kutaka kukiua sasa kabla hakijafa naamua kujiondoa ili maneno yao yasitimie nikiwepo, ukweli nimepoteza uhalali wa kuwa chadema kutokana na kauli hizo.

“Pia nimefadhili operesheni mbalimbali cha kujenga chama kwa fedha zangu binafsi na nimetumia zaidi ya Sh. milioni 15 kuhakikisha majimbo matatu ya Mkoa wa Njombe yanashiriki mchakato wa uchaguzi wa ndani ya chama na hakuna anayeweza kubisha kwani kumbukumbu zipo,” amasema.
Hatua hiyo ya kujiengua Chadema kwa kada huyo inakuja miezi kadhaa baada ya kudaiwa kujeruhiwa na mmoja wa walinzi wa Chadema wakati wa kikao cha ndani kilichoongozwa na Makamu Mwenyekiti, John Heche, Machi 25, 2025, mkoani Njombe.